HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 29, 2019

Mradi wa umeme wa Kinyerezi I Extension kukamilika mwezi Agosti mwaka huu

Na Teresia Mhagama

Imeelezwa kuwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi wa Kinyerezi I extension utakamilika mwezi Agosti mwaka huu ambapo utazalisha umeme wa kiasi cha megawati 185.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam tarehe 28 Aprili, 2019 na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya umeme ambapo aliambatana na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, Mhandisi Juma Mkobya  na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Tito Mwinuka.

Alisema kuwa, Kituo cha Kinyerezi I tayari kinazalisha megawati 150 hivyo kuongezeka kwa megawati 185 kutafanya kituo hicho kuzalisha umeme kiasi cha megawati 335.

Aliongeza kuwa, mradi huo wa Kinyerezi I Extension unatekelezwa kwa fedha za ndani ambapo jumla ya Dola za Marekani milioni 188 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo na malipo yamekwishafanyika kwa asilimia 60.85.

Awali, Meneja Miradi kutoka TANESCO, Mhandisi Stephen Manda alieleza kuwa, mradi wa Kinyerezi I Extension unahusisha ununuzi, usanifu na utengenezaji wa mitambo na viambata vyake, ujenzi wa laini ya msongo wa kV132 kutoka Kinyerezi hadi Gongo la Mboto na upanuzi wa ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme.

Alisema kuwa, tayari mitambo minne ya kuzalisha umeme itakayofungwa kwenye eneo hilo imeshafika nchini na kwamba mitambo miwili inatarajiwa kuwashwa na kuungwa kwenye gridi ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu na mitambo inayobaki itawashwa mwezi Agosti mwaka huu.

Alitaja baadhi ya kazi zilizokamilika hadi sasa kuwa ni ujenzi wa misingi ya mitambo, ujenzi wa kituo cha kupoza umeme na ujenzi wa laini ya msongo wa kV 220 kutoka katika mitambo ya umeme ya Kinyerezi I hadi Kinyerezi II, hivyo kwa ujumla mradi umetekelezwa kwa asilimia 82.

Awali, Waziri wa Nishati, alikagua kazi ya ufungaji wa transfoma kubwa yenye uwezo wa megawati 240 katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo kwa watendaji wa TANESCO kuwa kazi hiyo ikamilike tarehe Moja mwezi wa Saba mwaka huu ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Vilevile, Dkt. Kalemani alikagua kituo cha kupoza umeme cha Kurasini na kukuta kimeshakamilika hivyo kimeanza kazi ya kusambaza umeme katika eneo la Kigamboni hali itakayopelekea eneo hilo kupata umeme wa uhakika.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akitoka kukagua kazi ya ufungaji wa mitambo itakayozalisha kiasi cha umeme cha megawati 185 kupitia mradi wa Kinyerezi I Extension jijini Dar es Salaam.
Meneja Miradi kutoka TANESCO, Mhandisi Stephen Manda (wa pili kushoto) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) kuhusu utekelezaji mradi wa Kinyerezi I Extension utakaozalisha megawati 185. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.
Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, Mhandisi Juma Mkobya akizungumza na Mhandisi Edson Ngabo kutoka Wizara ya Nishati, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati katika mradi wa umeme wa Kinyerezi I Extension jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad