HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 15, 2019

TANZANIA INATARAJIA KUPATA DOLA ZA MAREKANI MILIONI 500 KWA AJILI YA MRADI WA ELIMU

Na Eva Valerian na Ramadhani Kissimba, Washington Dc

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayewakilisha nchi za Afrika Bi. Anne Namara Kabagambe, Mjini Washington DC, Marekani.

Mazungumzo hayo yalilenga katika kubadilishana uzoefu juu ya utekelezaji wa Sera mbalimbali za fedha na namna uchumi wa Dunia unavyoendeshwa.

Katika mazungumzo hayo baadhi ya miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa(SGR), ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha umeme la mto Rufiji, mradi wa elimu,na miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ilijadiliwa. 

Dr. Mpango alieleza dhamira ya Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuinua kiwango cha elimu, kwa kutafuta fedha zaidi na mikopo ya masharti nafuu ambayo itaelekezwa kwenye elimu.

‘’Katika Mradi wa Elimu unaotarajiwa kuwasilishwa Benki ya Dunia mwezi Novemba, 2019, tunatarajia kupata dola za Marekani milioni 500, na nimemuomba Bi. Anne Namara Kabagambe azidi kusisitiza ili Taifa liweze kupatafedha hizi kwa wakati, na tunaamini kwamba fedha hizo zitaidhinishwa na Benki ya Dunia kama tunavyotarajia.”Alisisitiza Dkt Mpango.

Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango alisema pamoja na miradi ya Elimu, Sekta ya nishati ya umeme pia ni muhimu katika kuinua uchumi wa nchi kwa sababu ukipatikana umeme wa kutosha utasaidia kwa vitendo agenda ya uchumi wa viwanda kwa kuongeza thamani ya mazao na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii nchini.

Aliiomba Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa zisaidie kwenye miradi ya mikubwa inayotekelezwa na Serikali hasa katika sekta ya umeme na miundombinu.

Aidha Dkt. Mpango alieleza kuwa hivi karibunii Benki ya Dunia iliipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 450 kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF, awamu ya tatu.

“Hivyo kupitia miradi miwili ya Elimu na TASAF, Tanzania inatarajia kupata dola za Marekani milioni 950”. Aliongeza Dkt. Mpango

Kwa upande wa Benki ya Dunia Bi. Anne Namara Kabagambe alielezea kufurahishwa na utekelezaji wa miradi inayofanyika Tanzania kwani alipata fursa ya kuona miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na miradi inayotekelezwa na TASAF, na kuelezea kuwa ni miradi ya mfano na kwa nafasi yake ataendelea kuitangaza miradi hiyo ili Tanzania iweze kupata fedha zaidi ya kutekeleza miradi hiyo.

Dkt. Mpango anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Dunia IMF ambapo amesema mikutano hiyo ni muhimu kwa kuwa nchi itapata fursa ya kuweza kujadiliana na Taasisi hizi za IMF na WB kuhusu miradi wanayofadhili.

Aidha, kupitia mikutano hiyo vipaumbele vya nchi vitaelezwa na kupitia changamoto zilizopo kwa sasa, kutetea maslahi mapana ya Tanzania katika utekelezaji wa programu za maendeleo na mabadiliko ya kimfumo katika uendeshaji wa uchumi kutegemeana na mwenendo wa Dunia unavyokwenda,

Alisisitiza kuwa nchi inapata uzoefu wa nchi nyingine wanavyotekeleza na kusimamia program zao na wao pia kuweza kuzieleza nchi nyingine namna ambavyo Tanzania inatekeleza programu mbalimbali za kimaendeleo.
 Kutoka kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. (Mb)  Philip Isdor Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Mohamed R. Abdiwawa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Khamis M. Omary wakiwa kwenye mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia (hayupo pichani) kuhusu miradi ya maendeleo nchini Tanzania.
Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kundi la  Afrika Bi Anne Namara Kabagambe na Mshauri Mwandamizi kundi la Afrika Bw. Zarau Kibwe akielezea mafanikio aliyoyaona alipotembelea miradi ya Maendeleo Tanzania.  (Picha na Kitengo cha Mawasiliano SerikaliniWizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad