SERIKALI YAPONGEZA UWEZESHAJI WA BENKI YA MAENDELEO YA TIB KATIKA VIWANDA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 17 October 2019

SERIKALI YAPONGEZA UWEZESHAJI WA BENKI YA MAENDELEO YA TIB KATIKA VIWANDA

Na Mwandishi wetu, Kibaha
Serikali imepongeza uwekezaji unaofanywa na Benki ya Maendeleo ya TIB kwa kuwezesha uwekezaji kwa viwanda na makampuni ya wazawa hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Pongezi hizo zilitolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya wakati alipotembelea Banda la Benki ya Maendeleo TIB wakati wa Maonesho ya Wiki ya Viwanda ya Mkoa wa Pwani yanayoendelea mjini Kibaha.
Mhandisi Manyanya aliyekuwa akimwakilisha Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa maonesho hayo alisema kuwa uwekezaji unaofanywa na Benki ya Maendeleo TIB umechangia kwa kiasi kikubwa kuondoa utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kutoa ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wake Naibu wa Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wazalishaji wa nyaya na vifaa vya umeme kuwa waendelee kuzalisha vifaa bora, kwa kuwa soko la bidhaa hizo lipo hasa kwa kuzingatia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya nishati.
“Naomba niwahakikishie kuwa soko la bidhaa zenu lipo na kama mnavyofahamu Serikali imezuia uingizaji wa bidhaa kutoka nje ambazo zinaweza kuzalishwa na wawekezaji wa ndani ya nchi,” alisema.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Patrick Mongella alisema kuwa TIB ikiwa benki ya kisera inatekeleza kwa vitendo juhudi za serikali kwa kuwezesha uwekezaji wa viwanda nchini ili kuongeza ajira na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

“Benki ya Maendeleo TIB ni taasisi ya kifedha ambayo imekuwa ikisaidia nchi katika ukuaji wa uchumi na maendeleo katika sekta za kimkakati, hivyo tunatekeleza mikakati ya Serikali inayolenga kuchagiza maendeleo ya haraka ya kiuchumi,” alisema.
Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Patrick Mongella (wapili kulia) akitoa maelezo kwa Mgeni Rasmi wa Ufunguzi wa Maonesho ya Wiki ya Viwanda ya Mkoa wa Pwani, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya (watatu kushoto). Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (wapili kushoto).
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya (watatu kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (wapili kushoto) wakiangalia nyaya za umeme zinazozalishwa na Kampuni ya Konnectt Wire moja ya wateja waliowezehswa na Benki ya Maendeleo TIB.
Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Patrick Mongella akimkabidhi zawadi Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad