HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 23, 2019

UWT MAGHARIBI WAFANYA ZIARA DIMANI

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania(UWT) Mkoa wa Magharibi kichama Ndugu Zainabu Ali Maulidi, amewaagiza uongozi wa ngazi za matawi hadi wilaya mkoani humo kuandaa mipango mikakati ya kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa dola mwaka 2020.

Agizo hilo amelitoa katika ziara maalumu ya Kamati ya Utekelezaji ya UWT ya Mkoa huo ya kutembelea Majimbo 13 ya Umoja huo huko katika Jimbo la Dimani Unguja,amesema huu ni wakati wa kazi hivyo kila mwanachama anatakiwa kutumia kutumia uwezo na maarifa yake kuhakikisha Chama kinashinda.

ZainabU,alifafanua kuwa mipango mikakati hiyo baada ya kuandaliwa ni lazima itekelezwe kwa vitendo ili kuongeza tija katika mipango ya kujiimarisha kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Zainabu, alisema ziara hiyo itafanyika kwa majimbo yote ya Mkoa huo na kusikiliza changamoto na ushauri wa viongozi, Watendaji na wanachama wa ngazi mbali mbali kisha kutoa maelekezi yatakayosaidia Utatuzi wa changamoto hizo.

"Ziara hii ni ya kikazi zaidi kwani hakuna muda tena wa kusema tu bila kutenda ni lazima akina mama wenzangu tuwe mstari wa mbele kulinda heshima ya historia yetu ndani na nje ya CCM kwani sisi ni jeshi kubwa la kufanikisha ushindi wa Chama.", amesema Zainab.

Akitoa mada ya udhalilishaji Mjumbe wa Kamati tekelezaji ya Mkoa huo ndugu Asha Makungu Othman, alisema licha ya serikali kutunga sheria za kudhibiti uhalifu huo bado umeendelea kufanyika kwa kasi na kuwaathiri Watoto na Wanawake.

Alishauri jamii kufanya mikutano ya mara kwa mara ya zoni na shehia kuvitumia vikundi vya polisi jamii kuthibiti udhalilishaji huo kama walivyodhibiti vitendo vya uhalifu wa aina mbali mbali mitaani.

Alieleza kuwa tatizo linalochangia kuongezeka kwa udhalilishaji ni jamii kuacha malezi,utamaduni na desturi za zamani badala yake kufuata utamaduni wa kigeni unachongia kuporomoka kwa maadili.

kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Fatma Ali Ameir, akizungumza katika ziara hiyo aliwasihi akina mama hao kuepuka kufanya kampeni za kuwanadi watu wenye nia ya kugombea uongozi kabla ya wakati uliopangwa kisheria.

"Viongozi bado wapo madarakani alafu wanajitokeza wengine wanataka kuchukua nafasi zao, hiyo sio tabia nzuri kwani inaweza kuleta machafuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi.", amesema Fatma.

Alisema ni muhimu kila viongozi na wanachama ndani ya UWT wafuate miongozo,kanuni na maelekezo ya Katiba za Umoja huo na Chama cha Mapinduzi ili kujiepusha na migogoro.
 MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Magharibi Kichama Ndugu Zainab Ali Maulid, akizungumza na Wanawake wa Umoja huo katika Jimbo la Dimani huko Kombeni Unguja katika ziara ya Kamati ya utekelezaji ya Mkoa huo ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika Majimbo 13 ya Mkoa.
Akina Mama wa UWT jimbo la Dimani wakiwemo Wajasiriamali wa kutengeneza bidhaa mbali mbali wakisikiliza mada zinazotolewa na Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Mkoa wa Magharibi katika ziara hiyo maalumu ya kuimarisha uhai wa CCM.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad