HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 14, 2020

RAFIKI YANGU KING KIKI ALINIIMBIA NYIMBO

 Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv

Mjumbe wa kamati ya Utendaji wa Yanga Dr Tobias Lingalangala amemtembelea na kumjulia hali rafiki yake wa muda mrefu Mwanamuziki Mkongwe King Kiki anayeumwa kwa muda kidogo.

Baada ya kufika na kumjulia hali, Lingalangala amewaomba watanzania kuendelea kumuombea mzee wao ili arejee katika majukumu yake ya kazi.

Lingalangala amemtembelea na kumjulia rafiki yake huyo wa muda mrefu ambaye amefanyiwa upasuaji wa Pingili za shingo na kwa sasa anaendelea vizuri.

Akizungumza baada ya kumaliza kumjulia hali, Lingalangala amesema rafiki yake huyo alimuimbia wimbo ulioitwa nimepigwa ngwala baada ya kumuelezea kisa cha ukweli kilichomtokea.

Amesema, mbali na hilo urafiki wao ni muda mrefu sana na katika kipindi chote ambacho Mzee King Kiki anaumwa hakuwa nchini na ndiyo maana baada ya kurejea aliamua kuja kumjulia hali na kutoa pole kwa familia nzima.

Aidha, Lingalangala amesema King Kiki ndiye msanii wa kwanza aliyeanza kuimba nyimbo za kuhamia Dodoma na tungo nyingi sana zenye kuonesha uzalendo kwa nchi yetu.

Kwa upande wa familia ya Mwanamuziki Mkongwe   Mzee King Kiki, Mke wake Costansia Gabriel amewashukuru watanzania kwa maombi wanayoendelea kumuombea mzee wao pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefika nyumbani kumjulia hali Mzee wao.

Pia,  Costansia amesema wamepokea salamu za Pole kutoka kwa Rais Dkt John Pombe Magufuli nazo wanapenda kusema wanashukuru sana na ana imani dua za watanzania wote zitamrejesha King Kiki katika hali yake ya zamani.

"Kwa sasa anaendelea vizuri, baada ya kupata ushauri wa Daktari kuwa Mzee wetu anahitajika afanyiwe upasuaji watu wengi walinitisha sana ila nilimuachia mungu na kwa sasa kama unavyoona anaendelea vizuri,"

"Hospitali walituambia Kiki anasumbuliwa na uti wa mgongo ila  Pingili za Shingo ndizo zilisagika sana na hapo walimchoma sindano ya kuua viungo vyote ila maendeleo yake ni mazuri kwa sasa," amesema Costansia.

Taarifa ya kuugua kwa King Kiki ilianza muda kidogo kusambaa katika mitandao ya Kijamii ambapo Familia ilitoka na kutolea ufafanuzi wa jambo hilo.
Mjumbe wa kamati ya Utendaji wa Yanga Dr Tobias Lingalangala akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumtembelea rafiki yake wa muda mrefu Mzee King Kiki ambaye anaugua kwa muda mrefu na kuwataka watanzania kumuombea ili arejee katika kazi zake za kila siku.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad