HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 10, 2020

WANAFUNZI MILIONI 20 TANZANIA KUVALISHWA VIATU KUTOKA KILIMANJARO

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ,Abdalah Ulega akizungumza jambo alipotembelea kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro .
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvivi ,Abdalah Ulega akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bidhaa za ngozi ya Kilimanjaro Mhandisi Masud Omari  wakat wa ziara yake ya siku moja kiwandani hapo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ,Abdalah Ulega akitembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho.
Moja ya majengo ya kiwanda hicho yaliyojengwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo .
Sehemu ya mashine zilizofika kwa ajili ya kusimikwa katika kiwanda hicho.
Awamu ya pili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakta ngozi ukiendelea katika eneo lililopo jirani na Gereza la Karanga mjini Moshi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ,Abdalah Ulega akitizama mashine za kuchakata ngozi alipotembelea kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro .
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bidhaa za Ngozi ya Kilimanjaro Mhandisi Masud Omari akiumuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi moja ya mashine zitakazotumika katika kuchakata ngozi katika kiwanda hicho .
Mashine kwa ajili ya kuchakata Ngozi ambazo zinatarajiwa kufungwa katika kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro .


Na Dixon Busagaga ,Kilimanjaro 

SERIKALI imesema ipo kwenye mchakato wa kutengeneza sera itayowezesha wanafunzi Mil 10 hadi Mil  20 wa shule za msingi na Sekondari wanaoanza masomo yao kutumia viatu vitakavyozalishwa na Kampuni ya bidhaa za Ngozi ya Kilimanjaro iliyopo mjini Moshi .

Hayo yameelezwa na naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalah Ulega wakati ya ziara ya siku moja  mkoani Kilimanjaro  ambapo ametembelea  mradi wa ujenzi wa viwanda vya kuchakata bidhaa za ngozi vilivyopo chini ya kampuni ya Kilimanjaro Leather Industries Co Ltd.

Akizungumza mara baada ya kujionea hatua za ujenzi zilipofikia Naibu Waziri Ulega alisema katika kuunga Mkono Jitihada za Rais Wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk John Joseph Pombe Magufuli za kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa viwanda, Mfuko Wa PSSSF umewekeza katika Mradi wa ujenzi wa Kiwanda kipya cha Bidhaa za Ngozi Mkoani Kilimanjaro .

“Wito wangu tu ni kwamba taasisi za serikali ,ni muhimu sana zikanunua bidhaa zetu sisi wenyewe tunazozalisha hapa sisi wenyewe hapa nyumbani ,kwa mfano watu wengi hawajaamini kama vitu vinavyotengenezwa na wajasiliamali wadogo wadogo na viwanda vyetu kama kweli ni ngozi .álisema Ulega.

“Tunalo tatizo la bidhaa hizi za plastiki yaliyokarabatiwa karabatiwa ,yameingia kwa wingi sana ,yamefanya hata wajasilia mali wetu hapa zile bidhaa wanazotengeneza sio ngozi ,lakini zile ni ngozi na watanzania tuamini kwamba zile ni ngozi.”aliongeza Ulega .

Alisema serikali inakusudia kuanza na watoto  katika mashule ya msingi na Sekondari baada ya kukubaliana na watungaji sera na viongozi katika wizara mbalimbali ambapo watoto kati ya Mil 10 na 20 watapata viatu .

Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hiki Mhandisi Masud Omar amesema Kampuni hiyo  pamoja na kampuni za Italia ,TMC na ITALPROGETTI wapo kwenye taratibu za mwisho za kuanza kazi ya kusimika mitambo na kwamba  janga la virusi vya Corona vimechangia kuchelewa kwa kazi hiyo.

“Ili kutekeleza agizo la Serikali, Kampuni ijulikanayo kwa jina la “Karanga Leather Industries Co Ltd” (KLICL) ilianzishwa mnamo tarehe 30 Mei, 2017 kwa lengo la kuanzisha mradi wa viwanda vya bidhaa za ngozi katika eneo la Gereza la Karanga, Moshi, Kilimanjaro kwa lengo la kuboresha kiwanda cha ngozi kilichopo na baadae kujenga kiwanda kipya cha kisasa cha utengeneaji wa ngozi na bidhaa zake. “alisema Mhandisi Omari .

Mhandisi Omari alisema kampuni hiyo ilianzishwa kwa ubia kati ya uliokuwa Mfuko wa Pensheni wa PPF, ambao kwa sasa majukumu yake yamechukuliwa na PSSSF pamoja na Jeshi la Magereza kupitia kampuni yake ya Prisons Corporation Sole.

“Hatua ya kwanza (LOT 1) ya utekelezaji wa mradi inayohusisha ujenzi wa kiwanda cha viatu yaani ujenzi wa jengo ya Ukataji na ushonaji, umaliziaji, ghala na nyumba ya umeme yamekamilika na mmiliki ameanza kuyatumia kwa matumizi ya kiofisi.

Alisema ujenzi huu umeenda sambamba na uwasilishwaji wa mitambo ambapo mitambo yote kwaajili ya kiwanda hivi vilivyokamilika vishawasili katika eneo la kiwanda huku zikisubiria wataalamu kutoka Italia kuja kuzifunga.

Kiwanda kipya kimejengwa katika eneo  la hekari 25  lililotengwa katika Gereza la Karanga Manispaa ya Moshi Mjini huku uzalishaji wa kiwanda hiki ukitazamiwa kuzalisha jozi 4,000 za viatu kwa siku sawa na jozi 1,200,000 kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad