HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 6, 2019

SIMAMIENI VIAPO VYENU: JAJI MSTAAFU SHANGALI


Na Mary Gwera, Mahakama Kuu-Iringa
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Mary Simbo Shangali ametoa wito kwa Majaji na Mahakimu waliopo katika Utumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia viapo vyao. 
Akizungumza na Waandishi wa Habari Aprili 05, 2019 mara baada ya hafla ya kuagwa rasmi kitaaluma, iliyofanyika Mahakama Kuu Iringa, Jaji Mstaafu Shangali alisema kuwa ni vyema kutekeleza majukumu kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu.
“Katika usikilizaji wa kesi ni vyema kumshirikisha Mungu na kusimamia viapo, hivyo tusicheze na mambo ambayo tumeapa mbele za Mungu tunapotekeleza majukumu yetu,” alieleza Jaji Mstaafu Shangali.
Aidha; Jaji Shangali aliwatia moyo Majaji na Mahakimu Wanawake  nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi na sheria zilizopo bila kuteteleka.
“Kuwa Jaji mwanamke kwa nchi zetu za Afrika si kazi rahisi kutokana na baadhi ya mila desturi zilizopo, kwa hiyo ni vyema wanawake kutekeleza na kusimamia haki bila kuteteleka,” alisema Jaji Shangali.
Kwa upande mwingine, Jaji Shangali alitoa wito kwa jamii kuelewa kuwa pindi unapokuwa na kesi Mahakamani kuna kushinda au kushindwa, hivyo ni vyema kukubaliana na matokeo.
“Haki sio kushinda bali ni kupata kile unachostahili, kudai kwamba umenyimwa haki sio lugha sahihi, lazima upande mmoja utashinda na mwingine utashindwa,” alisema Jaji Shangali.
Kwa upande wake Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania,  Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi aliyeongoza hafla hiyo alimuelezea Jaji Mstaafu Shangali kuwa alikuwa mchapa kazi na mara zote alisimamia haki.
“Jaji Mstaafu Shangali ni mfano mzuri wa wachapakazi, amefanya kazi vizuri na hadi kufikia mwisho hakuna jalada lolote la kesi aliloacha bila kukamilisha na huu ni mfano mzuri,” alisisitiza Jaji Kiongozi.
Jaji Mstaafu Shangali, alianza kazi Mahakama ya Tanzania mwaka 1983, ambapo katika utumishi wake alishika nafasi mbalimbali na hadi anastaafu Jaji Shangali alikuwa Jaji namba. 1 wa Mahakama Kuu ya Tanzania na vilevile Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, na kufanya jumla ya miaka 35 ya Utumishi wake ndani ya Mahakama.
Jaji Shangali ameishukuru Viongozi na Watumishi wa Mahakama kwa ujumla kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha utumishi wake.
 Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania,  Jaji. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa tatu kulia) pamoja na Majaji wenzake wa Mahakama Kuu wakijumuika kumuaga kitaaluma Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Mary Simbo Shangali (wa tatu kushoto).
 Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Messeka Chaba (kushoto) pamoja na Naibu Msajili, Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Agatha Chugulu wakiwa katika hafla hiyo.
 Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali wa Mkoa wa Iringa, Bw. Adolf Maganda (kushoto) pamoja na Wakili wa Kujitegemea, Mwakilishi kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bw. Rwezaula Kaijage (kulia) wakiwa katika hafla fupi ya Kumuaga Kitaaluma Jaji Mstaafu Mary Shangali.
 Mtendaji anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo nchini, Bw. Humphrey Paya (katikati) pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Bw. Elvin Mwakajinga (kulia) na sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kanda ya Njombe na wageni waalikwa wakiwa katika hafla ya kumuaga kitaaluma Jaji Mstaafu Shangali.
 Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi pamoja Wahe. Majaji wenzake akiwa katika picha ya pamoja Wanasheria wa Serikali mkoani Njombe waliohudhuria katika hafla hiyo,wa tatu kushoto ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Jaji Mary Shangali, wa tatu kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Panterine Kente, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji Dkt. Paul Kihwelo, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Immaculata Kajetan Banzi, wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Dunstan Ndunguru na wa kwanza kulia ni Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Bw. Adolf  Maganda.
 Wahe. Majaji pamoja na Jaji Mstaafu Shangali wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili, Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya-Iringa.
 Picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu-Iringa na Njombe.
Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa aliyepo uhamishoni kuelekea Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Immaculata Kajetan Banzi (kushoto) akimkabishi ua kama ishara ya pongezi kwa Jaji Mstaafu Shangali (kushoto), anayeshuhudia katikati ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi.

(Habari na Picha na Mary Gwera, Mahakama Kuu-Iringa)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad