HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 27, 2019

Watumishi wa TAA wasisitizwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania  Mhandisi Julius Ndyamukama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano wa 24 wa Baraza Kuu la Wafanya kazi akifafanua jambo wakati wa Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha , kulia kwake ni Katibu wa Baraza hilo Bi, Naomi Semadio.
Wajumbe Wengine  wa Mkutano wa 24  wa Baraza Kuu  la Wafanyakazi wakifuatilia kwa makini taarifa mbalimbali wakati wa Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha.
Wajumbe wa Mkutano wa 24  wa Baraza Kuu  la Wafanyakazi wakifuatilia kwa makini taarifa mbalimbali wakati wa Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha hapo .
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania  Mhandisi Julius Ndyamukama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano wa 24 wa Baraza Kuu la Wafanya kazi alipokuwa akimkaribisha  mgeni rasmi wakati wa Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha.
Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi) Bw, Grayson Mwaigombe akifunga Mkutano wa 24 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Arusha aliyenyoosha mkono Mhandisi Elipid Tesha akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Mkutano wa 24 wa Baraza kuu la Wafanyakazi walipotembelea miradi inayoendelea katika Kiwanja hicho..

Watumishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania wamesisitizwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa umma mahala pa kazi kwa kufuata taratibu na kanuni za uendeshaji wa kazi za Serikali katika maeneo yao ya kazi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya uchukuzi) Bw, Grayson Mwaigombe  kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leornard Chamuriho alipokuwa akifunga Mkutano wa 24 wa Baraza kuu la Wafanyakazi Jijini Arusha.
“Umetolewa mfano  na Mwenyekiti wa Baraza  eneo la uendeshaji katika Kiwanja cha Ndege cha  kimataifa cha Julius Nyerere kwa mujibu wa sheria za maadili na sheria za fedha za Umma kama Watumishi tunaohudumia Mamlaka hatupaswi kujiingiza katika shuguli za kibiashara za Mamlaka husika kwani sheria za maadili ya umma zinatoa muongozo wa katazo wa kushiriki shuguli za biashara za Taasisi yako” alisema.
Aidha Mwaigombe aliendelea kusema tathmini mbalimbali kutoka kwa Idara na Vitengo mbalimbali na yale yote yaliyotolewa kama mchango na taarifa, Menejimenti ya Mamlaka iangalie namna ya kuyafanyia kazi na kuboresha ili kufikia kikao kingine kuwe na taarifa zinazoridhisha kutokana na yale yaliojadiliwa.
Akizungumzia kuhusu afya Bwana Mwaigombe alisema elimu iliyotolewa ya ugonjwa wa Homa ya ini ikalete chachu kwa wajumbe wa Baraza hilo ili kuweza kupima  afya zao  huku menejimenti ikiangalia namna ya kulifanyia kazi kwa kuweza kuwasaidia Watumishi wote kuweza kupima na kupata chanjo kwani limekuwa ni gonjwa linalopoteza nguvu kazi katika kulijenga Taifa kwa ujumla.
Awali akizungumzia kuhusu uadilifu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo  Mhandisi  Julius ndyamukama alisema ni lazima Watumishi wote wajitathmini haswa katika eneo la kuwa miongoni mwa watu wenye mikataba ya biashara ndani ya Taasisi kwani ni kinyume na taratibu za maadili ya utumishi wa umma huku akiwashauri wanaofanya hivyo kujitathmini.
Pia Mhandisi Ndyamukama alisisitiza kuwa ni  kosa kutuma taarifa za Taasisi  kiholela  na  zisizo rasmi kwenye makundi sogozi (Social Media)  na vyombo vya habari ikiwa sio msemaji wa Taasisi  hivyo Watumishi wanapaswa kuliangalia hilo kwa umakini kwani hata sheria ya mwaka 2015  ya makosa ya mtandao hairuhusu kufanya hivyo.
Wajumbe wa Mkutano wa 24 wa  Baraza pia wameweza kutembelea Kiwanja cha ndege cha Arusha kujionea miradi mitatu ambayo inafanywa na kiwanja hicho ikiwemo la utengenezaji wa eneo jipya la maegesho ya magari  lenye ukubwa wa mita za mraba 13,296  kwa kiwango cha lami ambalo litakuwa na uwezo wa  kupaki magari 250 , eneo la “parallel tax way” lenye urefu wa  mita 500  ambalo litasaidia ndege kuelekea  katika eneo la maegesho ya ndege  na barabara mbadala ya njia ya magari.
 Akizungumza Meneja wa Kiwanja hicho cha Ndege Mhandisi Elipid Tesha  alisema  baada mara baada ya kukamilika kwa miradi hiyo mradi utakaofuata baada ya taratibu za zabuni kukamilika ni  kuongeza eneo  la mita 200 la  barabara ya kuruka na kutua ndege  ili kuwezesha ndege aina za Bombardier Dash 8 Q- 400 kuweza kutua katika Kiwanja hicho pamoja na eneo la kugeuzia ndege.
Mkutano huo wa 24 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi umefanyika kwa siku mbili  katika Ukumbi wa Mikutano wa AICC Jijini Arusha ukijumuisha Wajumbe Kutoka Kanda mbalimbali pamoja na menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na kufungwa rasmi katika siku ya jana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad