HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 23, 2020

KAMPUNI YA JATU PLC YAORODHESHWA KWENYE SOKO LA HISA LA DAR ES SALAAM


 
*Jitihada za JPM zatajwa kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha.

IMEELEZWA kuwa utendaji na uongozi madhubuti wa Rais Dkt. John Joseph Magufuli katika kuweka mikakati na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu kisera imechochea ukuaji wa sekta ya fedha hususani katika masoko ya mitaji na uchumi kwa ujumla nchini.

Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama leo jjini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa hisa za JATU Plc katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE.)"Nawashukuru wadau wa sekta ya fedha kwa kuhudhuria hafla hii ya kuorodheshwa kwa hisa za Kampuni ya JATU Plc kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, huu ni uthibitisho kwamba sekta ya fedha ina wadau wengi wanaounga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli iliyoweka mazingira wezeshi na kiutendaji yenye malengo ya kukuza uwekezaji kupitia masoko ya mitaji." Ameeleza.

Amesema kuwa, hisa zapatazo 2,164,349 kutoka Kampuni ya JATU Plc zimeorodheshwa katika soko la hisa leo na hiyo ni kutokana na matokeo chanya ya elimu na ufahamu waluoupata viongozi waanzilishi wa JATU Plc ambao ni vijana wa kitanzania waliotumia fursa hiyo baada ya kushiriki shindano la masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini.

Aidha ameeleza, Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) itaendeleza majukumu yake ya kusimamia, kuratibu na kuendeleza sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini.

"Sekta hii husaidia Kampuni katika upatikanaji wa mitaji kwa muda mrefu na kuorodheshwa kwa JATU Plc katika soko la hisa la Dar es Salaam ni matokeo chanya ya kufanikisha azma ya Serikali ya awamu ya tano katika kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo ili kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo na kuifanya sekta hiyo kuwa ya biashara." Amesema.

Pia ameipongeza JATU Plc kwa kujidhatiti kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali pamoja na kutoa ajira zipatazo 10,650 wakiwemo wanawake kwa asilimia kubwa na kuwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa uaminifu ili kuweza kufikia azma ya maendeleo.

Vilevile ameielekeza bodi ya Wakurugenzi na uongozi wa Kampuni ya JATU kuhakikisha kunakua na ongezeko la thamani katika uwekezaji wao ili waweze kunufaika kiuchumi ikiwemo kupata gawio la faida.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE,) Moremi Marwa amesema, Kampuni ya JATU Plc imeorodhesha hisa zake 2,164, 349 zenye ukubwa wa mtaji wa thamani ya shilingi bilioni moja na milioni 83.

Amesema, malengo kwa kuorodhesha hisa za JATU ni kuwezesha wanahisa wa JATU Plc kuendelea kununua na kuuza hisa zao katika bei inayoamuliwa na soko.

"Ninaupongeza uongozi wa JATU kwa kufikia hatua hii na kuwapa imani Wana hisa wake kupitia shughuli wanazozifanya ikiwemo kilimo na masoko, hii ni hatua kubwa katika kuelekea maendeleo...Tunaamini kupitia hatua hii ajira zitazalishwa kwa wingi pamoja na kuongeza pato la Serikali kupitia kodi." Ameeleza.

Amesema Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA,) imekuwa ikishiriki katika kuzileta sokoni kampuni za namna hiyo, na hadi leo Kampuni 28 ikiwemo JATU zimeorodheshwa huku Kampuni 27 zilizoorodheshwa awali zikiwa na ukubwa wa mtaji wa thamani ya shilingi trilioni 15, huku trilioni 9.1 zikitokana na kampuni za ndani.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa JATU Peter Isare, alisema kampuni hiyo inayomilikiwa na wanawake,vijana pamoja na watu wa kipato cha kati, wamejiunga pamoja na kushirikiana katika miradi mikubwa ya kilimo, viwanda, masoko na Tehama.

Alisema hadi kufikia mafanikio hayo ya kusajiliwa soko la hisa, wameweza kuanzisha mashamba katika hekari zipatazo 17,678 yaliyopo katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Tanga, Manyara, Singida,Ruvuma,Morogoro na Njombe.

Alisema hatua ya kampuni hiyo kuorodheshwa katika soko la hisa kutazidi kuiwezesha kushiriki katika miradi mikubwa zaidi na hivyo kuisaidia kubadirisha maisha ya maelfunya watanzania.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama (wa tatu kulia) akipiga kengele kuashiria kufunguliwa kuanza kuuzwa kwa hisa za kampuni ya JATU PLC katika Soko la Hisa la Dar Es Salaa (DSE),kwenye hafla fupi ya kuorodheshwa kwa hisa za Kampuni ya JATU Plc katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE.)

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama akizungumza mbele ya Waandishi wa habari na Wageni waalikwa mbalimbali waliofika kwenye hafla hiyo leo jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla fupi ya kuorodheshwa kwa hisa za JATU Plc katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE.)
Baadhi ya Wageni waalikwa wakifuatilia hafla hiyo fupii iliyofanyika leo jijini DarAfisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE,) Moremi Marwa akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari na wageni waalikwa waliofika kwenye hafla fupi ya kuorodheshwa kwa hisa za Kampuni ya JATU Plc kwenye soko la hisa la Dar es Salaam


Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya JATU Plc Peter Isare akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari na Wageni waalikwa mbalimbali wakati wa kampuni hiyo ikiorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam,Isare alisema kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na wanawake,vijana pamoja na watu wa kipato cha kati, wamejiunga pamoja na kushirikiana katika miradi mikubwa ya kilimo, viwanda, masoko na Tehama.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad