HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 20, 2019

KING KIKI ALIAPA KUFIA KATIKA MUZIKI

Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam

King Kiki ni mwanamuziki mwenye historia ndefu yenye mvuto wa kipekee, hajawahi kufanya kazi nyingine tofauti na muziki katika kipindi chote cha maisha yake.Licha ya kuonekana bado ana nguvu, mtanashati mwenye tabasamu wakati wote, amefikisha umri wa miaka 72.

Kiki amejijengea umaarufu kwa wapenzi wa muziki wa dansi, kila kona hapa nchini kwa kutoa burudani katika sherehe mbalimbali zikiwemo za Kitaifa.
Kiki aliingia hapa nchini kwa mara ya kwanza mnamo miaka ya 1970, alipofuatana na bendi ya Orchestra Fouvette toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wakati huo ilikuwa ikitwa Zaire.

Bendi hiyo iliyofanya maonesho yake ya muziki humu nchini ikiwa ya uongozi wa Fred Ndala Kasheba. Mwandishi wa makala hii alifanikiwa kufanya mahojiano maalum na nguli huyo nyumbani kwake Mtoni kwa Azizi Ali, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Katika mahojiano hayo King Kiki alieleza kwa undani historia ya maisha yake, ikiwamo ya muziki, mafanikio na njia alizopitia hadi kufikia hapo alipo. Akiwa na tabasamu tele usoni mwake, alianza kuelezea Wasifu wake akitamka majina yake kuwa anaitwa Kikumbi Mwanza Mpango.

Kiki alisema kwamba alizaliwa Januari 01, 1947 katika mji wa Lubumbashi uliopo katika mkoa Katanga huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). “Mimi ni mtoto wa tano kwa kuzaliwa toka kwa wazazi wangu mzee Katambo Wabando Paulino na mama yangu Mwanza Jumban Elia Maria…” alisema Kiki.

Alieleza kwamba akiwa na umri wa miaka sita akisoma shule ya awali mwaka 1952, kundi la muziki kutoka Afrika Kusini likiwa limeambatana na mwanamuziki mahiri Miriam Makeba ‘Mama Afrika’, lilifanya ziara nchini mwao. Kiki aliendelea kusimulia kwamba wakati huo alikuwa na kaka yake aliyemtaja kwa majina ya Koroumba Joseph.

“Kwa bahati nzuri kaka yangu alikuwa akinipenda sana, hivyo muda mwingi nilikuwa nikiongozana naye kwenye dansi, hususan mwishoni mwa wiki, hata kwenye onesho la Miram Makeba alinipeleka...” alisema King Kiki. Licha ya miaka mingi kupita hajamsahau kiongozi wa kundi hilo aliyekuwa anaitwa Dambuza Mulele.

Wanamuziki wengine wa kundi hilo walikuwa akina Sekena Kolaye, Tigizi Kwankwa, Dolira Jebe na mwenyewe nguli Miriamu Makeba. Miriam Makeba aliyekuwa akiongoza safu ya uimbaji kwa pamoja na wanamuziki wa kundi hilo, waliimba na kucheza kama vile hawana mifupa kwenye miguu na mwili kwa ujumla.

Kiongozi wao Dambuza Mulele, alikuwa na sauti nzito hivyo alikuwa ‘akichombeza’ maneno walipokuwa wakiimba kama afanyavyo Koffi Olomide katika baadhi ya nyimbo zake. Kiki alisema kwamba mwimbaji Miriam Makeba alipokuwa anaimba, alikuwa anaona kama jina hilo halikumstahili kuitwa.

Akawaza kama angelipewa fulsa ya kumtafutia jina linaloendana na hadhi yake. Kwa bahati nzuri wakati akiwaza hivyo, akasikia kiongozi wa bendi hiyo akipaza sauti akisema anapenda kumwita mwanamama huyo ‘Chocolate girl’. “Kwa kweli nimezunguka nchi nyingi kufanya muziki, nimeona shoo nyingi za Kimataifa, hakuna aliyewahi kuvunja rekodi ya kile nilichokiona siku hiyo kwa Miriam Makeba...” alisisitiza King Kiki.

Mwaka 1953 alipelekwa kwenda kuanza masomo ya awali akiwa na umri wa miaka sita. Baadae aliendelea na elimu ya msingi katika shule ya Officialle Laique de Kolwezi, ambako alimaliza darasa la saba mwaka 1959. Kikumbi alitamka kuwa wakati akiwa darasa la nne, baba yake aliyekuwa mfanyakazi katika kampuni ya madini inayotambulika kwa majina ya Gecamiou Athenee Royale kwa sasa, alipata uhamisho na kuhamia katika mji wa Likwasi huko DRC.

Wakati huo kampuni hiyo ilikuwa ikijulikana kama Union Miniere Du Hut Katanga. Kiki tangu zamani alikuwa anapenda sana kuimba, ambapo mwalimu wake akaliona hilo akamjumuisha katika vikundi vya ngoma na muziki shuleni hapo. Akawa anachukua utaalamu wa kucheza mitaani na kuupeleka shuleni, akawaunganisha wanafunzi wenzake watatu na kuanzisha kikundi cha muziki wa dansi wakiwa darasa la tano.

Walimu wake waliupenda muziki wao na jinsi walivyokuwa wakiimba na kucheza. Hivyo kila sherehe za shule waliitwa kutoa burudani. Sifa za umahiri wa kundi hilo zikavuma ikizingatiwa kwamba walikuwa vijana wadogo wanaofanya mambo makubwa. “Haikuishia hapo hata katika sherehe za watu wa karibu na shule yetu, wanafunzi waliokuwa na sherehe majumbani mwao walikuwa wanatualika tunakwenda kuimba na kucheza bure…” alisema King Kiki.

Alifafanua kuwa mbali na kupenda muziki, pia alikuwa mahiri katika masomo darasani. Kikumbi alijigamba kwamba hakuwahi kuwa mtu wa tatu kila anapofanya mtihani na akifeli sana alishika nafasi ya pili. Akiwa shuleni hapo, alikuwa akipendekezwa kufanya fani mbalimbali zikiwemo za maigizo, ngoma kuimba na kucheza.

Kiki wakati akiwa bado masomoni mwaka 1958, alijiunga na kikundi cha watoto wenzake cha Bantu Negro, waliweza kubadili muziki huo kwenda kwenye muziki wa rumba. Bendi ya Bantu Negro ilikuwa ikifanya maonesho ambayo watazamaji walikuwa wanaketi wakiwatazama na kusikiliza jinsi vijana hao wanavyo poromosha muziki wakitumia ala.

Mwanza Mpango alijiunga na masomo ya sekondari kidato cha kwanza katika shule ya Attene Iwayala, mwaka 1960. Kwa kuwa Kiki muziki ulikuwa umemtawala sana, mwaka 1962 ilimlazimu kuacha shule akiwa kidato cha tatu, akaanza kuimba rasmi mwaka huo. Hata hivyo alikuwa akikumbana na kizingiti kikubwa toka kwa wazazi wake ambao hawakupenda kabisa awe mwanamuziki, walimtaka aendelee na masomo shuleni.

King Kiki anakiri kuwa muziki ulikuwa umemuingia ndani ya damu, akawa akipigwa na wazazi wake ili aende shule, lakini hakubadili msimamo wake.
 “Kaka yangu alikuwa akinifunga kamba kwenye baiskeli huku akinikimbiza umbali wa Kilometa takriban 20, kama adhabu ya kutokwenda shule lakini yote hayo haikusaidia…” alitamka Kiki huku akitabasamu.

Alisema ukali wa kaka na wazazi wake alilazimika kutoroka nyumbani na kwenda kujihifadhi kwa marafiki zake. Usemi usemao kwamba “Uchungu wa mwana ajuwae mzazi” ulijidhihirisha pale wazazi wa Kiki kuaona kwamba kijana wao mwenye akili sana darasani ameshindikana. Baba yake alimuweka chini akamuuliza iwapo atakuwa tayari kufanya kazi nyingine yeyote tofauti na muziki.

Pasipo woga mbele ya baba huyo, Kiki alimjibu kwamba muziki umemteka sana na kwamba atakufa nao. Kwa majibu hayo baba yake akawa hana jinsi, ila alimbariki na kumtakia mafanikio mema katika muziki. “Baba aliposema hivyo, niliruka ruka kwa furaha, nikajihisi kama nilikuwa naelea katika dunia ya wapenda muziki…” anasema Kiki.

Mwaka 1964 akaenda mkoa wa Kasai ambako alijiunga na bendi ya Norvella Jazz. Katika mazungumzo hayo, Mwanza Mpango aliwataja wanamuziki wakongwe waliomfanya kubadili mfumo wa muziki akiwa katika bendi hiyo. Aliwataja akina Tchamala Joseph Kabasele ‘Grand Kale’, Tabu Ley na Fanco Luambo Makiadi.

Yeye pamoja na wanamuziki wenzake wa bendi ya Norvella Jazz, walilazimika kutafuta vyombo vingine vizuri vya muziki. Wakapita katika vikundi mbalimbali hadi wakafika mkoa wa Kasai (Mbudji Mai). Huko walikutana na vikundi mbalimbali kutoka mkoa wa Kinshasa vya African Jazz, Conga Success, Negro Success, Eco Bantu, African Fiesta vita na vingine mbalimbali, vilivyomfanya kupata uzoefu zaidi katika muziki wa rumba mwaka 1965.

Kiki alipiga muziki na bendi hiyo hadi mwaka 1967, lakini mara alipoondoka bendi hiyo ikasambaratika naye mwaka 1968 akarudi mkoa wa Katanga. Akiwa mkoani humo, alikutana na wanamuziki wa bendi ya Videt Jazz, iliyokuwa ikitoka nchini Zimbabwe. Mwanza Mpango alisimulia Kaka yake aliyekuwa na bendi yake, ilimzidishia hamasa katika muziki.

Aliwakumbuka baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakifanya kazi na kaka yake ambao ni Zapta Mfana, Kumaro Kadima, Andre Kaka na Joseph Kolomba. “Naweza kusema hao walinipa ujuzi mkubwa kwani nilijifunza kupiga vyombo pamoja nao, hapo ndipo nilipopenda kucheza, sikuwa mnene kama nilivyo sasa ungeniona ungefurahi…” alisema Kikii akiyatikisa maungo yake yaliyojaa minofu.

Alieleza kuwa ipo picha ya video iliyorekodiwa wimbo wa ‘Kasongo rudia’ wanaonekana yeye, Chinyama Chiyaza, Mtombo Lufungula, Mbuya Makonga, Kanku Kelly wakicheza kwa kupishana huku na kule wakati huo bado vijana. Kuna wakati Kikumbi alikuwa akipata mialiko ya huku na kule kiasi cha kutambuliwa na Wakurugenzi wa makampuni ambao walimuahidi kumpatia vyombo vya muziki.

Kwa ujasiri wa aina yake alikuwa akikataa. Hakuwa tayari kufanya kazi chini ya kampuni ya mtu, akijielekeza katika kutafuta njia ya kujikwamua mwenyewe kwa kutumia jasho lake.  “Nikiwa napiga muziki kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo, baadhi ya pesa nilizokuwa nikizipata nilipelekea kwa baba yangu kumuonesha kuwa muziki unalipa…” Kiki alitamka.

Hata hivyo wazazi wake pamoja na kuzipokea pesa hizo, bado walikuwa wakimshauri kwamba anayo nafasi ya kurudi shule kuendelea na masomo. Kauli hizo za wazee wake akaona bora awe mbali na nyumbani. Alikuwa mwanamuziki Fred Ndala Kasheba aliyemkaribisha King Kiki kujiunga katika bendi ya Orchestra Fouvette.

Alipojiunga na bendi hiyo Kiki alianza kuimba nyimbo mbili zilizotamba sana, nazo ni ‘Jacqueline’ na ‘Kamarade ya Nzela’ ambazo ndizo zilizompa nafasi ya kufuatana na bendi ya Fouvette kuja nchini Tanzania. Ikiwa hapa nchini bendi hiyo iliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi katika maonesho yao kadhaa.

Bendi hiyo baada ya kufanya maonesho hayo, ilirejea kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako waliamua kubadili majina, ikaitwa Safari Nkoi.
Mwaka 1977 Kikumbi Mwanza Mpango akiwa kwao DRC, alifuatwa na Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, aliyekuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa tayari ipo katika jiji la Dar es Salaam.

Kiki hukukurupuka kukubali bali alianza kumhoji Mzee Paul iwapo Wanamuziki waliopo Maquis du Zaire wanakidhi viwango? Majibu ya Mzee Paul yalionesha wasiwasi, ndipo yeye akapendekeza wachukuliwe wanamuziki wengine toka huko DRC.

Kiki aliwapendekeza wanamuziki wa kuondoka naye kuja nchini Tanzania akiwemo Nkashama Kanku Kelly, aliyekuwa akipuliza tarumbeta, Mutombo Sozy, aliyekuwa akizicharanga drums, Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’na aliyekuwa akipiga gitaa la besi.

Wakiwa safarini kuja nchini, walipitia mji wa Kamina, ambako walimpata mwanadada Ngalula Tshiandanda, aliyekuwa mnenguaji katika bendi ya Sakayonsa ya mjini humo. Bendi ya Maquis du Zaire wakati huo ilikuwa chini ya uongozi wa mwanamuziki Chinyama Chiaza ‘Chichi’.

Baada ya kutua Maquis, Kiki alianza kuonesha cheche zake baada ya kubuni mtindo wa Kamanyola, ambao baadaye ukawa gumzo katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake. Alieleza maana halisi ya Kamanyola akisema Kamanyola ni mji huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

“Nilitunga mtindo huo baada ya kujiunga na bendi hiyo mwaka 1977, niliongeza maneno ya ‘bila jasho’. Kwa maana mchezaji wa muziki huo atacheza taratibu kwa raha zake huku akijidai…” Kiki alifafanua. Mwaka huohuo  kulifanyika sherehe za sikukuu ya Wakulima kitaifa mkoani Mbeya. Bendi ya Maquis du Zaire ilialikwa kwenda kutoa burudani. Baada ya kurejea Dar es Salaam, walitunga wimbo wa ‘Safari ya Mbeya’.

Kwenye wimbo huo, sauti ya King Kiki inasikika akianza kwa kughani. Umahiri wa kutunga na kuimba Kiki aliedelea kuachia vibao vya ‘Nimepigwa Ngwala’, Kiongo na ‘Kyembe’. Baadhi ya nyimbo nyingine alizoshiriki kutunga na kuimba ni pamoja na Kasongo, Kibwe Mutondo, Sofia, Mokili, Yoka Mateya Babote, Dora mtoto wa Dodoma, Sababu ya Nini, Usinifiche siri, Noele Krismas na nyingine nyingi.

Bendi ya Maquis du Zaire iliingia nchini mwanzoni mwa miaka ya 1970 kwa mbwembwe nyingi ikipiga muziki kwa mtindo wa ‘Chakula chakula Kapombe’. Lakini ilikuja kusambaratika ikiporomosha muziki maridadi katika ukumbi wa White House, Ubungo jijini Dar es Salaam.

Safu ya waimbaji wenzake wakati huo walikuwa ni akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’,  Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clyton’, Mbombo wa Mbomboka, Tshimanga Kalala Assosa na Masiya Radi ‘Dikuba Kuba’. Safu hiyo ilikamilishwa kwa waimbaji Issa Nundu na Tabia Mwanjelwa.

Waswahili wanasema “Chema Chajiuza” Usemi huo ulijidhihirisha baada ya miaka miwili, akatafutwa na mfanyabiashara maarufu katika jiji hilo la Dar es Salaam, Hugo Kisima. Kisima alikuwa mmiliki wa ukumbi wa Safari Resort na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS), iliyokuwa na makao yake katika huko Kimara, jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo yao waliafikina kuondoka katika bendi ya Maquis du Zaire, akajiunga na OSS, baada ya ‘kumegewa’ kitita cha fedha. Baada ya kuingia OSS, alishirikiana vyema na waimbaji wa bendi hiyo akina Skassy Kasambula, Monga Stani Liki, Dingituka Molay, Mobali Jumbe, Kalala Mbwebwe, Tshibanda Sony na Kabeya Badu.

Aidha Kiki alitambulisha mtindo mpya wa ‘Masantula Ngoma ya Mpwita’. Pamoja na tungo zake nyingi kuna kumbukumbu zisizosahaulika katika enzi za mtindo wa Masantula. Kikumbi alipotunga na kuimba nyimbo za Mimi msafiri, Mama Kabibi na Kitoto kaanza tambaa, zilimletea sifa nyingi sana kwa wapenzi wamuziki wa dansi wakati huo.

Wimbo wa Mimi msafiri, alikuwa akijibashiria kuwa bendi hiyo ndiyo ingelikuwa ya kuzeeka nayo. Lakini mambo hayakuwa hivyo kwa kuwa aliamua kujikwamua badala ya kuajiriwa.

Mwaka 1982 alipata ufadhili toka kwa Dk. Alex Khalid, ambaye alisafiri naye kwenda Ujerumani kununua vyombo vya muziki. Aliporejea na vyombo hivyo vipya, ndipo alipoanzisha bendi yake ya King Kiki Double O’ iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Embalasasa shika breki’. Baadhi ya nyimbo walizotamba nazo ni  za ‘Kitoto kaanza tabaa, Dodoma Capitale , Pilikapilika Mtaa wa Samora, Lamanda , Malalamiko  Njigina, Salamule, Mtoto wa Elia, Sababu ya Nini na Malalamiko.

Mwaka 1997 bendi hiyo ilikufa kufuatia uchakavu wa vyombo vya muziki. Baada ya kusambaratika bendi hiyo, Kiki aliitumia talanta yake katika muziki akawa msanii mgeni au mwalikwa katika bendi mbalimbali. Moja kati ya bendi ambazo alikuwa akishiriki maonesho yao bila kuajiriwa, ilikuwa ni ya Orchestra Sambulumaa ‘Wana Zuke Muselebende’.

Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na mfanyabiashara Emmanuel Mpangala pamoja na mwanamuziki Chimbwiza Mbambu Nguza ‘Vicking’, aliyekuwa ameiacha bendi ya Maquis du Zaire. Kiki alifanya shughuli hiyo kwa takribani miaka minne, akaondoka kwenda kuungana na Fred Ndala Kasheba.

Kwa umoja wao wakaunda bendi ya Zaita Musica mwaka 1994, iliyokuja kuwa maarufu hususani baada ya kuachia wimbo wa ‘Kesi ya Kanga’. Hapo ndipo mtindo wa ‘Kitambaa Cheupe’ ulipozaliwa. Mwaka 2003 akiwa na Ndala Kasheba walianzisha bendi ya La Capitale ‘Wazee Sugu’.

“Lakini kwa mapenzi ya mungu mwenzangu Kasheba akafariki dunia mwaka mmoja baadaye, yaani 2004…” alisema Kiki. Bendi hiyo bado inauendeleza mtindo wa Kitambaa cheupe ambao umeiletea bendi yake wateja wengi wanaopenda muziki wa kistaarabu wakicheza na vitambaa vyeupe mikononi.

Alifafanua kitendo cha kuweka Kitambaa Cheupe ni kama ishara ya upendo na amani. Kikumbi alishirikana vyema na mtunzi na mwimbaji mahiri Baziano Bwetti, ambaye pia walikuwa wote katika bendi ya Orchestra Fouvette. Baada ya kuishi kwa muda mrefu humu nchini, aliamua kuomba Uraia wa Tanzania.

Kiki alizifuata taratibu zote za Idara ya Uhamiaji, hadi mwaka 1997, alipokubaliwa kuwa raia halali wa Tanzania. Kiki na bendi yake hiyo miaka ya 2000, walifanikiwa kwenda katika jiji la London nchini Uingereza, ambako waliporomosha muziki maridadi kwa Wantanzania waishio huko. Baada ya kurejea nchini, akatunga wimbo uliopewa jina la ‘Safari ya London’.

Katika wimbo huo uwalielezea jinsi safari yao ilivyofana wakiwataja baadhi ya watu waliofanikisha ziara hiyo wakiwemo baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza. Ukisikiliza mirindimo ya wimbo huo, hataitofautisha sana na ile ya wimbo wa ‘Safari ya Mbeya’. Baada ya kukongwa na nyoyo za baadhi ya mashabiki na wapenzi wake walimpachika majina ya ‘Bwana Mukubwa’.

King Kiki anayo imani kwamba bendi ya La Capitale ‘Wazee Sugu’ iliyoundwa mwaka 2003, ndiyo bora kwa muziki wa dansi kwa sasa. Alipoulizwa nini  kilichomshawishi zaidi kuwa mwanamuziki. Kiki alieleza kuwa alishawishika kuingia kwenye muziki akiwa na miaka sita, baada ya kumshuhudia mwanamama Miriam Makeba, toka Afrika ya Kusini alipofanya maonesho nchini mwake.

Kikumbi ‘aliifagilia’ bendi yake ya La Capitale iliyoundwa mwaka 2003, kuwa ndiyo bora kwa muziki wa dansi kwa sasa, na huenda ikawa ndiyo atakayozeekea nayo. Aidha Kiki aliweza kusimulia siri ya mafanikio ya kung’ara kwake akisema “…inawezekana kung’aa kwangu katika muziki kunatokana na nyota njema iliyojionyesha mapema, kwani nilizaliwa Januari Mosi, saa 11 alfajiri…” 

Akiainisha baadhi ya mafanikio aliyokwisha yapata katika muziki kuwa ni pamoja na kuweza kusafiri kwenda kufanya maonesho katika mataifa mbalimblai makubwa duniani likiwemo la Marekani. Kiki alitamka kuwa alipokuwa huko Marekani, aliweza kukidhi kiu ya Waafrika waishio huko alipoporomosha ‘bonge la shoo’ akiwashirikisha wanamuziki wa kundi la Soukuos Stars Lokassa ya Mbongo na Ngouma Lokito.

Aidha alisema ameweza kumudu maisha yake na familia kwa ujumla pia kumiliki bendi mbili nyingine ipo katika jiji la Mwanza. Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ni baba wa familia ya mke na watoto kadhaa. Kati yao ni binti mmoja pekee aliyefuata nyayo za baba yake katika uimbaji. Nguli huyo alionesha kujali ukweni kwake mkoani Mbeya, alipotunga na kuimba wimbo wa Barua.

Katika wimbo huo anaagiza kufikishiwa salamu afikapo Igulusi, Uyole, Makambako na kwingineko. Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ bado anaendeleza talanta yake ya muziki katika jiji la Dar es Salaam na kwingine anako alikwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad