Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
MKUU wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, amewajia juu maafisa
tarafa, watendaji wa vijiji na kata, wilayani Bagamoyo kuhakikisha
wanatimiza wajibu wao wa kazi na kutatua kero za wananchi ikiwemo
migogoro ya ardhi, ndani ya mwezi mmoja kabla hajachukua maamuzi mazito
dhidi yao.
Aidha ameeleza ,wilaya hiyo imehemewa na migogoro ya ardhi hali
inayosababisha baadhi ya wananchi badala ya kukimbizana na maendeleo
wanakimbizana na mashauri ya migogoro hiyo katika mabaraza ya ardhi na
mahakamani.
Akizungumza katika ziara yake aliyoianza mkoani Pwani, kusikiliza
kero za wananchi, akianzia Bagamoyo, Ndikilo ameshtushwa kupokea
malalamiko 88 ambayo mengi yapo ndani ya uwezo wa kutatuliwa ngazi ya
chini.
Ndikilo alielezea, mabaraza ya ardhi kata pia hayafanyi kazi
kiufanisi na ni chanzo cha migogoro hali inayosababisha baraza la ardhi
Kibaha kuhemewa na mashauri.
"Hii inaashiria watendaji wa chini hawawajibiki, naweza kuandika
mapendekezo muondoke wote na nawapa salamu msipokaa sawa mtaondoka."
Hata hivyo Ndikilo alibainisha, idara ya ardhi ofisi ya mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo wasichelewe kufanya maamuzi ya
mashauri ya wananchi kwani inasababisha kero.
"Mchukue hatua haraka kulingana na mashauri yao, malizeni kwa muda
mfupi." Wananchi wanataka haki zao, teteeni wanyonge kama hana haki
ijulikane kuliko kuzungushwa." Alisisitiza Ndikilo.
Pamoja na hilo ,mkuu huyo wa mkoa alivitaka vyombo vya dola
kushughulikia vikundi vya kiuhalifu vinavyolalamikiwa na wauzaji ardhi
wanaotumia mabavu ili kulinda raia na mali zao .
Nae mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ,Zainab Kawawa alieleza kero
zinazohusu kushughulikiwa na ofisi ya mkuu wa wilaya atazifanyia kazi na
zipo ambazo kishaanza kuzishughulikia .
Kwa upande wa wananchi akiwemo Swaiba, mzee Hussein Mfaume, Asha
Mwambala na Amina Ramadhani wanakabiliwa na migogoro ya ardhi miaka
mingi na tatizo lipo katika kuchelewesha mashauri wanayoyapeleka.
No comments:
Post a Comment