Na Khadja Khamis - Maelezo Zanzibar
Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Mohamed Ali Ahmed amekemea
vitendo vya uvunjifu wa sheria vinavyofanya na baadhi ya wanachama wa
ACT Wazalendo na waliokuwa wafuasi wa CUF wanaomuunga mkono aliyekuwa
Katibu Mkuu Maalim Seif Sharifu Hamad .
Mohamed aliyasema hayo Ofisini kwake Mbweni wakati alipokuwa
akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu vitendo visivyo vya
kiungwana baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa hukumu ya Mgogoro wa
viongozi kwa CUF ambapo ilimthibitisha Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
kuwa Mwenyekiti halali wa Chama hicho.
Alisema Ofisi ya Vyama vya Siasa haitovumilia uvunjifu wa sheria na
kutumia dini katika masuala ya vyama vya siasa vinavyofanywa na
mashabiki wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa Maalim Seif Sharifu Hamad.
Aliwataka wanachama na wafuasi hao kuacha kufanya vitendo vya kuchoma
bendera za chama pamoja na kuhujumu mali za CUF kwani kufanya hivyo ni
kukiuka sheria za vyama vya siasa nchini.
Aidha alisema Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa haitomvumilia chama
chochote cha siasa kinachokiuka sheria ikiwemo matumizi ya dini kwa
lengo la kujinufaisha kisiasa.
“Suala la kutumia dini katika harakati za kisiasa halitapewa nafasi
katika zama hizi na atakayejishughulisha na vitendo hivyo atapambana
na mkondo wa sheria,” alisisitiza Naibu Msajili wa vyama vya siasa.
Alisema Sheria ya vyama vya siasa inatekeleza majukumu yake ya
kuhakikisha vyama vinaendeshwa katika misingi ya kistaarabu kwa lengo
la kuleta maendeleo ya wananchi.
Naibu Msajili wa vyama vya siasa alitoa wito kwa wananchi na wafuasi
wa vyama vya siasa kutii sheria za nchi na kutokubali kurubuniwa na
wanasiasa na hatimae kujiingiza katika matatizo ambayo hayaleti tija
yoyote kwa upande wao.
Naibu Msajili wa vyama Vya siasa Tanzania Mohamed Ali Ahmed akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu vitendo vya uvunjifu wa Sheria vinavyofanywa na mashabiki wa vyama vya Upinzani Zanzibar Ofisini kwake Mbweni Wilaya ya Magharibi B.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia maelezo ya
Naibu Msajili wa vyama vya Siasa Tanzania Mohamed Ali Ahmed alipokuwa
akizungumza katika ukumbi wa Ofisi ya Msajili ya Vyama vya siasa
Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Picha Na Miza Othman –Maelezo Zanzibar.
No comments:
Post a Comment