HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 4, 2020

MASANJA ARIPOTI OFISINI KWA DC KATAMBI, AOMBA RADHI NA KUSAMEHEWA

 Mchekeshaji Emmanuel Mgaya 'Masanja' (kulia) akizungumza na wandishi wa habari baada ya kumaliza kuhojiwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi (kushoto) mchana wa leo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi akizungumza na wandishi wa habari baada ya kumaliza kumhoji Masanja baada ya jana kuagiza kuripoti ofisini kwake.
Charles James, Michuzi TV
YAMEISHA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi kumsamehe mchekeshaji Emmanuel Mgaya 'Masanja' baada ya kuitikia wito wake alioutoa jana.
DC Katambi alimpa Masanja siku tatu kuripoti ofisini kwake ili kuhojiwa na kueleza sababu ya yeye kurikodi kipindi chake akiwahoji wananchi wa Dodoma maana ya Covid19 jambo ambalo kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya lililenga kupotosha kwamba wananchi wake hawana uelewa na ugonjwa huo.
Kufuatia wito huo jana hiyo hiyo Masanha aliripoti ofisi ya DC na kuelekezwa kuja leo ambapo ameripoti na kuhojiwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo aliomba msamaha na kuahidi kutumia nafasi yake kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa Corona.
Akizungumza na wandishi wa habari baada ya kumaliza mahojiano, Masanja amempongeza DC Katambi kwa kuwa mwepesi wa kugundua kuwa kulikua na shida kwenye kipindi chake alichorusha jambo linaonesha kweli yeye ni kijana na anaenda na spidi ya Rais Magufuli katika kuwatumikia watanzania.
" Niombe radhi kwa kueleweka vibaya lengo la kipindi chetu lilikua kuelimisha na siyo kuleta mzaha, namshukuru Mkuu kwa wito wake huu ambao umenisaidia pia kwa namna moja ama nyingine kujua wapi nilipoteleza.
Kama Taifa tunapita kwenye kipindi kigumu kutokana na maambukizi ya ugonjwa huu hivyo tuendelee kuchukua tahadhari zote kama tunavyoelekezwa na wataalamu wetu ili tuzidi kuwa salama," Amesema Masanja.
Mchekeshaji huyo ambaye pia ni Mchungaji amemuahidi DC Katambi kuwa atatumia kipawa chake cha kuhubiri pia kuhamasisha watanzania kutumia vitakasa mikono na kufuata masharti yote ambayo yanatolewa na viongozi.
Nae DC Katambi amesema hana tatizo binafsi na Masanja wala kituo cha DW ambacho muigizaji huyo anafanyia kazi bali walimuita kwa ajili ya kuwekana sawa.
" Sisi hatuna tatizo binafsi, ukiangalia kipindi kile maudhui yake ni kama kuonesha kwamba watanzania wote na hasa wanadodoma hatuna uelewa na virusi hivi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona.
Kitendo cha kuweka watu wote waliokosea kujua maana ya covid19 ni kuuaminisha umma kwamba Tanzania siyo mahali sahihi kwa kwa kipindi hiki maana wananchi wake hawajui hata maana ya ugonjwa huu, kumbe ni njia zilizotumika ndizo hazikua sawa, hivyo tumemhoji Masanja na baada ya kuelewa na kuomba radhi tumemsamehe," Amesema Katambi.
Amesema serikali imeendelea kuchukua hatua zote za kuhakikisha zinakabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo na kuwataka watanzania kuendelea kuchukua tahadhari na kumuomba Mungu kama ambavyo Rais Magufuli alielekeza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad