Na Marco Maduhu Shinyanga.
Shirika
la Investment in Children and their Societies (ICS) limeungana na
Serikali mkoani Shinyanga kuzindua mpango mkakati wa kutokomeza matukio
ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ambao utadumu kwa muda wa miaka
mitano, ili kusiwepo tena na matukio hayo mkoani humo zikiwemo mimba na
ndoa za utotoni.
Mpango
huo umezinduliwa jana katika Kata ya Segese halmashauri ya Msalala
wilayani Kahama, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani
Shinyanga, likiwamo Shirika la ICS, AGAPE, Rafiki SDO, WFT,Mtandao wa
Kijinsia Tanzania TGNP, UN WOMEN, UNFPA na KOICA.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab
Telack, amesema Serikali ya mkoa huo ni ya kwanza hapa nchini kati ya
mikoa 26 , kuzindua mpango wake mkakati wa kutokomeza matukio ya ukatili
dhidi ya wanawake na watoto.
“Tumezindua
mpango huu mkakati wa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake
na watoto, ambao utadumu kwa muda wa miaka mitano, kuanzia (2020-2025)
kwa kuonyesha dira ya mkoa, na kubainisha changamoto zilizopo katika
mkoa wetu ambazo ni chanzo cha matukio haya na kuzifanyia kazi,”amesema
Telack.
“Mashirika
yote yasiyo ya kiserikali katika utekelezaji wao wa miradi ya mpango
mkakati wa kitaifa wa Serikali wa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya
wanawake na watoto MTAKUWWA, watautumia mpango huu ambao tumeuzindua
leo na kuwa kama dira yao,”ameongeza.
Aidha
amesema kazi ya kuandaa mpango huo umefanywa na viongozi wa Serikali
mkoani Shinyanga, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo mkoani humo,
likiwamo Shirika la ICS, Women Fund Tanzania (WFT) ,Rafiki SDO, pamoja
na AGAPE, ambapo pia wameshiriki kufadhili uzalishaji wa nyaraka za
vitabu na uzinduzi wa kitabu hicho cha mpango mkakati.
Ameitaka
jamii ya mkoa wa Shinyanga, kuachana na matukio ya ukatili dhidi ya
wanawake na watoto, pamoja na kuacha kuendekeza mila potofu ambazo ni
kandamizi zilizopitwa na wakati.
Amesema
dhamira ya mkoa huo ni kuona kunakuwepo na usawa wa kijinsia kwenye
nyanja zote, zikiwemo shughuli za kiuchumi, pamoja na watoto wa kike
kuwa sawa kimasomo na wa kiume, na kuacha tabia ya kuwaozesha ndoa za
utotoni na kuzima ndoto zao.
Naye
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Sifuni Msangi, ameipongeza Serikali ya mkoa wa
Shinyanga, kwa kuzindua mpango wake mkakati wa kutokomeza matukio ya
ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ambao ni moja ya utekelezaji wa
MTAKUWWA, ambao umelenga ifikapo mwaka 2025 matukio hayo ya ukatili yawe
yamepungua.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Investment in Children and their
Societies (ICS) Kudely Sokoine, ambao ni miongoni mwa wadau wakubwa
walioshiriki kuandaa mpango mkakati wa mkoani Shinyanga wa kutokomeza
matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, amesema wao wataendelea
kuutumia mpango huo katika kutekeleza miradi yao ambayo tayari shughuli
hizo wanazifanya ndani ya jamii.
Amesema
ili kuwa na Taifa zuri, lazima kuwepo na usawa wa kijinsia, na ndio
maana Shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kwa kushirikiana na Serikali
pamoja na mashirika mengine, kupambana kutokomeza matukio hayo ya
ukatili ndani ya jamii dhidi ya wanawake na watoto.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akizungumza kwenye uzinduzi wa
kitabu cha mpango mkakati wa Serikali mkoani Shinyanga wa kutokomeza
matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Katibu
tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela, akizungumza kwenye uzinduzi
wa mpango mkakati wa Serikali mkoani humo wa kutokomeza matukio ya
ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akimkabidhi kitabu cha mpango huo
mkakati wa Serikali mkoani Shinyanga wa kutokomeza matukio ya ukatili
dhidi ya wanawake na watoto, Mkurugenzi mkazi kutoka shirika la umoja wa
mataifa na idadi ya watu (UNFPA) Dr. Willfred Ochani.
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akimkabidhi kitabu cha mpango huo
mkakati wa Serikali mkoani Shinyanga wa kutokomeza matukio ya ukatili
dhidi ya wanawake na watoto, Mkurugenzi mkazi kutoka Shirika la
maendeleo la korea Koica Kyucheol Eo.
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akimkabidhi kitabu cha mpango huo
mkakati wa Serikali mkoani Shinyanga wa kutokomeza matukio ya ukatili
dhidi ya wanawake na watoto, Makamu mwakilishi wa mashirika
yanayojihusisha na usawa wa kijinsia (UN WOMEN) Julia Broussard.
Awali
mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akiingia uwanjani tayari kwa
kuzindua kitabu cha mpango huo mkakati, akiwa na mkuu wa wilaya ya
Shinyanga Jasinta Mboneko, pamoja na mkuu wa wilaya ya Kshapu Nyabaganga
Taraba.
Na Marco Maduhu- Shinyanga.
No comments:
Post a Comment