HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 19 August 2019

Dkt. Maleko: Andaeni Maandiko ya Miradi yenye fursa pana za kiuchumi

 Na Mwandishi wetu, Mtwara

Wataalam wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini wametakiwa kuandika maandiko bora yenye kuzingatia mkondo mzima wa ongezeko la thamani (value chains) ili kuwezesha ukuaji wa uchumi jumuishi nchini.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Dkt. Jilly Maleko wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo watalaam hao wa mamlaka za serikali za mitaa juu ya uandishi bora wa maandiko ya miradi.

Akizungumza na watalaam hao mkoani Mtwara, Dkt. Maleko alisema kuwa wataalam hao hawana budi kujiridhisha na ubunifu wa miradi yao kuwa inaweza kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.

“Tunapobuni miradi ya kiuchumi ni muhimu kuzingatia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo husika kwa kuzingatia mkondo mzima wa ongezeko la thamani (value chains) ili kuwezesha ukuaji wa uchumi jumuishi,” alisema.

Dkt. Maleko aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujenga uchumi wa viwanda katika kufikia azma ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 hivyo uandishi bora wa maandiko ya miradi unaongeza tija kufika malengo hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Patrick Mongella alisema kuwa warsha hiyo inalenga kuwajengea uwezo wataalam hao ili kukabiliana na changamoto za uandishi wa maandiko bora yanayokopesheka.

Aliongeza kuwa warsha hiyo inayoendeshwa kwa ushirikiano kati Benki ya Maendeleo TIB na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa imelenga kuongeza tija ya uwekezaji unaofanywa na Serikali za Mitaa nchini.

“Warsha hii inalenga kuwajenga watumishi katika nyanja mbalimbali kama kuandaa miradi ya kibiashara katika manispaa na wilaya kama vile vituo vya mabasi na maeneo ya viwanda, ili kuhakikisha maandiko hayo yanakopesheka,” alisema.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mwakilishi kutoka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, Bw. Rashid Kitambulio alisema takribani watumishi 150 wanatarajia kujengewa uwezo wa mambo mbalimbali kuhusiana na kuandaa miradi ya kimaendeleo ambayo italeta faida kwa wananchi, mbali na hilo pia watafundishwa jinsi ya kuomba mikopo ya miradi ya kimaendeleo.

Aliongeza kuwa watumishi hawa wanatoka katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

Warsha hii ni matunda ya makubaliano kati ya Benki ya Maendeleo TIB na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ikiwa ni moja ya makubaliano waliyoyafikia mnamo mwezi Septemba 2017 ambapo walikubaliana kuwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa katika uandishi bora wa maandiko ya miradi.

Hii ni warsha ya tano tangu warsha hizi kuanza rasmi mwaka 2018, tayari warsha kama hii imefanyika katika Kanda ya Kaskazini (Arusha), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Kanda ya Kati (Dodoma) ambapo takriban watumishi 450 wamefaidika na mafunzo hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Dkt. Jilly Maleko (aliyesimama) akifungua warsha ya kuwajengea uwezo watalaam wa mamlaka za serikali za mitaa juu ya uandishi bora wa maandiko ya miradi.
Mwakilishi kutoka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, Bw. Rashid Kitambulio (aliyesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo.
Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Patrick Mongella akihimiza jambo wakati akifanya wasilisho kuhusu Programu maalum na Huduma za Fedha za Benki ya Maendeleo TIB.


Washiriki wa warsha ya kuwajengea uwezo watalaam wa mamlaka za serikali za mitaa juu ya uandishi bora wa maandiko ya miradi wakifuatilia mawasilisho wakati wa warsha hiyo.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad