HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 19, 2020

MKATABA WA BILIONI 70.5 KUPELEKA MAJI BUTIAMA WASAINIWA

 

 

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) na Meneja
wa Kampuni ya UNIK Construction Company Nchini Tanzania, He Yifeng
wakisaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa sh bilioni 70.5 wa kutoa maji
Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na
Butiama.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto)
akibadilishana mkataba wa ujenzi wa mradi wa kupeleka maji kwenye
maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na Butiama na Meneja wa Mkandarasi
Kampuni ya UNIK Construction Company, He Yifeng.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza wakati
wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa
Bilioni 70.5 wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya
Wilaya za Musoma Vijijini na Butiama.
Baadhi ya wadau waliohudhuria hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi
wa mradi wa kupeleka maji kwenye maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini
na Butiama. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji wa
Wizara ya Maji, Mhandisi Abbas Pyarali.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa tatu kushoto
waliokaa) katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na wawakilishi
wa Mkandarasi Kampuni ya Kampuni ya UNIK Construction Company mara
baada ya kusaini mkataba wa kupeleka maji Butiama na Musoma Vijijini.


Na Mohamed Saif, Musoma.

SERIKALI imesaini mkataba na Mkandarasi Kampuni ya UNIK Construction
Company ya Lesotho kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji
Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na
Butiama wenye thamani ya Shilingi Bilioni 70.5.

Akizungumza hapo jana Mkoani Mara wakati wa hafla
ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi
Anthony Sanga alisema mradi unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo ambao ni Benki ya Kiarabu ya
Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa. Maendeleo wa Saudia (SFD)

“Mradi tuliosaini leo thamani yake ni Shilingi Bilioni 70.5 na ni
fedha za Serikali ya Tanzania; nina kila sababu ya kumshukuru Rais
wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea fedha hizi kwa ajili ya
kuhakikisha unajengwa,” alisema Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alibainisha kwamba mradi utajengwa kwa Miezi 24 na
alimtaka Mkandarasi kuhakikisha anaukamilisha ndani ya muda huo hasa
ikizingatiwa kwamba maandalizi muhimu yamekamilika na hakuna sababu ya
kuchelewa.

Alisema kwa kawaida hua baada ya kusaini mkataba mkandarasi anapewa
mwezi mmoja kujipanga lakini kwa sasa utaratibu ni kwamba anapaswa
kuanza kazi mara moja hasa ikizingatiwa kuwa tayari anaelewa
anachostahili kukitekeleza.

“Serikali ya Awamu ya Tano ni ya vitendo, hakuna sababu ya Mkandarasi
kutumia mwezi mzima kujipanga kwani tayari hadi hivi anasaini mkataba
anaelewa kinachotakiwa kufanywa; maelekezo ya Serikali ni kwamba mradi
ukamilike kwa wakati,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alisema katika ujenzi wa miradi, Serikali inazingatia
vigezo vikubwa vitatu ambavyo ni ubora, gharama nafuu na muda wa
utekelezwaji wake yaani unapaswa ukamilike kwa wakati na hivyo
alimtaka Mkandarasi kuhakikisha vigezo hivyo vinazingatiwa.

“Kwa vigezo hivi nilivyovitaja tayari kigezo cha gharama nafuu
tumekizingatia na sasa tumebakiza hivyo viwili kwahiyo ninamsisitiza
Mkandarasi kuhakikisha anavizingatia na itakua vyema endapo
atakamilisha mradi kabla ya muda huo wa miezi 24,” alielekeza Mhandisi
Sanga.

Alisema ujenzi wa mradi ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John
Pombe Magufuli pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa wananchi wa
Butiama na Musoma Vijijini na kwamba Wizara ya Maji itahakikisha
hakuna kikwazo kitakachochelewesha utekelezwaji wake.

“Wananchi wanausubiri kwa hamu kubwa mradi huu kama ambavyo
walivyoahidiwa na viongozi wetu, sasa sisi kama Wizara ya Maji katika
hili hatutokubali uzembe wa aina yoyote ile, tunachotaka ni kuona
unakamilika kwa wakati na kwa ubora utakaoakisi gharama halisi ya
fedha itakayotumika,” alisisitiza Mhandisi Sanga na huku akiwataka
watendaji wa wizara yake kubaki Mkoani Mara ili kuhakikisha Mkandarasi
anakabidhiwa eneo la ujenzi wa mradi ndani ya Saa 24 na kuanza kazi.

Aidha, Mhandisi Sanga alimtaka Mkandarasi kuwapa kipaumbele cha ajira
wananchi wa maeneo ya mradi hususan kwenye shughuli ambazo wanazimudu
na pia aliwaasa wananchi watakaopata fursa kuhakikisha wanakuwa
waadilifu na wanashirikiana na mkandarasi kuulinda mradi.

“Ninaamini zipo shughuli nyingi ambazo wananchi wa maeneo ya mradi
wanaweza kufanya hivyo sitarajii kusikia hawapati fursa hizo na pia
sitarajii kusikia wananchi wanakwamisha mradi kwa namna yoyote ile,”
alisema Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga aliwakumbusha wananchi kuzingatia maelekezo ya Rais
Magufuli ya kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji kwa manufaa yao na
kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya UNIK Construction Company Nchini
Tanzania, He Yifeng alimhakikishia Mhandisi Sanga kwamba watatekeleza
mradi kwa kuzingatia mkataba na maelekezo ya Serikali.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji kutoka Wizara ya
Maji, Mhandisi Abbas Pyarali alisema eneo lenye mtandao wa majisafi
litaongezeka kufikia asilimia mia moja kwa miji ya Mugango, Kiabakari
na Butiama na kwamba zaidi ya wakazi 165,000 watapata huduma ya maji
kwa asilimia mia moja.

Mhandisi Pyarali alitaja maeneo yatakayonufaika kwenye awamu ya kwanza
ya mradi kuwa ni Miji ya Mugango, Kiabakari, Butiama na vijiji vya
Kwibara, Nyamisisye, Kiabakari, Singu, Mwanzaburiga, Kyawazaru,
Kamugegi, Kyatungwe, Ryamugabo, Bumangi, Bisarye, Tiring'ati, Butiama,
Rwamkoma, Buturu, Nyang’oma, Mayani, Katalyo na Tegeruka.

Halfa ya utiaji saini ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo
Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini, Mkuu wa Wilaya ya Butiama,
Annarose Nyamubi, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Vijijini, Dkt. Vicent Naano
na viongozi mbalimbali wa Kata na Vijiji vitakavyonufaika na mradi.

Utiaji saini wa mradi huo mkubwa wa maji ni wa kwanza kutekelezwa
tangu kuanza kwa  kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano chini
ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad