HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 10, 2019

KAMPASI ZA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA KUSHINDANISHWA KIUTENDAJI ILI KUBORESHA HUDUMA ZAKE

Serikali imepanga kushindanisha huduma zinazotolewa na kampasi za Chuo cha Utumishi wa Umma nchini ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wa chuo hicho, lengo likiwa ni kuboresha huduma zinazotolewa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa ziarayake ya kikazi mkoani Tabora ya kutembelea Chuo cha Utumishi wa Umma, kampasi ya Tabora ili kukagua utekelezaji wa miradi na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa chuo hicho.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, kampasi zitakazoshindanishwa ni za Dar es Salaam, Mtwara, Tabora, Singida, Tanga na Mbeya ambapo ameweka bayana kuwa, kampasi itakayoshinda katika utoaji wa huduma bora   itapewa tuzo.
“Utawekwa utaratibu ambao utashindanisha kampasi zote kwa kuzingatia vigezo stahiki ili kumpata mshindi anayestahili" Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, mashindano hayo yatakuwa ni chachu ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa kila mtumishi na kuongeza kuwa ufanisi huo utakiletea sifa chuo kuwa taasisi mahiri inayotoa mafunzo ya uhazili, menejimenti ya ofisi, utunzaji kumbukumbu na nyaraka za kiutumishi.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa kampasi zote za chuo hicho kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kutimiza malengo ya chuo.
Akizungumzia kuhusu uendeshaji wa kampasi ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameiagiza menejimenti ya chuo hicho kuhakikisha kampasi hiyo inajiendesha kwa mapato ya ndani badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikali kuu.

“Lazima muwe na vyanzo mbadala vya mapato ya ndani vitakavyosaidia uendeshaji wa ofisi. Mapato hayo yatoke kwenye vyanzo halali vinavyozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo” Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amehitimisha ziara yake ya kikazi kwa kutembelea majengo ya chuo hicho katika kampasi ya Tabora na kujionea maabara ya kompyuta, maabara za mashine za kuchapa, maktaba,mabweni ya wanafunzi na jengo jipya la ghorofa mbili linalotarajiwa kutumika kwa matumizi ya maktaba, chumba cha kompyuta, ofisi,  madarasa na kumbi za mikutano.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kampasi ya Tabora katika kikao kilichofanyika chuoni hapo mkoani Tabora.
Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kampasi ya Tabora, Dkt. Ramadhan Marijani akijibu hoja za Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kushoto) wakati wa kikao kati ya Naibu Waziri na watumishi wa chuo hicho.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akichapa kwa mashine alipotembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kampasi ya Tabora. Wanaoshuhudia ni Kaimu Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Emmanuel Shindika (kushoto) na Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kampasi ya Tabora, Dkt. Ramadhan Marijani.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akikagua jengo jipya la ghorofa mbili la Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kampasi ya Tabora. Wengine ni Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Tabora, Dkt. Ramadhan Marijani na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Kaimu Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) akiwasilisha ripoti ya chuo wakati wa kikao kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya UtumishiwaUmma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kulia) na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kampasi ya Tabora.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad