Na Munir Shemweta, WANMM HANDENI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula amewatuliza wananchi wa kijiji cha Sindeni kilichopo Tarafa ya
Sindeni wilayani Handeni mkoani Tanga kufuatia mgogoro kati yao na
Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhusu mpaka baina ya kijiji cha
Sindeni na Shamba la Miti la Korogwe.
Dkt Mabula aliwatuliza wananchi hao baada ya kufika katika shamba la
Miti la Korogwe lililopo wilayani Handeni kukagua maendeleo ya Ujenzi
wa ofisi na Nyumba za Watumishi za TFS zinazojengwa na Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) akiwa katika ziara yake ya siku mbili katika
mkoa wa Tanga.
Dkt Mabula ametaka idara ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya
Handeni ikisimamiwa na Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini kuhakikisha
inafanya uhakiki wa mpaka kati ya TFS na kijiji cha Sindeni na kuweka
alama ili kukomesha mgogoro huo unaozuka mara kwa mara.
‘Kitakachofanyika ni uhakiki wa mipaka ya kijiji chenu kinaishia wapi,
TFS wanaishia wapi, NARCO wanaishia wapi, tutaheshimu mipaka na
nyaraka zilizoanzisha vijiji vyenu’’ alisema dkt Mabula.
Uamuzi wa Dkt Mabula kutoa maagizo hayo unafuatia wananchi wa kijiji
hicho kulalamika mbele ya Naibu Waziri kuwa Wakala wa Huduma za Misitu
(TFS) uliongeza eneo inalomiliki katika shamba hilo kwa kuingia ndani
ya eneo la kijiji cha Sindeni jambo linalochochea mgogoro kati ya
pande hizo.
Ally Mhina mkazi wa kijiji cha Sindeni alimueleza Naibu Waziri wa
Ardhi kuwa, TFS iliacha eneo lake la asili na kuongeza eneo lingine
kuingia kijiji cha Sindeni wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Kwa upande wake Meneja wa Shamba la Miti la Korogwe Pregreen Mushi
alisema, wenyeji wa Sindeni walivamia eneo la Wakala wa Huduma za
Misitu huku wale wa Kwamatuko na Kwaingoma wakiuza maeneo ya hifadhi
kwa jamii ya wafugaji na Mkuu wa Wilaya ya Handeni alishatoa agizo
wote waliovamia kuondoka eneo la hifadhi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe alisema alishashughulikia
mgogoro huo na kuwataka wasioridhika wasioridhika na utatuzi wake
kwenda mahakamani na kufafanua kuwa katika jitihada zake za kutafuta
suluhu ya mgogoro huo baadhi ya wananchi walikubali kuwepo msitu huo
na sasa wananufaika kwa kupatiwa huduma mbalimbali ikiwemo ujenzi wa
shule.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mustafa Beleko
alisema pamoja maagizo ya Naibu Waziri kuhusiana na uhakiki wa mpaka
kati ya kijiji cha Sindeni na TFS lakini wao kama halmashauri
watachukua ramani ya kijiji wakati wa uhakiki mipaka ili kukomesha
kuibuka kwa mgogoro huo mara kwa mara.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza
pia kuweka alama za mpaka kati ya Wakala wa Huduma za Misitu na NARCO
kufuatia suluhu ya mpaka kati ya taasisi hizo mbili za serikali
kushindikana kutekelezwa kwa madai kuwa NARCO ilikaa kimya katika
utekelezaji makubaliano ya kuchangia gharama za ubainishaji mipaka.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Shamba la Miti la Shume Lushoto mkoani Tanga linalomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu katika wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi inayosimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Lushoto January Lugangika.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sindeni katika eneo la Shamba la Miti la Korogwe lililopo Handeni aliposikiliza malalamiko yao ya mpaka kati yao na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Ofisi ya Mkuu
wa Wilaya ya Muheza unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa jana
usiku akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayofanywa na
Shirika hilo katika mkoa wa Tanga. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa
Wilaya ya Muheza Mhandisi Mawanaasha Tumbo.
No comments:
Post a Comment