HALMASHAURI YA CHALINZE YATAKIWA KUSIMAMIA MAPATO YA NDANI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 13, 2020

HALMASHAURI YA CHALINZE YATAKIWA KUSIMAMIA MAPATO YA NDANINa Mwamvua Mwinyi, Chalinze

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Zainab Kawawa, ameitaka halmashauri ya Chalinze kusimamia mapato ya ndani na kuwaasa kutowafumbia macho watumishi ambao wanasababisha kushuka kwa mapato.

Aidha amesisitiza kuweka watumishi wanaosimamia ushuru kukaa kwenye maeneo ya uchimbaji kokoto, hatua inayolenga kuwadhibiti wafanyabiashara wanaojihusisha na ukwepaji wa ushuru.

Zainab alieleza hayo ,katika kikao cha kupitia taarifa ya mkaguzi wa Serikali (CAG), kilichofanyika shule ya sekondari ya Lugoba, ambapo Halmashauri hiyo imepata hati safi kwa miaka minne mfululizo.

"Lakini nashangaa kwa nini hivi sasa mnashuka , endeleeni na kusimamia ili muendelee kukaa katika hati safi,mpeni ushirikiano mkaguzi wa ndani na kumsikiliza ushauri akitoa ili kuinua mapato zaidi ,na yeyote atayezembea katika kitengo hicho aondoke mwenyewe," alibainisha Zainab.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya halmashauri kwa miaka minne mfululizo, mwenyekiti Said Zikatimu alisema,wamejenga shule mpya nne za sekondari, zahanati 39, wamegawa pikipiki kwa maofisa wa kilimo, mifugo pamoja na watendaji wa kata, kwa lengo la kuboresha majukumu yao.

Shule za sekondari zilizojengwa ni Pera, Lupungwi, Chahua na Chamakweza ambapo fedha zimepelekwa kwa ajili ya kumalizia ujenzi na fedha nyingine za kujenga majosho ya kuogeshea mifugo katika kila kata.

Nae Ofisa Mkaguzi wa ndani Consolata Kiria, alielezea utekelezaji wa mapendekezo ya hoja yaliyotolewa kwa mwaka 2018/ Juni 2019 yalikuwa 44, yaliyotekelezwa na hoja kufungwa 18 sawa na asilimia 41, yanayoendelea kufanyiwa kazi kulingana na maoni ya mkaguzi yapo 26 sawa na asilimia 59.

"Mheshimiwa Mwenyekiti Halmashauri yetu kulingana na taarifa ya Mkaguzi wa Serikali, tumeendelea kupata hati safi kwa mwaka wa nne mfululizo, hii inatokana na kuendelea vizuri kwa utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo kwenye Halmashauri ,"

Awali akimkaribisha mkuu wa Wilaya, Kaimu Mkurugenzi Zaynab Makwinya alifafanua kikao hicho kinalenga kupitia utekelezaji wa kazi ndani ya halmashauri hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad