

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa
na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu,
Abdulrahman Kinana ambaye aliwaomba wananchi wa Arusha wampigie kura,
Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Wabunge na Madiwani wa CCM katika mkutano
wa kampeni za CCM uliohutubiwa na Waziri Mkuu kwenye uwanja wa Relini
jijini Arusha

Mgombea ubunge wa CCM katika
Jimbo la Arusha Mrisho Gambo (kulia) akikumbatiana na Philemon Mollel
(MONABAN) mmoja wa watia nia waliowania uteuzi wa CCM katika kugombea
jimbo hilo . Walikuwa katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mjumbe
wa Kamti Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye uwanja
wa Relini jijini Arusha, Septemba 5, 2020. Monaban alitamka hadharani
kuwa hana kinyongo na Gambo na kwamba atashiriki kumpigia kampeni.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa
na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
2020-2025 mgombea Ubunge wa CCM katika Jimbo la Arusha, Mrisho Gambo
katika mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Relini jijini Arusha

Wananchi wa jiji la Arusha
wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa
Relini, . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………
*Asema lengo ni kuhakikisha Watanzania wanapata ajira
MJUMBE wa Kamati
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya utalii nchini kwa
kusimamia ipasavyo mikakati ya kukuza vivutio ili kuhakikisha Watanzania
wengi wakiwemo wakazi wa jiji la Arusha hususani vijana wananufaika kwa
kupata ajira.
Amesema Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeweza
kupata mafanikio mbalimbali katika sekta ya utalii yakiwemo kuongeza
idadi ya watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi kufikia 1,510,151
mwaka 2019, ambapo amewaomba wananchi wandelee kuiamini Serikali yao.
Aliyasema
hayo jana jioni (Jumamosi, Septemba 5, 2020) alipohutubia mkutano wa
kampeni uliofanyika katika uwanja wa Relini jijini Arusha baada ya
kumuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge jimbo la
Arusha, Mrisho Gambo na wagombea udiwani wa CCM.
“Sekta ya
utalii ina umuhimu mkubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
wananchi hususani kwa vijana kwa sababu vijana wengi wameajiriwa na
kujiajiri kupitia sekta ya madini. Serikali inawahakikisha kwamba
itaendelea kuboresha mazingira ili kuweza kuvutia watalii wengi zaidi
kuja nchini.”
Alisema
kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali katika sekta
hiyo mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini yameongezeka kutoka
Dola za Kimarekani milioni 1,901.95 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za
Kimarekani milioni 2,612.99 mwaka 2019.
Waziri Mkuu
alisema mafanikio yote hayo yanatokana na uongozi thabiti na makini wa
Rais Dkt. Magufuli, hivyo amewaomba wana Arusha na Watanzania kwa ujumla
kumchagua tena ili aweze kutekeleza mikakati mingine ya kuongeza wigo
wa utalii aliyoianzisha nchini.
“Ndugu
wanaArusha na Watanzania wote sina shaka kwamba mtakubaliana na ombi
langu la kuwataka tumchague tena Rais Dkt. Magufuli kwa sababu mnapenda
maendeleo na kwa Tanzania mtu atakayewaletea maendeleo si mwingine bali
ni Dkt. John Pombe Magufuli tujitokeze kwa wingi kumpigia kura.”
Akizungumzia
kuhusu Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 alisema inaielekeza
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kutekeleza mikakati mbalimbali ya
kuboresha sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kukuza wigo wa bidhaa na
mazao ya utalii.
Ilani
imeelekeza Serikali ihakikishe inaongeza idadi ya watalii na kufikisha
watalii 5,000,000 kwa mwaka ifikapo 2025 na kuongeza mapato kutoka Dola
za Kimarekani bilioni 2.6 mwaka 2020 hadi Dola za Kimarekani bilioni 6.0
mwaka 2025.
Pia
kushirikisha sekta binafsi na kuandaa wataalam wa ukarimu na kuwatambua
wataalam wenye ujuzi na weledi unaohitajika katika utoaji wa huduma za
utalii ili kukuza sekta hiyo na kuongeza ajira kwa wananchi na pato la
Taifa kwa kubuni na kutekeleza mikakati ya kuweka mazingira wezeshi ili
sekta binafsi na umma zishiriki kikamilifu katika uwekezaji wa utalii.
Kadhalika,
Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu suala la bima ya afya, ambapo alisema
Serikali iweka mikakati Madhubuti inayowawezesha wananchi kutibiwa ikiwa
ni pamoja na kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambapo wananchi
wanachangia kiasi kidogo na Serikali inawaongeza na kuwawezesha kutibiwa
bure wao na familia zao.
Pia, Waziri
Mkuu aliongeza kuwa utaratibu mwingine ni kupitia Mfuko wa Bima ya Afya
(NHIF) ambao ni maalumu kwa ajili ya watumishi wa umma kuchangia kiasi
kidogo kupitia mishahara yao na mpango huo unawawezesha kutibiwa bure,
hivyo hakuna tatizo la huduma ya bima ya afya nchini. Amewataka wananchi
wasikubali kupotoshwa na waendelee kuiamini Serikali yao.
Aidha, katika
ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 imeilekeza Serikali kuimarisha mfumo wa
bima ya afya nchini ikiwamo mifuko ya bima za afya (NHIF na CHF) ili
kufikia lengo la serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote.
No comments:
Post a Comment