MJUMBE wa
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Watanzania wana kila sababu ya kumchagua Rais Dkt. John Pombe Magufuli
katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu kwa sababu ni kiongozi
makini, shupavu, mbunifu na mwenye uwezo wa kusimamia vizuri rasilimali za
Taifa kwa manufaa ya wananchi wote.
Amesema katika
kipindi cha miaka mitano ya awamu ya kwanza ya uongozi wake, Rais Dkt. Magufuli
amefanya mambo mengi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini na
yamewanufaisha Watanzania wote wakiwemo na wakazi wa wilaya ya Siha mkoani
Kilimanjaro bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Ameyasema hayo
leo (Jumanne, Septemba 8, 2020) alipokuwa akimuombea kura Rais Dkt. Magufuli,
mgombea ubunge wa jimbo la Siha Dkt. Godwin Mollel na wagombea udiwani kwa
tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Matadi
kata ya Ndemet wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro.
Amesema
Watanzania wanatakiwa wamchague Rais Dkt. Magufuli ili aweze kuwaongoza katika
kusimamia vizuri matumizi ya rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo na
kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini. Amesema Tanzania ni nchi
tajiri yenye uwezo wa kuwaletea wananchi wake maendeleo bila ya utegemezi,
hivyo wachague viongozi makini kwa manufaa ya Taifa.
“WanaSiha wote
nimekuja hapa kwenu leo nina kazi moja tu ya kumuombea kura mgombea wa nafasi
ya urais kupitia CCM, Rais Dkt. Magufuli ambaye ni kiongozi imara, mzalendo na
mchapakazi, mgombea ubunge wa jimbo la Siha Dkt. Mollel na wagombea udiwani
wote wa CCM katika wilaya hii. Ikifika siku ya kupiga kura tuhakikishe
tunawachagua.”
Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa lazima wananchi waamini kwamba uongozi unatoka kwa
Mwenyezi Mungu na Rais Dkt. Magufuli ameletwa na Mwenyezi Mungu, hivyo
amewaomba wampe ridhaa ya kuongoza katika kipindi cha miaka mitano mingine ili
aendeleze kazi za maendeleo alizozianza.
“Nawasihi
inapofika siku ya kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu tunapotumia haki ya msingi ya
kidemokrasia, tukamchague Rais Dkt. Magufuli kwa sababu ni kiongozi anayejali
maslahi ya Watanzania wote na ni kiongozi anayeweza kujua nchi inawakulima,
wafanyakazi na wafanyabiashara ambao kila mmoja anatakiwa afanye shughuli zake
kwa uhuru bila ya kusumbuliwa.”
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi wa Siha kuwa
Serikali itayarudisha mashamba yote ya Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro
(KNCU) yanayomilikiwa kinyemela na watu wachache kwa manufaa yao binafsi
“Kuna watu
wamejimilikisha mahekari ya mashamba ya KNCU ambayo ni mali zenu,
nawahakikishia tutawanyang’anya na kuyarudisha kwenu ili atakayelima alime,
atakayefuga afuge”
Amesema KNCU ni
mali ya wananchi (wanaushirika) na kwamba Serikali imefanya kazi kubwa ya
kurudisha hadhi ya ushirika katika kipindi cha miaka mitano, ikiwa ni pamoja na
kuwafikisha mahakamani waliohusika kufanya ubadhirifu katika vyama hivyo na
itaendelea kurejesha mali zote kwa wananchi ili wafanyie shughuli za maendeleo.
Akizungumzia
upatikanaji wa nishati ya umeme wilayani Siha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kati
ya vijiji 60 vilivyopo Siha vijiji vyenye umeme ni 58 na viwili tu ndio havina
umeme na kwamba navyo vitaunganishwa umeme, amewaomba wakazi wake waendelee
kuwa na subira.
Amesema Rais
Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa
gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika
vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Rombo. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni
sh. 27,000 tu.
Pia Waziri Mkuu
amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala fomu za
maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo
zote zimeshabebwa na Serikali yao.
No comments:
Post a Comment