WANANCHI 1,000 kati ya wakazi 4,250 wa Kijiji cha Getanyamba Wilayani
Mbulu Mkoani Manyara, wamenufaika na mradi mpya wa maji baada ya
kuangaika kwa muda mrefu na changamoto ya kuchota maji korongoni.
Hata hivyo, mradi huo utawanufaisha watu 1,000 pekee kwenye kijiji
hicho chenye wakazi 4,250 na wengine 3,250 bado wataendelea kukabiliwa
na changamoto ya ukosefu wa maji.
Mratibu wa pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP) Eliminata Awet
akizungumza baada ya mradi huo kuzinduliwa na mwenge wa uhuru alisema
umewezeshwa na Norwegian Church Aid (NCA).
Awet alisema lengo la mradi huo ni kusaidia kupunguza tatizo la maji
kwa wananchi hao waliokuwa wanafuata huduma hiyo kwa kuchota maji
korongoni umbali wa kilomita tatu hadi tano.
Alisema hadi kukamilika kwa mradi huo umegharimu sh. 61 milioni ambapo
4CCP ilitoa sh51.9 milioni, wananchi wamechangia nguvu zao
zilizothaminishwa sh10 milioni na halmashauri ya wilaya ya Mbulu
ikatoa wataalamu.
"Faida ya mradi huu ni kuwezesha wananchi hao kupata huduma hiyo kwa
ukaribu ili waweze kupata muda zaidi wa kufanya shughuli zao nyingine
nyingine za kujiletea maendeleo," alisema Awet.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Mzee Mkongea Ally akizungumza
baada ya kuzindua mradi huo aliwapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa
kushiriki kuufanikisha ikiwemo kubeba kokoto na kuzoa mchanga.
"Pamoja na hayo nawashukuru viongozi wa wilaya ya Mbulu kwa
ushirikiano na jamii kufanikisha maendeleo ila wananchi wa Getanyamba
hakikisheni mnautunza vyema mradi huu," alisema Ally.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga aliwashukuru wadau wa
maendeleo 4CCP kwa kufanikisha mradi huo mkubwa wa maji ambao
utasaidia jamii ya eneo hilo.
"Mara nyingi 4CCP wamekuwa mstari wa mbele kusaidiana na serikali
katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wetu wa
Mbulu, nawashukuru sana tutaendelea kuwaunga mkono," alisema Mofuga.
Mkazi wa kijiji hicho Ezekiel Bayo aliipongeza 4CCP na Norwegian
Church Aid kwa kuwezesha mradi huo ambao kwa kiasi kikubwa umewakomboa
wananchi wa eneo hilo.
"Tulikuwa tunategemea kupata huduma ya maji kutoka kwenye korongo la
Haydom ambayo hayakuwa masafi wala salama, ila baada ya kuwepo kwa
mradi huu jamii ya eneo hili inafaidika," alisema Bayo.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Mzee Mkongea Ally akipanda mti kwenye mradi wa maji wa Kijiji cha Getanyamba Wilayani Mbulu Mkoan Mkoani Manyara, wenye thamani ya shilingi milioni 61.9 ambapo 4CCP walitoa shilingi milioni 51.9 na wananchi wakachangia nguvu zilizothaminishwa kwa shilingi milioni 10.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Getanyamba Wilayani Mbulu Mkoani
Manyara wakishuhudia ufunguzi wa mradi wa maji wenye thamani ya
shilingi milioni 61.9 ambapo kituo cha pembe nne za utamaduni Haydom
kilichangia shilingi milioni 51.9 na wananchi shilingi milioni 10.
No comments:
Post a Comment