Na Teresia Mhagama
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ametoa Wiki Moja kwa wasimamizi
wa mradi wa usambazaji umeme vijijini mkoani Morogoro kutoka Wizara ya
Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TANESCO kuhakikisha kuwa
wanatatua changamoto ya nguzo za umeme mkoani Morogoro.
Naibu Waziri alitoa agizo hilo, tarehe 23 Mei, 2019 mkoani Morogoro
wakati alipofanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini
wilayani Mvomero na Gairo na kuwasha umeme katika Kijiji cha Dibamba
wilayani Mvomero na Kijiji cha Sanganjeru wilayani Gairo.
Agizo la Naibu Waziri limekuja baada ya sampuli ya nguzo za mkandarasi
wa umeme mkoani Morogoro kupimwa na wataalam wa TANESCO na kuonekana
kuwa hazina vigezo huku mkandarasi huyo akidai kuwa sehemu ya nguzo
zake zinafaa kwa matumizi ya umeme.
" Hatutaki kuona mivutano kati ya wakandarasi na wasimamizi wa miradi
ya umeme vijijini kwani inachelewesha upelekaji umeme kwa wananchi
hivyo nawaagiza mtatue suala hili kwa kupima nguzo zote na Wizara
ipate taarifa ndani ya Wiki Moja."alisema Naibu Waziri
Kuhusu kasi ya mkandarasi anayesambaza umeme vijijini mkoani Morogoro,
kampuni ya State Grid, alisema kuwa, bado haridhishwi na kasi ya
mkandarasi huyo na kutoa onyo kuwa Serikali itamchukulia hatua endapo
hatatekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba.
Aidha alitoa agizo kwa wazalishaji wa vifaa vya umeme, wasambazaji na
wakandarasi wa umeme vijijini kutatua changamoto zao kwa haraka mara
zinapojitokeza ili kutochelewesha miradi ya umeme vijijini.
Akieleza kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali katika kazi ya
usambazaji umeme vijijini, alibainisha kuwa hadi sasa asilimia 57 ya
vijiji nchini tayari vimesambaziwa umeme kati ya Vijiji 12,268 huku
kazi hiyo ikiendelea na kwamba Tanzania ndiyo inayoongoza katika nchi
za Afrika Mashariki kwa usambazaji umeme vijijini.
" Wakati Serikali ya Awamu ya Tano, inaingia madarakani ilikuta vijiji
8783 havina umeme kati ya Vijiji 12,268, ndio ikaanza safari ya
kufikisha umeme kwenye vijiji hivyo kupitia miradi mbalimbali ikiwemo
huu wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza, mradi wa ujazilizi Awamu
ya Pili mzunguko wa kwanza na miradi mingine," alisema Mgalu
Kuhusu bei ya umeme aliendelea kusisitiza agizo la Serikali kuwa ni
elfu 27,000 tu, awe anasambaza mkandarasi wa umeme vijijini au TANESCO
ili kuleta usawa wa utoaji huduma kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akiwasha umeme katika Kijiji cha Dibamba wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Tabuhoteli wilayani Gairo Mkoa wa Morogoro wakati alipofika kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe na kulia ni Msimamizi wa mradi wa usambazaji umeme vijijini kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Ahmed Chinemba.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akikata utepe kuashia uwashaji umeme katika Kijiji cha Sanganjeru wilayani Gairo Mkoa wa Morogoro. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe.
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akitoa maelezo kuhusu kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa Kijiji cha Sanganjeru wilayani Gairo Mkoa wa Morogoro wakati alipofika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme na kuwasha rasmi umeme.
Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
(hayupo pichani) wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha
Tabuhoteli wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro.
No comments:
Post a Comment