HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 12 March 2019

MWENYEKITI WA UWT TAIFA AFANYA ZIARA KUSINI UNGUJA

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), umewataka Akina Mama wa Mkoa Kusini Unguja kutobweteka na hali ya kisiasa Mkoani humo na badala yake waandae mbinu imara za kulinda ustawi wa CCM.

Wito huo ameutoa Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka katika mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa huo alipokuwa akizungumza kwa wakati tofauti na wanawake wa UWT wa Wilaya mbili za Mkoa, huo ambazo ni Wilaya ya Kati na Wilaya ya Kusini Unguja.

Alisema licha ya Mkoa huo kusifika kwa kuwa ngome ya CCM Visiwani Zanzibar bado hakina Mama wana jukumu la kulinda heshima hiyo ili isichafuliwe na Vyama vya upinzani nchini.

Aliwasihi wanawake hao kuungana na kuhakikisha wanafanya kazi kwa pamoja katika kukiletea ushindi Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu ujao. Alisema mafanikio yaliyofikiwa katika Chama Cha Mapinduzi yametokana na juhudi kubwa za wanawake wa UWT wanaopigania maslahi ya taasisi hiyo usiku na mchana ili isonge mbele kimaendeleo.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Bi.Gaudensia alikemea vitendo vya udhalilishaji wa watoto katika Mkoa huo na kuiagiza taasisi za kisheria kuchukua hatua kwa watu wanaofanya uhalifu huo kwani unaharibu ndoto na malengo ya watoto ambao ndio taifa la leo na kesho.

Pamoja na hayo aliwakumbusha wanawake wa Mkoa huo kuhakikisha wanakuwa wanachama hai wa CCM kwa kulipia ada ili pindi pakitokea nafasi yoyote ya kuwania uongoi wake na vigezo sahihi vya kuingia katika ushindani wa nafasi hizo. Alisisitiza umuhimu wa UWT na CCM, kufanya uhakiki wa mara kwa mara wa wanachama ili kujiridhisha na kutambua takwimu sahihi za wanachama.

Awali aliwapongeza Viongozi mbali mbali wa Kitaifa wakiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa utendaji wao ulioiletea heshima kubwa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Alieleza kuwa Zanzibar imekuwa ni nchi yenye maendeleo endelevu kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kutoa huduma muhimu katika nyanja za kijamii,kiuchumi na kisiasa. "Wananchi nyote ni mashahidi juu ya mambo ya maendeleo yaliyotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi wa Dk.Shein.

Hatuna cha kuwalipa viongozi wetu kwa utendaji wao kwani nchi zetu zimepiga hatua kubwa za maendeleo,wananchi wameondoka katika wimbi la umaskini uliokithiri na kuwa na kipato cha kati kinachowawezesha kujikimu kimaisha.",alisema Mwenyekiti huyo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Thuwaiba Kisasi, alimwakikishia Mwenyekiti huyo kuwa Mkoa huo una historia ya kudumu ya wanachama wake kuwa wanachama wazalendo wenye misimamo imara isiyoyumba.

Akizungumza Katibu Mkuu wa Umoja huo Taifa, Mwl.Queen Mlozi alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM sambamba na maandalizi ya kongamano la kumpongeza Rais wa Zanzibar, na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kwa utekelezaju wake wa Ilani kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo alisema Akina Mama wa UWT wanajengewa uwezo juu ya masuala mbali mbali ya kimaendeleo ikiwemo ujasiriamali wajiajiri wenyewe.

Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kusini Unguja,Ndugu Shemsa Abdallah Ali alisema kuwa CCM imeendelea kuimarika kisiasa,kijamii na kisiasa. Alisema kuwa katika kupambana na Changamoto ya kujikwamua kiuchumi Akina Mama wamekuwa wakijiajiri wenyewe kupitia miradi mbali mbali ya vikundi vya ujasiriamali katika Mkoa huo.

Aidha Mwenyekiti huyo wa Umoja huo Taifa Bi.Gaudensia amewakabidhi wanachama wapya 338 kadi za UWT ,ambapo Wilaya ya Kati ni wanachama 188 na Wilaya ya Kusini wanachama 150. Sambamba na hayo Wilaya zote mbili pamoja na CCM Mkoa huo wamekabidhi Taarifa za Utekelezaji kwa Mwenyekiti huyo.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti huyo amekabidhi Mifuko 100 ya saruji kwa Hospitali ya Wilaya ya Makunduchi iliyotolewa na Wabunge na Wawakilishi wa Viti Maalum wa Mkoa huo. Sambamba na hayo Mbunge wa Jimbo la Paje Mhe.Jaffar Sanya Jussa amekabidhi shilingi milioni tano kwa Vikundi Vitano vya ushirika vya Jimbo hilo. 
  MWENYEKITI wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka akizungumza na Akina Mama Wajasiriamali wa Jimbo la Peje katika ziara yake Wilaya ya Kusini Unguja.
 MWENYEKITI wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka(kulia), akimkabidhi fedha shilingi milioni tano za vikundi vitano vya Jimbo la Paje zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Katibu wa CCM Wilaya ya Kusini Ndugu Hafidh Hassan Mkadam.
MWENYEKITI wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka akikabidhi Saruji mifuko 100 iliyotolewa na Wabunge, na Wawakilishi wa Viti Maalum wa Mkoa huo kwa uongozi wa Hospitali ya Wilaya iliyopo Makunduchi Unguja.


No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad