HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 1, 2019

WAZIRI MKUU ASHUHUDIA USAFIRISHAJI WA KOROSHO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea bandari ya Mtwara na ameshuhudia shehena ya korosho ziliyonunuliwa na kampuni ya Tang Long zikipakiwa katika meli kubwa yenye jina la AS Christiana kwa ajili kusafirishwa kwenda nchini Vietnam.

“Ni faraja kuona mzigo wa korosho ukiondoka na kutoa nafasi ya kuingiza mzigo mwingine mpya wa korosho utakaopatikana baada ya kuanza msimu mpya mwezi huu. Na mnunuzi huyu ameahidi kununua tani 100,000 katika msimu wa mwaka huu.”

Waziri Mkuu ametembelea Bandari ya Mtwara leo (Jumanne, Oktoba 1, 2019) kwa ajili ya kujionea kazi ya usafirishaji wa korosho inavyofanyika na amesema kwamba ameridhishwa na kasi na utaratibu unaoendelea badarini hapo.

Amesema kampuni ya Tang Long ya nchini Vietnam licha ya kuahidi kununua korosho katika msimu wa mwaka huu, pia imeomba kupatiwa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho nchini na kwamba wapo tayari kuanza hata Desemba, 2019.

Waziri Mkuu amesema suala la ujenzi wa viwanda vya kubangulia korosho nchini litaongeza thamani na kuwezesha dunia nzima kutambua kuwa korosho hizo zimetoka Tanzania kwa sababu kwenye vifungashio watakuwa wameandika, hivyo kuongeza soko.

Akizungumzia kuhusu msimu wa uuzaji wa korosho wa mwaka huu, Waziri Mkuu amesema kipaumbele cha kwanza watapewa wenye viwanda vya ndani na kisha tani zinazobaki zitauzwa kwa wanunuzi kutoka nje.

“Wito wa Rais Dkt. John Magufuli wa ujenzi wa viwanda unalenga katika kuongeza ajira kwa wananchi kwa kuwa viwanda vinaajiri watu wengi wenye kada tofauti. Wakuu wa mikoa endeleeni kurahisisha mazingira ya uwekezaji.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Geoffrey Mwambe amesema licha ya kampuni ya Tang Long kununua korosho nchini pia imeomba ikodishwe kiwanda kimojawapo cha Serikali ili waweze kuanza ubanguaji wa korosho ikiwa ni mpango wa muda mfupi na katika mpango wao wa muda mrefu wameomba eneo kati ya mkoa wa Lindi au Mtwara ili wajenge kiwanda cha kubangua korosho. Taratibu zinaendelea.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Renatus Mkinga wakati alipotembelea bandari ya Mtwara kukagua kazi ya usafirishaji wa korosho, Oktoba 1, 2019.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa (kushoto) wakati alipokagua kazi ya kusafirisha korosho kwemye bandari ya Mtwara, Oktoba 1, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad