HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 14 March 2019

RC MWANRY AZINDUA JUKWAA LA SITETELEKI MKOANI TABORA

SERIKALI  imewatahadharisha vijana na kuwataka kuchukua tahadhari ya kupata maambukizi ya Ukimwi (VVU) na wachukue maamuzi sahihi yatakayowasaidia kutimiza ndoto zao za maisha.

Tahadhari hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri  wakati akizindua Jukwaa la Mawasiliano la Vijana (SITETELEKI) litakalotumika kuwaelimisha vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 kuzingatia afya ya uzazi na matumizi sahihi ya huduma hizo zikiwemo za Ukimwi kwa waathirika.

Alisema  vijana chini ya umri wa miaka 25 wanakabiliwa na hatari ya kupata maambukizi ya Ukimwi (VVU) na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao za maisha endapo hawatapata elimu sahihi ya afya ya uzazi na VVU, hivyo wafanye maamuzi sahihi kwa mstakabali wa maisha yao kupitia jukwaa hilo.
Mwanri alisema jukwaa hilo limeanzishwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ili kutoa elimu itakayowajengea uwezo vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 katika masuala ya afya na VVU, wajitambue , wabadilishe tabia na mienendo yao ili kuepuka kupata maambukizi mapya na mimba za utotoni .

Alieleza kuwa SITETELEKI itahamasisha matumizi sahihi ya kondomu, kupima VVU na kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi (ARVs), tohara ya hiari kwa vijana wa kiume na afya ya uzazi salama.
“Vijana ni kundi linalokabiliwa na changamoto za ongezeko la maambukizi mapya ya VVU na mimba za utotoni kwa sababu ya uelewa mdogo (elimu) na upungufu wa huduma rafiki za afya ya uzazi na VVU. Hivyo, serikali, jamii na wadau wana jukumu la kuwaelimisha vijana kujitambua , wakijitambua na kujali afya zao kutakuwa na matokeo chanya na watafanya maamuzi sahihi, hawatachezea afya zao,” alisema Mwanri.

Mkuu huyo wa mkoa alieleza zaidi kuwa jukwaa la  SITETELEKI  litawafanya wawe na afya na maisha bora, lengo la serikali ni kuwafikia wasijiinginze kwenye changamoto zinazohatarisha maisha yao ya baadaye na kuwahimiza waende vituo vya huduma za uzazi na kupima afya.
Aidha, aliongeza kuwa baada ya kujengewa uwezo  na kujitambua watatimiza azma ya serikali ya Tanzania ya uchumi wa kati wa viwanda kwa kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa inayotegemewa kwenye mchango wa uchumi  huo wa viwanda.

Hata hivyo, vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 sawa na asilimia 40 wana maambukizi ya VVU, kati ya hao asilimia 70 ya wasichana ndio wanaokabiliwa na hatari ya maambukizi mapya huku asilimia  41 ya vijana wa kiume wakizingatia njia za afya ya uzazi kutumia kinga kwa usahihi wakati wa kujamiiana.

Pia wasichana wanaopata huduma hizo ni asilimia 37, hivyo vijana wakijengewa uwezo watajitambua watasimama kwenye misimimo thabiti,watafuata maelekezo ya wataalamu wa afya  kupitia jukwaa hilo linalolenga kuimarisha afya ya jamii chini ya mradi wa USAID Tulonge Afya fhi 360.

 Kwa mujibu wa Mwanri serikali inajitahidi kuweka mazingira bora ya huduma ya afya ya uzazi kwa vijana na kuwafanya wawe sehemu ya mipango yake, hivyo lazima kuwe na huduma za viwango vya  kuwavutia na kuchochea fikra zao waende kwenye maeneo ya kutolea huduma.

 Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la “SITETELEKI” litakalozungumzia maswala ya Afya hususani Vijana chini ya mika 25 ili waweze kujitambua na kuwa na tabia chanya.Uzinduzi huo ulifanyika jana Mkoani Tabora.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry akipiga makofi kwa kushirikiana na baadhi ya wadau wa Afya maya baada ya kuzindua Jukwaa la “SITETELEKI” litakalozungumzi maswala ya Afya hususani Vijana chini ya mika 25 ili waweze kujitambua na kuwa na tabia chanya.Uzinduzi huo ulifanyika jana Mkoani Tabora.
Baadhi ya Vijana wa Mkoani Tabora wakimfuatilia Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry(hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la “SITETELEKI” litakazungumzia maswala ya Afya haswa kwa Vijana chini ya miaka 25 uliofanyika jana Mkoani Tabora.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad