HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 24, 2020

DITOPILE AZINDUA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA MRIJO, AFUNGUKA MAFANIKIO YA SERIKALI SEKTA YA AFYA

 

Charles James, Michuzi TV
KAZI ya kutafuta ushindi wa Chama cha Mapinduzi CCM kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu imeendelea katika Kata ya Mrijo wilayani Chemba kwa Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile kuzindua kampeni za Udiwani na kunadi Sera za chama hicho.

Ditopile amezindua kampeni kwenye kata hiyo ambapo mgombea wake ni Abdallah Suti ambapo amemuombea kura mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, mgombea Ubunge wa Jimbo la Chemba, Mohammed Monni na mgombea Udiwani.

Akizungumza katika mkutano huo, Ditopile amesema kwa kipindi cha miaka mitano serikali ya CCM inayoongozwa na Dk John Magufuli imepiga hatua kubwa kimaendeleo ambapo kwenye sekta ya Afya pekee kata ya Mrijo imenufaika na kituo cha Afya kilichogharimu zaidi ya Milioni 700 huku pia Wilaya ya Chemba ikipata Hospitali ya Wilaya zote hizo zikiwa ni ahadi za Magufuli za mwaka 2015.

" Ndugu zangu wa Mrijo tunamuombea kura Dk Magufuli kwa sababu ametekeleza yale yote aliyoahidi kuyafanya mwaka 2015, aliahidi ataboresha sekta ya Afya leo wote ni mashahidi kwa jinsi ambavyo tumepiga hatua, katika vituo vya afya 484 vilivyojengwa nchini sisi kata ya Mrijo pia tumepata kituo cha afya cha kisasa kabisa, hii ni kuonesha jinsi gani Magufuli ni mtendaji na anaishi ahadi zake.

Dk Magufuli ametuletea Milioni 500 za ujenzi wa kituo cha Afya na Milioni 250 zikaletwa kwa ajili ya vifaa tiba na kituo kimekamilika. Lakini pia ngazi ya Wilaya alisema atatuletea Hospitali ndio maana katika Hospitali 77 za Wilaya zilizojengwa Wilaya yetu ya Chemba imepata Hospitali ya kisasa kabisa na huduma zinatolewa." Amesema Ditopile.

Amewaomba wananchi hao kumchagua tena Dk Magufuli ili azidi kuwatumikia watanzania ikiwemo wao wananchi wa Mrijo na Chemba ambapo katika ilani ya uchaguzi ya mwaka huu wamepanga kuhakikisha Halmashauri 98 ambazo zimebaki zote zinapata Hospitali lakini pia kuboresha bima ya Afya ili kila mnyonge aweze kupata matibabu kwa urahisi.

" Tusiwasikilize wapinzani kazi yao ni kuwahadaa tu, fikirieni Dk Magufuli alivyowabana wazungu kwenye sekta ya makinikia leo wapinzani kwenye ilani yao wanasema wakishinda wataweka rasilimali zetu hizo rehani, jamani kweli tuwape Nchi watu wa namna hii?.

Mgombea Ubunge wa Chadema hapa Chemba namfahamu, tumekua nae bungeni ni mbabaishaji tu hana upendo wowote kwenu zaidi ya kueneza ubaguzi wa kikabila, kwa miaka mitano hii aliyokua mbunge wa viti Maalum amefanya jambo gani hapa Chemba? Hata kusomesha mtoto mmoja tu ameshindwa, hajatoa fursa zozote za kimaendeleo kwenu zaidi amewekeza mjini, angekua na uchungu na nyinyi si angewekeza hapa wote mnufaike? Achaneni nao waongo na wababaishaji tu hao," Amesema Ditopile.

Amewaomba wananchi wa Mrijo waichague CCM kuanzia Diwani, Mbunge na Rais ili waweze kushirikiana kuendelea kutatua changamoto chache zilizobaki katika kata hiyo na Jimbo hilo. 

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni za Udiwani kata ya Mrijo, Chemba CCM, Mariam Ditopile (kushoto) akimnadi na kumkabidhi Ilani ya CCM mgombea Udiwani wa kata hiyo, Abdallah Suti.
Wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za Udiwani kata ya Mrijo wilayani Chemba, Dodoma kupitia Chama cha Mapinduzi wakifuatilia mkutano huo uliozinduliwa na Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile na kumnadi mgombea Udiwani, Abdallah Suti.
Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile akizungumza katika mkutano wa kampeni za Udiwani kata ya Mrijo wilayani Chemba, Dodoma.Wanachama na wafuasi wa CCM waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za Udiwani kata ya Mrijo wilayani Chemba, Dodoma.
Akina Mama ambao waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za Udiwani kata ya Mrijo wilayani Chemba  wakimsikiliza mgeni rasmi ambaye ni Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile.
Wananchi wa Kata ya Mrijo wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Udiwani kata hiyo ambapo zimezinduliwa na mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad