Wanahabari wekezeni na NHIF- RC Mwanza - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 14, 2020

Wanahabari wekezeni na NHIF- RC Mwanza

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela akizindua rasmi mpango wa huduma za matibabu kwa waandishi wa habari nchini. Mpango huu unahusisha waandishi wote na watajiunga kupitia vyama vyao.


Na Grace Michael, Mwanza

SERIKALI imewataka waandishi wa habari nchini kufanya uwekezaji katika afya zao kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao umeweka mfumo rasmi kwa ajili ya kuhudumia kada ya wanahabari nchini.

Mwito huo umetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela wakati wa uzinduzi wa mpango wa huduma za matibabu kwa waandishi wa habari jijini Mwanza.

“Tukio hili la leo ni kubwa na ni la kihistoria kwa kada ya wanahabari kutokana na changamoto zilizopo juu ya upatikanaji wa huduma za matibabu, nafahamu mazingira wanayofanyia kazi hivyo mpango huu utakuwa ni suluhisho kubwa la kuwapa amani wakati wote wanapotekeleza majukumu yao,” alisema.

“Niseme tu kwamba waandishi tuacheni ubahiri hasa katika suala hili ambalo linahusu afya zetu moja kwa moja, mchango ambao umewekwa na NHIF kwa kundi lenu ni nafuu sana ikilinganishwa na gharama za matibabu kwa sasa, wote tutambue kuwa mtaji mkubwa wa kila mmoja wetu ni afya njema na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Alitumia fursa hiyo pia kupongeza uongozi wa NHIF kwa kuona umuhimu wa kuweka utaratibu wa kuwapa huduma za matibabu waandishi wa habari hivyo akawaomba wadau wote wakiwemo viongozi kwa nafasi zao kuhakikisha agenda ya bima ya afya inawafikia wananchi wote ili kila mmoja awe ndani ya mfumo huu wa bima ya afya.

“Tusiiachie NHIF peke yake kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa bima ya afya, wadau wote wakiwemo viongozi na kila mmoja kwa nafasi yake tuhamasishe ili wananchi wote kwa ujumla wawe katika utaratibu mzuri na Ilani ya uchaguzi ya mwaka huu 2020 imeweka wazi juu ya bima ya afya kwa wote , NHIF kwa upande wao wamefanya jitihada kubwa za kuweka utaratibu wa kila kundi kuwa na mfumo wa kujiunga na huduma za matibabu na wanastahili pongezi kubwa,’ alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela akizungumza katika mkutano huo.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula alisema kuwa “Mpango huu ni upendeleo mkubwa kwenu wanahabari kutokana na hali halisi ya gharama za matibabu kwa sasa hivyo tuhakikishe tunalipa kipaumbele sana suala hili na kujiunga mara moja, jambo hili tusiliwekee mjadala wowote zaidi ya kuchukua hatua ya kujiunga,” alisema.


Aliwaomba wanahabari hao kuweka nguvu kubwa katika kuelimisha wenzao na jamii kwa ujumla ili dhana ya bima ya afya ieleweke kwa kila mwananchi.

Kwa upande wa Rais wa Umoja wa Waandishi wa Habari Tanzania, Bw. Deogratius Nsokolo aliwaomba waandishi wa habari ambao hawajajiunga na mpango huu watumie fursa hii kujisajili katika kipindi hiki cha kuanzia sasa hadi mwezi Novemba ili waweze kunufaika na huduma za matibabu.


“Madhara yanayotokana na kukosa bima ya afya kwa waandishi yameonekana wazi hivyo kwa fursa hii ni vizuri kila mwandishi ajitoe kuhakikisha anajiunga na NHIF, wenzetu wa Mfuko wametuunganisha waandishi wote nchini kupitia mpango huu wa huduma za matibabu kwa kundi la wanahabari hivyo ni vyema sasa tukatumia fursa hii na kuachana na dhana ya kulalamika pale changamoto za ugonjwa zinapotokea,” alisema.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula akizungumza.

Alisema kuwa idadi ya waandishi waliojiunga ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya waandishi ambao hawako kwenye utaratibu wa bima ya afya hivyo akazigiza klabu za waandishi wa habari nchini kuweka utaratibu rahisi utakaowawezesha waandishi kujiunga na kutumia fursa hii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema mpango wa huduma za matibabu kwa wanahabari ni suluhu kwa changamoto zinazojitokeza wakati wanapopatwa na ugonjwa.

“Ugonjwa ni dharula huja bila taarifa, tumeshuhudia wengi wakiingia kwenye umasikini kwa kuuza mali zao hivyo kwa kuweka mpango huu watawekeza kwetu na watakapougua watapatiwa huduma bila ya usumbufu wowote, utaratibu uliopo ni waandishi kujiunga na Bima ya Afya kupitia vyama vyao na sio wao kuja mmoja mmoja tumefungua dirisha la usajili kwa muda wa miezi mitatu kuanzia sasa hivyo naomba watumie muda huu kuhakikisha wanajiunga na kwa upande wetu tumejipanga vilivyo kuwahudumia waandishi wa habari,” alisema Bw. Konga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad