HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 5, 2020

WAZIRI LUKUVI ATAKA WAMILIKI WA ARDHI WENYE HATI ZA MIAKA 33 KUZIHUISHA OFISI ZA ARDHI ZA MIKOA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizundua ofisi ya ardhi mkoa wa Mara jana. Kushoto kwa Waziri Lukuvi ni Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima na kushoto ni Bi Sophia Lugera mmoja wa wananchi wa kwanza kupatiwa hati kwenye ofisi hiyo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza katika Masijala ya ardhi ya ofisi ya Ardhi Mkoa wa Mara wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo jana. Wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza huku akiwa amezungukwa na wananchi wa mkoa wa Mara walimfuata kutaka kutatuliwa kero zao za ardhi wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Mara jana.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiangalia maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara sehemu ya jengo la Huduma ya Mama na Mtoto alipokwenda kufuatilia maendeleo ya ujenzi huo jana wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Mara.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimpa mkono wa shukurani Padri Cleophas Sabure wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma kufuatia kutoa msaada ya Printer kwa ajili ya urahisishahi utendaji kazi wa ofisi mpya ya ardhi mkoa wa Mara jana. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wamiliki wa ardhi ambao hati zao za ardhi zinaishia miaka 33 kwenda ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni kuzihuisha ili kupatiwa za miaka 99.

Lukuvi ametoa kauli hiyo jana mkoani Mara wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Mara ambayo ni ofisi ya kumi na mbili kuzinduliwa ikiwa ni mfululizo wa kuzindua ofisi za ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Alisema, kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi kwenye mikoa mbalimbali ambao viwanja vyao vimepimwa na michoro kuidhinishwa lakini hati zao ni za miaka 33 na wamiliki hao watakapoenda kuzichukua wanatakiwa kuziangalia ili zibadilishwe na kupatiwa hati za miaka 99.

‘’ Hati nyingi za wale wamiliki ambao hawajazichukua zimekwisha muda wake, muende kwenye ofisi za ardhi za mikoa, huko mtaelekezwa na Wasajili Wasaidzi wa ardhi katika ofisi hizo namna ya kuzibadilisha ili mpatiwe za miaka 99’’ alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, zaidi ya wamiliki wa ardhi 50,000 kwenye mkoa Mara hawajachukua hati za ardhi wengi muda wa hati zao unaishia miaka 33 na kutaka kufika ofisi za ardhi mkoa wa Mara kurekebishiwa na kupatiwa za miaka 99 ili iwe rahisi kupata mikopo mikubwa .

Akizungumzia uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Mara, Lukuvi alisema mkoa huo umekuwa na migogoro mingi ya ardhi na kubainisha kuwa uzinduzi wa ofisi hiyo utawawezesha wananchi wa Mara kumaliza migogoro kupitia ofisi hiyo badala ya kuipeleka migogoro kwake.

Waziri Lukuvi aliongeza kuwa, pamoja na Wizara yake hapo awali kushughulikia kero na migogoro ya ardhi lakini tatizo la kimfumo lilikuwa kubwa na kuweka wazi kuwa uzinduzi wa ofisi za mikoa unakomesha kero ambapo sasa hakutakiwa na gharama yoyote kwa mmiliki wa ardhi zaidi ya ile atakayolipia wakati wa kuomba hati.

‘’Mgogoro wa kimfumo ulikuwa mkubwa zaidi na leo hii tumekomesha kero na hakuna gharama yoyote mmiliki wa ardhi ataingia kufuatilia hati zaidi ya ile aliyolipa wakati wa kuomba hati, serikali ya awamu ya tano imeondoa kero zote kwa wananchi kwenye utawala wa ardhi’’ alisema Lukuvi.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima alisema, ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko na kero nyingi na kati ya malalamiko kumi na mbili anayopokea kwa siku sita yanahusiana na ardhi na kusisitiza kuwa, mingi ya migogoro ya wananchi lazima nguvu hutumika jambo alilolieleza kuwa linaongeza gharama za kiafya katika masuala ya matibabu na kubainisha kuwa uwepo ofisi ya ardhi katika mkoa huo utarahisisha huduma katika sekta ya ardhi..

‘’ Kila malalamiko kumi na mbili ninayopata ofisini kwangu sita ni ya ardhi na mengi yana sura ya kijamii na hapa kuna neno la msamiati ukisikia vyesi ujue ni kesi’’ alisema Malima.

Mmoja wa wakazi wa Musoma aliyepatiwa hati katika uzinduzi ofisi ya ardhi Bi. Mara Sophia Lugera alifurahishwa na usogezwaji huduma za ardhi mkoani Mara na kubainisha kuwa aliifuatilia kwa muda mrefu hati yake iliyokuwa ofisi ya Kanda Mwanza na kusema, baada ya kuipata hati ataitumia kuchukulia mkopo benki ili aendeleze biashara yake ya ujasiriamali.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alitembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara inayojulikana kama Mawalimu Nyerere Memorial Hospital iliyopo eneo la Kwangwa Musoma mkoa wa Mara.

Akiwa katika mradi huo, Lukuvi aliagiza kukamilika kwa jengo ya Huduma ya Mama na Mtoto kufikia mwisho wa mwezi huu ili lianze kutumika kwa wananchi wa mkoa huo na Mikoa jirani.

Alisema, ujenzi wa jengo hilo umechukua muda mrefu na anataka kuona sehemu ya jengo hilo inakamilika kufikia julai 31 mwaka huu na Agosti mosi 2020 atamuagiza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwenda kuona kama agizo lake limetekelezwa kama alivyoahidiwa.

Mhandisi na Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Hosiptarli ya Rufaa mkoa wa Mara Renald Kazyoba alisema, kimsingi sehemu ya ujenzi wa mradi huo sehemu ya Huduma ya Mama na Mtoto (Wing C) itakamilika kama alivyoagizwa kwa kuwa kazi kubwa imefanyika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad