NCHI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUWAJENGEA UWEZO WATAALAM WA JIOLOJIA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 24 October 2019

NCHI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUWAJENGEA UWEZO WATAALAM WA JIOLOJIA

Na Asteria Muhozya, DSM
Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa wito kwa kuzitaka nchi za Afrika kujenga uwezo kwa Wataalam wa ndani wa Jiolojia ili kuwawezesha kujenga uwezo wa tafiti za rasilimali madini ili pindi nchi au taasisi wafadhili wanapoacha kufadhili, mamlaka husika ziwe kwenye nafasi ya kuendeleza shughuli hizo.

Waziri Biteko ameyasema hayo Oktoba 24, 2019 wakati akifungua Mkutano wa 36 wa Wataalam wa Jiolojia kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao wanakutana jijini Dar es Salaam. 

Mkutano huo unalenga katika kuwapatia wataalam hao mafunzo yanayogusa masuala mabalimbali kuhusu sekta ya Madini ikiwemo kubadilishana uzoefu katika utafutaji rasilimali madini na kuangalia namna bora ya kuendeleza rasilimali hizo ili kuhakikisha kwamba zinayanufaisha mataifa husika. 
Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kujifunza na kutumia vyema uzoefu mzuri utakaotolewa na mataifa mengine ili kuwezesha kuongeza thamani  katika kutekeleza majukumu  ya taasisi zao  katika uendelezaji wa rasilimali madini.

‘’ Afrika lazima tujifunze wenyewe kuendeleza na kujenga miradi yetu wenyewe. Katika mkutano yapasa kujiuliza siku Wafadhili wetu Umoja wa Ulaya na  taasisi nyingine zinazofadhili mafunzo haya zikiacha tutaweza kujisimamia wenyewe?,’’ amehoji Waziri Biteko.
Amesema kwa upande wa Tanzania kama taifa linaamini katika kuwajengea uwezo wataalam wa ndani ambapo tayari serikali imechukua hatua kadhaa za kuhakikisha zinawendeleza wataalam wake ili kuwezesha taifa kuzalisha wataalam waliobobea katika taaluma ya jiolojia na ambao watakuwa na mchango katika utafutaji wa rasilimali madini.

Amesema mradi huo wa kutoa Mafunzo kwa Taasisi za Jiolojia Afrika unafadiliwa na Umoja wa Ulaya pamoja na taasisi nyingine 12 ambapo tangu kuanzishwa kwa mradi huo mnamo mwaka 2017, tayari umewezesha kuwapatia mafunzo wataalam wapatao 1,100 kutoka Mataifa mbalimbali ya Afrika huku wataalam 30 wa Tanzania wakiwa wamepatiwa mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkuu wa Idara ya Ushirikiano  Kutoka Umoja wa Ulaya, Jose Dorreia Nunes, amewataka washiriki wa mkutano huo kutafakari namna rasimali hizo zitakavyozinufaisha nchi zao ikizingatiwa kwamba madini ni chanzo kikubwa cha mapato kwa nchi za Afrika hivyo ni muda sahihi kupitia mafunzo yanayotolewa na Umoja huo yawezeshe kujenga uwezo wa wataalam wa ndani katika kutafiti, kusimamia na kuendeleza rasilimali katika nchi zao.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Yorkberth Myumbilwa akizungumza na waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo amesema mafunzo yanayotolewa na Taasisi wafadhili yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yanagusa moja kwa moja shughuli zinazofanywa na taasisi hizo zikiwemo tafiti, wingi wa mashapo, urithi wa Jiolojia, namna ya kuhifadhi data na masuala mengine.
Ameongeza kwamba, suala la kukutanishwa na taasisi nyingine lina umuhimu kwa GST kwa kuwa linawezesha kujenga mahusiano mapya na Taasisi nyingine za Jiolojia kutoka nchi nyingine. 

Nchi zinazoshiriki mkutano unafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 24 – 25 Oktoba, 2019 ni pamoja na Tanzania, Namibia, Sengel Morroco, Kenya, Afrika Kusini , Rwanda, Zambia na Ghana.
 Waziri wa Madini Doto Bteko akifungua Mkutano wa 36 wa Watalaam wa Jiolojia kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
 Wataalam wa Jiolojia kutoka nchi mbalimbali wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Wataalam wa Jiolojia. 
 Waziri wa Madini Doto Biteko akiteta jambo na baadhi ya Wataalam wa Jiolojia kutoka Mataifa mbalimbali.
Waziri wa Madini Doto Biteko katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mkutano wa 36 wa Wataalam wa Jiolojia kutoka nchi mbalimbali za Afrika unaofanyika Jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad