Na Ahmed Mahmoud, Arusha
Wahitimu nchini wameaswa kutumia elimu yao vizuri katika kuwa chachu
ya kuwakomboa wengine katika changamoto mbalimbali zinazowakabili
ndani ya Jamii.
Hayo yalisemwa Jana na Mwenyekiti wa umoja wa wanawake ccm mkoa wa
Arusha, Yasmin Bachu wakati akizungumza katika mahafali ya 20 ya
wanafunzi 154 wa kidato cha sita katika shule ya sekondari Enaboishu
iliyopo mjini hapa.
Alisema kuwa, wanapaswa kutumia elimu hiyo waliyoipata kuwa watatuzi
wa changamoto mbalimbali katika jamii kwani wao Ndio wanaotegemewa
kuleta mabadiliko chanya.
Aidha aliwataka wanafunzi hao pia kuhakikisha wanatoa elimu na
kupinga vitendo viovu vya madawa ya kulevya kwa vijana sambamba na
kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia ambao ndio umeshamiri katika
jamii nyingi kutokana na mila na desturi zilizopo.
"nawaombeni jamani mkawe mfano wa kuigwa na muwe mabalozi wazuri wa
kabadilisha Jamii Kwa kutoa elimu Kwa vijana wenzenu juu ya vitendo
mbalimbali viovu, ili kupitia nyie tuweze kuona mabadiliko makubwa.
"alisema Bachu.
Kwa upande wa Mkuu wa shule hiyo, Godwin John alisema kuwa, shule hiyo
imekuwa ikiwandaa wanafunzi kufanya vizuri ikiwemo kutoa motisha kwa
wanafunzi wanaofanya vizuri pamoja na walimu ili kuongeza kiwango cha
ufaulu zaidi shuleni hapo.
Alisema kuwa, shule hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu
wa vioo vya vyumba vya madarasa, ukosefu wa madarasa, ulipaji ada wa
kusuasa hivyo kuwataka wazazi pamoja na walezi kuhakikisha wanawekeza
zaidi kwa watoto wao kwani huo ndio urithi pekee unaotakiwa kutolewa
kwa watoto.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Titi mzava aliwataka wanafunzi
hao kutobweteka na elimu hiyo waliyoipata badala yake wakawe mfano
bora wa kuigwa katika kuitangaza shule hiyo.
Aidha aliwataka wanafunzi hao pindi wanaporejea mtaani wakawe chachu
ya mabadiliko kwa vijana wenzao kupitia elimu hiyo waliyoipata.
No comments:
Post a Comment