WANAFUNZI 237 WAPATA MAFUNZO YA BTEC KUTOKA MTANDAO WA KUSIMAMIA HAKI ZA MTOTO WA KIKE CAMA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 27 November 2019

WANAFUNZI 237 WAPATA MAFUNZO YA BTEC KUTOKA MTANDAO WA KUSIMAMIA HAKI ZA MTOTO WA KIKE CAMA

Na, Irene Mwidima, Globu ya Jamii
DSJ
MTANDAO wa Kupambana na Kusimamia  haki  za msingi za mtoto wa Kike CAMA AGM wamefanya mkutano Mkuu wa  kumi na tatu wa kufunga mwaka na Kukabidhi vyeti kwa wanafunzi  237 waliohitimu mafunzo ya  BTEC.

 Mkutano huo umefanyika leo Jijini  Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mgeni rasmi  Afisa Mwandamizi Wa Elimu ya Sayansi na Teknolojia Naomi Swai akimwakilisha Kamishna wa Elimu Dr Lyabwene Mutahaba,

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa CAMA Taifa Tanzania Mwanahamisi Boraafya amesema CAMA imeanzishwa mwaka 2006 ikiwa na matumaini ya kumsaidia binti au mtoto wa kike na kusimamia haki zao za msingi na  Ikiwa imeanzishwa ndani ya mkoa mmoja ambao ni Iringa.

Amesema, baadae walizidi kutanua wigo na  kwenda mikoa mingine mpaka kufika mikoa tisa ambayo ni Iringa, Dar-es-salaam, Tanga, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Pwani na Singida.

"Wakati tunaanzisha mtandao huu ulilenga zaidi katika kumsaidia binti au mtoto wa kike ikiwemo ma  kumsimamia haki zake za msingi na kuepukana na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia, pia kuwapa mafunzo mbalimbali yatakayowainua kiuchumi," amesema Mwanahamisi.

Afisa Mwandamizi Naomi amesema  serikali ya awamu ya tano  inalenga kujenga uchumi wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na Ili kutimiza malengo hayo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo yenye dhamana ya kusimamia utoaji elimu, ujuzi, maarifa na stadi zitakazowawezesha vijana wetu kutoa mchango unaotakiwa katika ujenzi wa uchumi wetu.

Naomi amesema, wamejipanga kusimamia vyema elimu na mafunzo yanayotolewa ili kuhakikisha yanakuwa bora na yanatoa mchango wenye tija katika ujenzi wa uchumi wa nchi.

"Napenda kuupongeza mtandao wa CAMA kwa kuhamasishwa ushiriki wa jamii katika kuboresha miundombinu ya kufundisha na kujifunza shuleni ikiwemo utoaji wa chakula, vifaa vya shule kwa wanafunzi, kuboresha miundombinu kama madawati, vitanda, ukarabati wa mabweni ya wasichana na nyumba za walimu, hii imechangia kuongeza uelewa kwa jamii katika utekelezaji wa waraka wa elimu bila malipo",amesema Naomi

Pia ameongeza, "Niwapongeze pia kwa kuanzisha elimu ya stadi za maisha katika shule za sekondari. Elimu hii imewezesha wanafunzi kujitambua, kuboresha ustawi wao na kufahamu vipawa vya ndani walivyonavyo, kuboresha mahudhurio na kupunguza utoro mashuleni"

"Napenda kuwapongeza wahitimu 237 wa BTEC nitakaowapatia vyeti vyao siku ya leo. Kwa kweli nimefurahi kuona vijana wana ari ya kujiendeleza ili kujiongezea ujuzi na maarifa na baada ya kuwagawia vyeti mkutano huu utakuwa umefungwa rasmi", amesema Naomi 

Mtandao wa CAMA umekuwa na utaratibu wa kutoa elimu na mafunzo mbalimbali kwa vijana na hususani wakiwalenga watoto wa kike ili waweze kujikimu kimaisha na kuachana na masuala ua unyanyasaji wa kijinsia.
 Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Naomi Swai akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mkutano mkuu wa mwaka wa kumi na tatu wa CAMA AGM uliofanyika katika ukumbi wa Msimbazi Centre Marantha.
 Upendo Essau kutoka Mwanza mfadhiliwa wa CAMFED akipokea cheti cha kutambua uwezo wake katika fani mbalimbali kutoka kwa Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Naomi Swai leo katika ukumbi wa Msimbazi Centre Marantha jijini Dar es Salaam.
 Wahitimu 237 wa BTEC wakimsiliza kwa makini Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Naomi Swai.
 Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Naomi Swai (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa BTEC leo jijini Dar es Salaam.

(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad