HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 8, 2019

Waziri Ummy azikaribisha nchi za SADC kutibiwa Muhimbili, MOI na JKCI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu  amezikaribisha nchi wanachama wa SADC kutumia huduma za ubingwa wa juu zinazopatika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Ummy ameyasema hayo leo alipotembelea  mabanda ya MNH, MOI na JKCI yanayoshiriki maonesho ya viwanda yanayofanyika katika viwanja vya ukumbi  wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kuelekea mkutano mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi zilizopo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao utaanza mapema wiki hii.

Waziri Ummy amesema Wizara yake imeweka wataalam wa afya ili kutoa huduma kwa wajumbe wa mkutano wa SADC watakaohitaji huduma za matibabu pamoja na wananchi wengine watakaokuwapo katika viwanja hivyo.

Aidha ameziomba nchi za SADC kupata huduma za ubingwa wa juu zinazopatikana MNH kama upandikizaji figo (kidney transplant), upandikizaji watoto vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implant), tiba kwa njia ya radiolojia (interventional radiology).

Kwa upande wa MOI, Waziri Ummy amezitaka nchi za SADC kuja kupata huduma za upasuaji wa mivunjiko ya kikombe cha mfupa wa nyonga, upasuaji wa kuweka nyonga na magoti bandia na upasuaji wa magoti, ubongo na mgongo kupitia matundu madogo.

Kwa upande wa JKCI amezitaka nchi za SADC kupata huduma za tiba ya umeme wa moyo, kuzibua mishipa ya damu na upasuaji wa kufungua kifua kwa ajili ya kurekebisha valvu au matundu kwenye moyo.

 “Kama Wizara tumeweka wataalam wa afya hapa eneo la mkutano  ili kutoa huduma kwa wajumbe wa nchi za SADC. Wataalam wetu wa Muhimbili, MOI, JKCI na pamoja  Hospitali ya Lugalo wako tayari kuhudumia wageni wetu ambao watapata changamoto yoyote ya kiafya,” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ametembelea kliniki maalumu zilizoandaliwa kwa ajili ya kuhudumia wageni na wananchi mbalimbali wanaotembelea maonesho ya viwanda na maandalizi ya mkutano wa 39 wa SADC.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alipotembelea leo. Kushoto ni Dkt. Juma Mfinanga akiwa na Waziri Ummy Mwalimu baada ya kumweleza jinsi MNH ilivyojiandaa kuwahudumia wajumbe wa mkutano wa SADC pamoja na wananchi wengine.
 Daktari Bingwa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dkt. William Mugisha (kulia) akimweleza Waziri Ummy Mwalimu kuhusu huduma ya upasuaji wa mivunjiko ya kikombe cha mfupa wa nyonga alipotembelea banda la MOI leo.
 Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Pedro Pallangyo akimweleza Waziri Ummy Mwalimu huduma zinazopatika JKCI zikiwamo huduma za tiba ya umeme wa moyo na  kuzibua mishipa ya damu.
 Daktari wa Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam, Dkt. Andrew Laiser akieleza jinsi walivyojiandaa kuhudumia wajumbe wa mkutano wa SADC na wananchi wengine.
 Waziri Ummy Mwalimu akisoma jarida la Muhimbili linaloeleza huduma mbalimbali za afya zinazopatikana MNH. Kulia ni Dkt. Juma Mfinanga akimweleza jambo Waziri.
  Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, wataalam wa afya pamoja na wataalam wengine wakiwa katika viwanja vya ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kukagua mabanda na kliniki zitakazotumika kuhudumia wajumbe wa mkutano wa SADC.
Wataalam wa afya wa Muhimbili, MOI, JKCI na Hospitali ya Lugalo wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri Ummy Mwalimu leo katika viwanja vya ukumbi  wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad