HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 5, 2020

WIKI YA WAWEKEZAJI DUNIANI YAANZA RASMI LEO, MAMLAKA KUWAJENGEA UWEZO WATANZANIA KUFAHAMU UMUHIMU WA FURSA ZILIZOPO

 

 Na Mwandishi Wetu ,Michuzi TV


MAMLAKA ya Masoko ya Uwekezaji wa Mitaji ya Masoko na Dhamana imeanza wiki ya kimataifa ya Uwekezaji Duniani ambapo itatumia maadhimisho hayo kuendelea kuelimisha Umma wa Watanzania kuhusu kutambua fursa zilizopo na jitihada zinazoendelea za masoko ya mitaji na kuweka mazingira bora, shirikishi na endelevu ya kisera, sheria na utendaji.

Juhudi hizo zinalenga kukuza Uwekezaji kupitia masoko ya mitaji, hivyo kuchochea kwa uchumi nchini Tanzania huku ikielezwa kwamba mpaka sasa Uwekezaji katika masoko ya mitaji ni Sh.trilioni 27 ambapo uwekezaji katika hisa ni Sh.trilioni 15 ,hati fungani ni Sh.trilioni 11.5 na mifuko ya Uwekezaji wa pamoja ni Sh.Bilioni 500.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 5,2020 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu Mamlaka ya masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA,Nicodemus Mkama wakati akizungumzia Wiki ya Kimataifa ya Maadhimisho ya Wawekezaji Duniani kwa mwaka 2020 yenye kauli mbiu inayosema ambapo kauli mbiu inasema kuongeza uelewa na kulinda maslahi ya wawekezaji katika masoko ya mitaji.

Amefafanua kuwa Wiki ya Wawekezaji Duniani inaadhimishwa Kimataifa kwa kuratibiwa na Taasisi ya ushirikiano wa mamlaka za Usimamizi wa Masoko na Mitaji Duniani ambayo kwa kifupi inajulikana kwa IOSC na kwamba pamoja na majukumu mengine IOSC imeweka kanuni zenye vigezo vya kimataifa vya Usimamizi wa masoko na mitaji Duniani ili kuwezesha nchi mbalimbali kusimamia na kuratibu sekta ya masoko na mitaji kwa lengo la kuepusha athari za utandawazi kea kuzingatia vigezo vya Kimataifa na ushirikiano kati ya nchi wanachama.

"Kwa mantiki hiyo IOSC inaratibu shughuli za wiki ya maadhimisho hayo Duniani kwa lengo la kuongeza uelewa umuhimu wa elimu ya wawekezaji kwa umma na kulinda maslahi ya wawekezaji kwa kutumia njia na mbinu mbalimbali. Aidha kushiriki katika shughuli hiyo kunawezesha wadau mbalimbali katika sekta ya masoko ya mitaji kufanya kazi kwa pamoja katika nchi zao na Kimataifa.

"Katika kutekeleza azma hiyo CMSA inaadhimisha wiki hii kwa kushirikiana na na wadau mbalimbali katika masoko ya mitaji na ndio maana wanawaona Mfuko wa Uwekezaji wa pamoja wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu ,pia wapo Soko la hisa pamoja na watendaji katika masoko ya mitaji na kampuni ambazo zimepewa leseni kutoka Mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana.

"Kwa hiyo tunaanza rasmi leo kuadhimisha wiki hii hadi Ijumaa kwa lengo kuu moja kuwa na programu ambazo zitaongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masoko ya mitaji ili kuwezesha kuongeza Uwekezaji na kulinda maslahi ya wawekezaji, hivyo kuongeza mchango wa sekta ya masoko ya mitaji katika kukuza uchumi nchini,"amesema.

Ameongeza kuwa shughuli ambazo zitafanyika katika wiki ya maadhimisho hayo zitajumuisha kutoa elimu kwa wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa masoko ya mitaji katika uchumi, bidhaa mbalimbali zinazotolewa katika masoko ya mitaji, namna ya kupata mitaji kupitia masoko hayo,jinsi ya kushiriki kuwekeza katika masoko ya mitaji.

"Programu hiyo inalenga kuongeza bidhaa za kuwekeza na kuongeza matumizi ya masoko katika upatikanaji wa mitaji katika shughuli za uchumi na kupanua wigo wa Uwekezaji.Tukio hili ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa mamlaka wa miaka mitano ambao pamoja na mambo mengine tunapanga kuendeleza masoko ya mitaji Tanzania ikiwa pamoja na kutoa elimu ya masoko ya mitaji na dhamana kwa makundi mbalimbali,"amesema. 

Pia mkakati huo unalenga kujenga uwezo watendaji lakini na kuongeza uelewa wa umma kuhusu fursa na manufaa yanayopatikana kwa kuwekeza katika masoko ya mitaji huku akifafanua wawekezaji na washiriki katika masoko ya mitaji wanahitaji kupata uelewa wa kutosha kuhusu masoko ya mitaji na namna ya kushiriki katika hatua muhimu ya kuwawezesha kulinda maslahi yao na kufanya uwekezaji endelevu na hilo ni jukumu mojawapo la mamlaka hiyo kuhakikisha wanatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa sheria.

"Tukizingatia kwa sasa hivi Tanzania inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda ,mahitaji ya mitaji kwa shughuli za uchumi yanaongezeka , kwa hiyo ni dhahiri kujenga uwezo na ushirikiano wa pamoja kama wadau wakuu katika sekta ya masoko ya mitaji kuwezesha wahitaji wa mitaji kupata fedha hizo katika sekta hiyo kuongeza wigo wa kuwekeza Umma wa Watanzania.

"Ikumbukwe masoko ya mitaji yanatumika kukuza uchumi wa nchi kwa kuwezesha shughuli za uchumi kukua, kampuni kupata mitaji na kuongeza nafasi za ajira, kuongezeka kwa kodi stahiki za Serikali na kuwezesha Serikali kuboresha huduma za jamii na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kwa jamii nzima kwa ujumla,"amesema.

Hata hivyo amesema mpaka sasa uwekezaji katika masoko ya mitaji ni trilioni 27 ambapo uwekezaji katika hisa ni trilioni 15 ,hati fungani ni trilioni 11.5 na mifuko ya Uwekezaji wa pamoja ni Bilioni 500."Kwa hiyo mnaweza kuona kwa kiasi gani sekta hii ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.

"Elimu ya uwekezaji na uelewa wa masoko ya mitaji kunawezesha wananchi kwa ujumla kuepuka kushiriki katika fursa za uwekezaji ambazo sio halali na wenye udanganyifu kwani siku za karibuni kumekuwepo na wimbi kubwa kwa umma kutapeliwa na kushiriki kwenye danganyifu ,hivyo kwa kutumia maadhimisho hayo tutaendelea kutoa elimu Umma kuhusu sekta hii na umuhimu wa ushiriki wao." 
Afisa Mtendaji Mkuu Mamlaka ya masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA,Nicodemus akizungumza na kuzindua wiki ya kimataifa ya Uwekezaji Duniani mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar,ambapo CMSA itatumia maadhimisho hayo kuendelea kuelimisha Umma wa Watanzania kuhusu kutambua fursa zilizopo na jitihada zinazoendelea za masoko ya mitaji na kuweka mazingira bora, shirikishi na endelevu ya kisera, sheria na utendaji. 
Baadhi ya Wageni waaliakwa mbalimbali waliofika kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa Wiki ya kimataifa ya Uwekezaji Duniani inayoratibiwa na MAMLAKA ya Masoko ya Uwekezaji wa Mitaji ya Masoko na Dhamana (CMSA) hapa nchini. 
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mifuko ya Uwekezaji wa pamoja (UTT-AMIS,Simon Migangala akieleza mbele ya Wanahabari leo jijini Dar, namna watakavyoshiriki kutoa elimu kuhusu Mifuko ya uwekezaji wa pamoja kwa Wadau mbalimbali katika Wiki ya kimataifa ya Uwekezaji Duniani inayoratibiwa na MAMLAKA ya Masoko ya Uwekezaji wa Mitaji ya Masoko na Dhamana (CMSA) hapa nchini. 
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam,Brighton Kinemo akieleza mbele ya Waahabari leo jijini Dar, namna watakavyoshiriki  kutoa elimu kuhusu soko la hisa kwa Wadau mbalimbali katika Wiki ya Kimataifa ya Uwekezaji Duniani inayoratibiwa na MAMLAKA ya Masoko ya Uwekezaji wa Mitaji ya Masoko na Dhamana (CMSA) hapa nchini.
Mwenyekiti wa chama cha Watendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (TSEBA),Bwa,Gerase Kamugisha akizungumza mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani),leo jijini Dar namna watakavyoshiriki wiki ya Kimataifa ya Uwekezaji Duniani inayoratibiwa na MAMLAKA ya Masoko ya Uwekezaji wa Mitaji ya Masoko na Dhamana (CMSA) hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad