HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 1, 2019

UFAFANUZI WA TAARIFA INAYOSAMBAZWA NA WAFANYABIASHARA KATIKA UHAKIKI WA BIDHAA ZILIZOFUNGASHWA

Kumekuwepo na taarifa ambayo imesambazwa katika mitandao ya kijamii kutoka kwa mfanyabiashara mmoja katika Mkoa wa Morogoro akilalamika kuitwa katika ofisi za Wakala wa Vipimo kwa ajili ya kulipa faini kwa kosa alilolitenda la kuuza bidhaa zake pasipo kutumia mizani.

Napenda kuufahamisha umma kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura 340 Wakala wa Vipimo ina wajibu wa kukagua bidhaa zilizofungashwa Viwandani na katika maduka ya jumla ili kuhakiki usahihi wa vipimo kabla bidhaa hizo hazijamfikia mlaji wa Mwisho.

Kumekuwa na udanganyifu ambao unafanywa na wafanyabiashara wachache wasio waaminifu kwa kupunguza uzito wa bidhaa zilizofungashwa au kufungasha bidhaa pungufu kwenye viroba hususani unga wa mahindi ili kuwapunja wateja wanaoenda kununua bidhaa katika maduka yao.

Katika ukaguzi uliofanyika Mkoani Morogoro tarehe 29 Aprili, 2019 wafanyabiashara 29 wa maduka ya jumla walikaguliwa. Baadhi ya
waliokaguliwa walikutwa na kosa la kuuza bidhaa hususani unga wa mahindi ukiwa na uzito pungufu. Wafanyabiashara walijaziwa fomu maalumu za wito kuwataka wafike ofisi ya Wakala wa Vipimo Morogoro kwa ajili ya hatua zaidi. Zoezi hili lilikuwa maalumu kukidhi malalamiko yaliyoletwa Wakala wa Vipimo na baadhi ya Wananchi wakilalamika kuwa bidhaa nyingi hususani unga wa mahindi haufikii vipimo ambavyo vinaonyeshwa katika vifungashio vya unga huo.

Kama utaratibu wa Wakala wa Vipimo ulivyo wafanyabiashara hao walijaziwa fomu za wito ili wafike ofisini kwa ajili ya kupewa elimu na ushauri ikibidi kutozwa faini au kufikishwa mahakamani. Kwa mfanyabiashara wa jumla kuwa na mizani katika eneo lake la biashara kunamhakikishia kupokea na kuuza bidhaa iliyotimia kulingana na kiasi kilichoandikwa katika mfuko au kifungashio.

Wakala wa Vipimo inatoa wito kwa wafanyabiashara wote kufanya biashara zao pasipo kukiuka taratibu na Sheria ambazo zimewekwa na itaendelea kufanya kaguzi mbalimbali kwa lengo la kuwalinda wananchi ili waweze kununua bidhaa kwa usahihi kulingana na thamani ya fedha wanazotoa.

Imetolewa na;
Afisa Mtendaji Mkuu
WAKALA WA VIPIMO

 Mkurugenzi  wa Huduma za Ufundi Stella Khawa(katikati) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuhakiki bidhaa zilizofungashwa kwa kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo
Maafisa wa Wakala wa Vipimo wakieleza umuhimu wa kuhakiki bidhaa zilizofungashwa kwa kutumia vipimo sahihi (Mizani).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad