HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 28, 2019

MAWAKALA WA FORODHA ARUSHA WAMUOMBA WAZIRI MKUU KUINGILIA KATI MGOGORO ULIOPO KATI YAO NA WAKALA WA VIPIMO

Na Woinde Shizza Michuzi TV, Arusha

CHAMA cha Mawakala wa Forodha(TAFFA) tawi la Namanga mkoani Arusha wamemwomba Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa kuingilia kati mgogoro kati yao na Wakala wa Vipimo (WMA) unaowalazimisha kulipia tozo mpya inayotozwa kwa kila bidhaa badala ya kutumia utaratibu wa awali wa kulipia tozo kwa mzigo wote.

Aidha wamesema hawapo tayari kufanya kazi na wakala hao hadi hapo watakapo onyeshwa hiyo sheria mpya ambayo wanalazimishwa kuitekeleza bila kuwepo kwa makubaliano yoyote kitendo ambacho kinawaumiza wao. 

Wametoa ombi hilo leo kwenye kikao chao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa TFFA Ismail Lukas ambacho kilichofanyika Namanga, wilayani Longido ambapo wamesema walikuwa wakitumia sheria ya zamani ya mwaka 2016 ambayo walikuwa wakilipia asilimia 0.2 ya thamani ya mzigo ambapo kiwango cha chini cha malipo ilikuwa shs 100,000 kwa mzigo.

Wamesema wanachopinga ni WMA kuamua kuwatoza malipo ya shilingi laki moja kwa kila aina ya bidhaa (item ) badala ya mzigo mzima Kama sheria inavyoelekeza .

"Tunamwomba Waziri Mkuu aje Namanga kuja kuzungumza na sisi kuhusu huu mgogoro kwani tukiendelea na utaratibu huu tutakosa wafanyabiashara kwani hakuna mtu aliye tayari kupata hasara kwani jinsi tunavyopandishiwa gharama za tozo ndivyo hivyo hivyo bei za bidhaa zitakavyopanda,"amesema Ismail.

Kwa upande wake Meneja wa Tawi wa kampuni ya EDPAC Wilson Mkanza amesema kwa hivi sasa hawapo tayari tena kufanya shughuli yoyote bila kupata muongozo wa sheria mpya inayowalazimu wao kutumia utaratibu mpya wa kulipa tozo ya laki moja kwa kila bidhaa badala ya mzigo Kama utaratibu wa awali. 

Amesema kuwa walipokea barua mnamo may 15 mwaka huu ya ufafanuzi wa kanuni ya ada za ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa zinazoingia nchini kutoka nje ya nchi kutoka kwa kaimu meneja wa wakala wa vipimo mkoa, Dismas Maturine inayohusu wao kulipia bidhaa moja moja badala ya kutozwa kwa mzigo mzima kama ilivyokuwa hapo awali bila kushirikishwa chochote kabla ya kupewa barua hiyo. 

Wakati huo huo Janeth Mero kutoka kampuni ya Beam Tanzania Ltd alisema kuwa, uwepo wa utaratibu huo wa kulipa kwa kwa mzigo mmoja mmoja unatengeneza mazingira ya rushwa, hivyo kuwataka kuendelea kwa ule utaratibu uliokuwepo wa awali ili waendelee kulipa bila migogoro yoyote.

Mkurugenzi wa Ufundi kutoka wakala wa vipimo makao makuu, Stella Kahwa alisema kuwa, amesikiliza malalamiko hayo na yamepokelewa na yanaendelea kufanyiwa kazi na kusema kuwa, utaratibu utakaoendelea kutumika ni ule uliokuwa ukitumika awali wa kulipia laki moja kwa mzigo.
 mawakala wakisikiliza mwenyekiti kwa makini
 mwenyekiti wa Chama cha mawakala wa forodha( TAFFA)Ismail Lukas akiongea na wanachama wenzake. 
Mkurugenzi wa ifundi Stella kahwa akiongea na waandishi ofisini kwake

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad