Wauguzi na wakunga Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wametakiwa
kuzingatia sheria na kanuni za kazi wakati wa kutoa huduma kwa
wagonjwa mbalimbali wanaotibiwa katika hospitali hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Afisa Muuguzi wa Baraza la Wauguzi na
Wakunga Tanzania (TNMC), Gustav Moyo kwenye kongamano la siku moja
linalofanyika katika Hospitali ya Muhimbili.
Moyo aliwataka wauguzi kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia
taaluma ya uuguzi na ukunga inayoitwa “The Nursing and Midwifery Act.
2010” pamoja na kanuni zake.
Pia, aliwataka wauguzi na wakunga kutowatelekeza wagonjwa wakati
wanapohitaji huduma kwa kuwa kumtelekeza mgonjwa ni kosa kwa mujibu wa
sheria na hivyo amewataka kuzingatia sheria na kanuni za kazi ili
kuboresha huduma mahali pa kazi.
“Wauguzi na wakunga mnapaswa kuzingatia upendo na huruma kwa wagonjwa,
ndugu na jamaa wa wagonjwa. Jambo muhimu mnatakiwa kuboresha
mawasiliano na kuzingatia maandili na kuwaona ndugu wa wagonjwa ni
wadau,” amesema Moyo.
Naye Happy Masenga katika kongamano hilo alisisitiza umuhimu wa
wauguzi na wakunga kujiendeleza katika mafunzo mbalimbali ili kuendana
na sayansi na teknolojia wakati wa kutoa huduma.
Katika mafunzo hayo pia wamefundishwa jinsi ya kujaza kitabu maalamu
(Log Book) ambacho kinasaidia upatikanaji wa leseni kwa wauguzi. Watoa
mada katika kongamano hilo ni Gustav Moyo, Happy Masenga na Asha Gembe.
Afisa Muuguzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC), Gustav Moyo akitoa mada kwenye kongamano la siku moja kuhusu sheria na kanuni za kazi kwa wauguzi na wakunga wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Baadhi ya wauguzi na wakunga wabobezi wakiwa kwenye kongamano la siku moja kuhusu sheria na kanuni za kazi kwa wauguzi na wakunga wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
No comments:
Post a Comment