HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 14, 2019

KITUO KIKUBWA CHA BIASHARA CHA AFRIKA MASHARIKI KUJENGWA NYAKANAZI- KAGERA

Na Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali inatekeleza mpango mkakati wa kujenga Kituo kikumbwa cha Biashara cha Afrika Mashariki katika eneo la Nyakanazi Mkoani Kagera ili kuwanufaisha wananchi wanozunguka eneo hilo na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki- EAC.

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalaum Mhe. Halima Abdalallah Bulembo, alieuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kujenga Kituo cha Biashara katika mkoa wa Kagera unaopakana na nchi nyingi za EAC.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, ujenzi wa Kituo cha Biashara eneo la Nyakanazi utawezesha wananchi wa Tanzania pamoja na nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda kulifikia soko hilo.

Akijibu swali la Msingi la Mbunge huyo kuhusu mpango wa Serikali wa kuifanya Kagera ifaidike na uchumi wa kijiografia, Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati mkoani humo ukiwemo mradi wa Reli yenye kiwango cha Kimataifa (SGR) kipande cha Isaka- Rusumo chenye urefu wa kilometa 371 na ukarabati wa barabara ya Lusanga- Rusumo yenye urefu wa kilometa 91.

Aidha inatekeleza mradi wa umeme wa megawati 80 katika mipaka ya Rusumo na Mtukula kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kibiashara na nchi jirani za Rwanda na Uganda.

Naibu Waziri Dkt. Kijaji alisema, mazao ya wakulima wa Kagera na bidhaa za baadhi ya viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu vinafaidika kimasoko na jiografia ya Mkoa huo ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kusindika minofu ya Samaki cha Fish Co Ltd na Supreme Perch Ltd.

Viwanda vingine ni Ambiance Distillers Tanzania Ltd kinachozalisha vinywaji vikali, Bunena Development Co. Ltd, NK Botling Co. Ltd na Kabanga Bottlers Co. Ltd vinavyozalisha maji ya kunywa na kiwanda cha Mayawa kinachosindika wine ya Rosella na juisi.

Alisema kuwa, sambamba na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, Serikali kupitia Mamlaka ya Biashara (Tan Trade), ilitoa mafunzo ya kuhamasisha kuanzishwa kwa vikundi vya kurasimisha biashara mipakani katika vituo vya Kabanga, Rusumo na Mtukula vinavyopakana na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda ili kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia fursa za kiuchumi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji(Mb).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad