HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 6, 2020

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imewaasa mawakili kutoishambulia mahakama

Na Karama Kenyunko Michuzi TV 
OFISI ya Wakili Mkuu wa Serikali imewaasa mawakili kutoishambulia mahakama kwenye mitandao ya kijamii na kukumbuka wajibu wao bila kujiingiza katika mivutano na mihimili ya dola na ikiwa hawajaridhishwa na maamuzi yotote wakate rufaa ili kupata nafuu nyingine.

Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata ameyasema hayo leo Agosti 6, 2020 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hukumu ya Mahakama ya Rufaa, iliyotolewa jana, na kuongeza kuwa baada ya hukumu hiyo, baadhi ya mawakili walipinga maamuzi ya mahakama kwamba imeshindwa kusimamia katiba.

Amesema mawakili wanalo jukumu la kusimamia na kuhakikisha sheria zinasimamiwa huku jamii ikiwa na jukumu la kuzingatia wajibu na haki zao zinasimamiwa.

Amesema, kufuatia uamuzi wa mahakama ya Rufaa, watu wameanza kuikejeli mahakama kwa maneno kama mahakama imeshindwa kusimamia haki za Kikatiba.

"Ninawaomba mawakili, sisi kama mawakili tuna miiko yetu, hupaswi kuanza kuishambulia mahakama kwenye Media, kama hujaridhika na maamuzi ya mahakama unatakiwa kutafuta nafuu nyingine ya ama kukata rufaa au kutafuta nafuu nyingine yoyote ili kuhakikisha shauri lako linasikilizwa tena kwa mara nyingine kama unaona unanafasi hiyo." Amesema Malata.

"Ofisi ya wakili Mkuu wa serikali haitasita kupeleka rufaa katika mahakama za juu kwa ajili ya kupata nafuu nyingine pindi waonapoona sheria zinakiukwa.

Ameongeza kuwa kama jamii inadai sababu za kupelekwa kwa maombi hayo ni ubambikiziwaji wa kesi, lazima uwepo ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo na kwamba katika kesi hiyo hoja hiyo haijazungumzwa.

"Mahakama kwa kauli moja ilikubaliana na hoja za serikali kwamba kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai sura ya 20 ya Sheria za Tanzania hakikinzani na Katiba ya nchi," alisema Malata.

Alisema jopo la majaji watano waliotoa uamuzi katika kesi hiyo, Jaji Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika, Jacobs Mwambegele, Mwanaisha Kwariko na Ignas Kitusi, lilibainisha kuwa masharti ya kifungu hicho hayakiuki matakwa ya Ibara ya 13 (3) na 15(1) (2) ya katiba.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo,  maamuzi ya Mahakama Kuu hayakuwa sahihi kwa sababu katiba ndio inayoruhusu baadhi ya makosa kutokuwa na dhamana.

Akitolea mfano makosa ya mauaji Wakili Malata amesema, kama ingekuwa watu wanaofanya matendo ya mauaji wanaachwa kwenye jamii kwa dhamana wale ndugu wa waliouawa wangefurahi? 

Na ndio maana Bunge liliamua kuweka sheria hii ili makosa makubwa kama haya ya mauaji na mengine ya uhujumu uchumi, biashara haramu za binadamu, dawa za kulevya na uhaini kutokuwa na dhamana," alisema Malata na kuongeza;

"Unapoua usitarajie mahakama itakupa dhamana kwani ingeruhusiwa kufanya hivyo, kungekuwa na athari kubwa kwenye jamii ikiwemo usalama wa mtenda kosa anaweza kuuawa, kupoteza mashahidi na pia  itaruhusu kuendelea kwa vitendo vya mauaji katika jamii."amesema.

Amefafanua kuwa, kifungu hicho kililenga katika kutekeleza vifungu vya 13(3) kuhusu wajibu wa mamlaka nyingine za nchi zinazowajibika kulinda usalama wa raia na mali zao.

Aidha, amesema katiba kama sheria mama inapaswa kutafsiriwa kwa mapana yake kwa kuzingatia malengo, maudhui yake katika kulinda haki ya kila mtu na jamii kwa ujumla na kwamba ikitafsiriwa bila kuhusisha sheria nyingine ni rahisi kuleta sintofahamu katika jamii.

Amesisitiza kuwa utaratibu wa kuzuia dhamana ni wa kikatiba kwani wakati ibara ya 15(1) ya katiba inampa mtu haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru, ibara ya 15 (2) inaruhusu haki na uhuru wa mtu kuingiliwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria lengo ni kulinda haki na usalama wa jamii.

Mei 18, mwaka huu mahakama Kuu ilitoa uamuzi dhidi ya Maombi hayo na kusema kwamba Kifungu cha 148 (5)  cha sheria ya makosa ya jinai kinakiuka Katiba.

 AG na DPP walikata rufaa hiyo namba 175/2020 wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri namba 29/2019 lililofunguliwa na Dickson Sanga akitaka makosa hayo yawe na dhamana kwa sababu kifungu kilichokuwa kinazuia dhamana, kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 Wakili Mkuu wa serikali, Gabrieli Malata  akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam leo, juu ya uamuzi wa rufaa iliyokatwa na serikali kupinga hukumu ya mahakama Kuu ya kuruhusu makosa makubwa kupewa dhamana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad