HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 23, 2019

ZRB YATOA MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSIANA NA WAJIBU WAO KATIKA KODI

Na Faki Mjaka- Maelezo Zanzibar
Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) imefanya mafunzo kwa Waandishi wa habari juu ya ulipaji Kodi ikiwa ni mkakati wake wa utekelezaji wa ajenda ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Katika mafunzo hayo yaliyofanyika Ofisini kwao Mazizini, ZRB imewataka Waandishi wa Habari kuielimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa kulipa Kodi kwa maendeleo ya nchi na watu wake.

Akizungumza na Waandishi hao Meneja uhusiano na huduma kwa walipa Kodi ZRB Shaban Yahya Ramadhan amesema Waandishi wana wajibu wa kuijengea hamasa Jamii juu ya ulipaji Kodi kupitia vipindi na taarifa wanazozitoa katika Vyombo vyao.

Amewataka Waandishi hao kutoa ushirikiano kwa Maofisa wa Kodi ili kufanikisha makusanyo ya Kodi yaliyopangwa.

“Lengo la 17 la SDGs linatutaka sisi kushirikiana na Wadau wengine katika kufikia malengo tuliyojipangia na miongoni mwa Wadau wetu muhimu ni nyinyi ambao muna wajibu wa kutengeneza hamasa jamii ilipe Kodi” Alisema Meneja Uhusiano.

Kwa upande wake Afisa uhusiano wa ZRB Makame Khamis Mohamed wakati akielezea umuhimu wa Kodi amesema hutumika kuendeshea Serikali ikiwemo kulipa Mishahara ya Wafayakazi, Wawakilishi na watoa huduma nyingine.

Amesema Kodi inayokusanywa na ZRB huingizwa katika Hazina ya Serikali na baadaye hurudishwa kwa Wananchi kwa kuhudumia shughuli mbali mbali ikiwemo miundominu ya barabara, elimu, umeme na maji.

Ameongeza kuwa Kodi hiyo hutumika pia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi kwa kulipa mishahara kwa wakati watendaji wa Vikosi vya ulinzi na usalama.

Akielezea changamoto zinazoikabili ZRB Makame amesema ni pamoja na kuwepo kwa Wafanyabiashara wanaofanya biashara bila kusajiliwa kulipa kodi. Changamoto nyingine ni Wauzaji kutotoa Risiti kwa Wateja na Wanunuzi kushindwa kudai Risiti wakati wa manunuzi.

Kwa upande wao Washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru ZRB kwa kuwajengea uwezo kuhusu Kodi na kuahidi kuifanyia kazi elimu waliyoipata kwa faida yao na jamii kwa ujumla.

Aidha Waandishi hao wametoa wito kwa Taasisi zingine kuiga mfano wa ZRB katika kushirikiana na wadau wake ili kufikia malengo yaliyopangwa.

Mafunzo hayo yamekuja ikiwa ni utekelezaji wa lengo la 17 la ajenda ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (SDGs) linalohusu ushirikiano na Wadau katika kufikia Malengo.
 Meneja Uhusiano na Huduma kwa Walipa Kodi Shaban Yahya Ramadhan (kushoto) akitoa Elimu kwa Waandishi wa Habari kuhusiana na Utekelezaji wa SDGs katika mafunzo ya siku moja ya Wajibu wa Muandishi wa Habari katika Kodi na Utekelezaji wa SDG yaliofanyika Ofisi ya ZRB Mazizini mjini Unguja.
 Afisa Uhusiano Bodi ya Mapato Zanzibar(ZRB)Makame Khamis Mohd akitoa elimu kwa Waandishi wa Habari kuhusiana na Mahusiano na Huduma kwa Walipa Kodi katika mafunzo ya siku moja ya Wajibu wa Muandishi wa Habari katika Kodi na Utekelezaji wa SDG yaliofanyika Ofisi ya ZRB Mazizini mjini Unguja. 
 Muandishi wa Habari wa Hits Fm Kudra Mawazo akiuliza maswali katika mafunzo ya siku moja ya Wajibu wa Muandishi wa Habari katika Kodi na Utekelezaji wa SDG yaliofanyika Ofisi ya ZRB Mazizini mjini Unguja.
Muandishi wa Habari wa Habari Maelezo Faki Mjaka akiuliza maswali katika mafunzo ya siku moja ya Wajibu wa Muandishi wa Habari katika Kodi na Utekelezaji wa SDG yaliofanyika Ofisi ya ZRB Mazizini mjini Unguja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad