HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 28, 2019

OSHA YAPONGEZWA KWA UTENDAJI

Wakala wa Afya na Usalama Mahala Pa Kazi umepongezwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kusaidia nguvu kazi iliyopo kutumika kuchochea maendeleo.

Akizungumza wakati wa semina kwa wabunge wa Kamati hiyo iliyofanyika Machi 27, 2019 katika Bungeni Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Mohamed Mchengelwa amesema kuwa  Wakala huo umeonesha mfano bora katika kutekeleza majukumu yake na pia kwa kuwajengea uwezo wabunge  kuhusu masuala ya usalama mahala pa kazi na umuhimu wake katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

 “Elimu tuliyopata ni muhimu kwetu na kwa wananchi hivyo pamoja na kazi nzuri mnayofanya ni vyema sasa elimu hii ikatolewa kwa wananchi wote na wabunge kwa ujumla ili kusaidia kupunguza athari zinazotokana na kukosekana kwa elimu kuhusiana na masuala ya Usalama Mahali Pa Kazi ikiwemo namna ya kutoa huduma ya kwanza,” alisisitiza Mchengelwa

Akifafanua amesema kuwa katika masuala ambayo Kamati hiyo imetoa ni pamoja na kuongeza kiwango cha utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana Mhe. Antony Mavunde amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wabunge wanapata uelewa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya OSHA.

Aliongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa wakuwajengea uwezo wabunge kama wawakilishi wa wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Lengo letu kama Serikali ni kuhakikisha kuwa tunalinda nguvu kazi iliyopo ili iweze kusadia katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na maendeleo ya Taifa kwa ujumla,” alisisitiza Mavunde

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi. Khadija Mwenda amesema kuwa wameandaa semina hiyo kwa wabunge ili kuwajengea uwezo wa kujikinga na athari za ajali au panapotokea mgonjwa anayehitaji kupata msaada wa huduma ya kwanza katika mazingira yao ya kazi na mengine yanayowazunguka.

Aliongezea kuwa OSHA itaendelea kutoa elimu kwa umma ili kujua namna bora za kujilinda na kujiepusha na madhara yanayoweza kuwapata wawapo kazini pamoja na mazingira yote yanayowazunguka kwa kuzingatia misingi ya elimu ya utoaji wa huduma ya kwanza endapo kunatokea dharula au majanga kazini.

“Tumejipanga kuwafikia watanzania kwa wingi wao ili kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya Usalama mahala Pa Kazi kwa kuzingatia unyeti wa masuala hayo kwani ni muhimu wananchi wakaelewa namna bora za kujilinda kuepuka madhara wawapo kazini,”alisema Bi.Mwenda

OSHA imekuwa ikiwajengea uwezo makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo wabunge na wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuilinda nguvu kazi iliyopo kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama Mahala Pa Kazi Bi. Khadija Mwenda akieleza umuhimu wa kuzingatia kanuni za kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa au mtu aliyepata ajali wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Machi 27, 2019 Jijini Dodoma.
 Mkurugenzi wa Mafunzo na Tafiti na Takwimu kutoka Wakala wa Afya na Usalama mahala pa Kazi (OSHA) Joshua Matiko akiwasilisha mada wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wabunge ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuongeza tija.
 Mkurugenzi wa Mafunzo na Tafiti na Takwimu kutoka Wakala wa Afya na Usalama mahala pa Kazi (OSHA) Joshua Matiko akiwasilisha mada wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wabunge ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuongeza tija.
 Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia semina ya kuwajengea uwezo kuhusu majukumu ya OSHA leo jijini Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. David Mathayo akichangia jambo wakati wa mafunzo hayo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad