HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 21, 2019

Dar es Salaam Bingwa UMISSETTA 2019

Na Mathew Kwembe, Mtwara
Mashindano ya 40 ya Umoja wa Shule za Sekondari Tanzania UMISSETA yamefungwa rasmi leo katika uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Profesa Joyce Ndalichako kwa mkoa wa Dar es salaam kutangazwa kuwa mshindi wa jumla wa UMISSETA 2019.

Katika mashindano ya mwaka huu jumla ya mikoa 28 ikiwemo miwili ya Unguja na pemba ilishiriki mashindano hayo.

Mkoa wa Dar es salaam ulishika nafasi ya kwanza baada ya washiriki wake kufanya vizuri kwenye michezo ya mpira wa kikapu wasichana ambapo walishika nafasi ya kwanza, wavu walishika nafasi ya pili wasichana na wavulana, soka walishika nafasi ya tatu wasichana.

Pia washiriki kutoka mkoa wa Dar es salaam walifanya vizuri katika mchezo wa mpira wa meza ambapo wasichana walishika nafasi ya kwanza, netiboli pia walishika nafasi ya kwanza, na riadha wavulana walishika nafasi ya pili.

 Nafasi ya pili ilichukuliwa na Morogoro,nafasi ya tatu ilienda  Mwanza, nafasi ya nne ilichukuliwa na Tabora na Mbeya ulishika nafasi ya tano.

Kabla ya kutoa hotuba yake, Mhe. Ndalichako na wageni waalikwa walipata fursa ya kushuhudia pambano kali la fainali soka wavulana kati ya Songwe na Ruvuma ambapo mshindi ilibidi apatikane kwa njia ya penati baada ya timu hizo kufungana goli 1-1.

Katika hatua ya penati Ruvuma ilifanikiwa kuchukua ubingwa  wa UMISSETA wavulana baada ya kuifunga timu ngumu ya Songwe kwa penati 10-9.

Mshindi wa tatu Soka wavulana ni Mwanza ambapo golikipa bora kwa upande wa soka wavulana ni Nice kahemele wa Ruvuma na kwa wasichana ni Safina Haule pia kutoka mkoa wa Ruvuma.

Mfungaji bora kwa upande wa soka wavulana ni Paul Nyerere wa Mwanza ambaye alifanikiwa kupata magoli 6 huku mfungaji bora kwa upande wa soka wasichana ni Aisha Hamisi wa Mwanza ambaye alifunga magoli 13.

Mchezaji bora wa mashindano ya UMISSETA 2019 ni John Chinguku kwa upande wa soka wavulana kutoka Ruvuma na kwa upande wa soka wasichana mchezaji bora ni Ester Daniel kutoka Mwanza.

Kwa upande wa wachezaji walioonyesha mchezo mzuri (fair play) kwa soka wavulana ni Jackson Simba wa Ruvuma na kwa soka wasichana ni Lucy Mwenda pia kutoka mkoa wa Ruvuma.

Mapema kabla  ya kugawa zawadi kwa washindi mbalimbali, Waziri Ndalichako alisema kuwa serikali inayathamini sana mashindano ya UMISSETA kama sehemu sahihi ya kupata wanamichezo wenye vipaji watakaoweza kutumika kuendeleza sekta ya michezo nchini.

Hivyo akataka wizara yake ihakikishe kuwa pindi wanapofanya ukaguzi shuleni wahakikishe pia somo la michezo linakuwemo.

Pia akataka kila shule inayosajiliwa ihakikishe kuwa inakuwa na viwanja vya michezo ili kuwawezesha watoto watakaosoma katika shule hizo kupata fursa ya kucheza michezo mbalimbali.

Waziri Ndalichako amesema kuwa michezo ni sehemu nuhimu sana kwa wanafunzi kwani inawajengea afya ya akili pindi wanaposhiriki michezo mbalimbali na hivyo kuwawezesha kusoma vizuri.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Mhe.Mwita Waitara amesema kuwa Ofisi yake itaendelea kuhakikisha kuwa michezo ya UMISSETA inafanyika ili kuwawezesha vijana wengi wenye vipaji kuonyesha uwezo wao na hivyo kupata fursa ya kujiendeleza kimichezo.
 Mgeni Rasmi Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (katikati aliyevaa tracksuit ya bluu) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa  na kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu. Mhe. Mwita Waitara wakienda kutoa zawadi kwa washindi wa UMISSETA 2019 katika uwanja wa Nangwanda, mjini Mtwara  
 Mabingwa wapya soka wavulana wa UMISSETA 2019 timu ya mkoa wa Ruvuma mara baada kukabidhiwa kombe lao na  Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Profesa Joyce Ndalichako. Ruvuma iliifunga timu ya mkoa wa Songwe kwa penati 10-9
Mchezaji bora wa mashindano ya UMISSETA 2019 John Chinguku kutoka Mkoa wa Ruvuma akipokea tuzo yake kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais TAMISEMI Benjamin Oganga jana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad