HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 10 March 2019

KABAKA ATUA UNGUJA KUENDELEA NA ZIARA YAKE.MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka akipokelewa na Viongozi mbali mbali wa CCM na Jumuiya zake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Unguja akitokea Pemba.

Viongozi mbali mbali wa UWT Taifa wakiwa katika Chumba cha Wageni Mashuhuri(V.I.P),mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Unguja wakitokea Pemba.

WANACHAMA wa CCM na Jumuiya zake wakicheza kwa furaha katika mapokezi ya viongozi mbali mbali wa UWT Taifa kisiwani Unguja.
……………………………………………………………………….
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MWENYEKITI WA Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi(UWT) Tanzania Ndugu Gaudensia Kabaka leo amewasili Unguja kwa lengo la kuendelea na ziara yake ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 katika Wilaya mbali mbali za Unguja.

Ndugu Gaudensia mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, aliwapongeza Wanachama wa CCM na Jumuiya zake kwa mapokezi na maandalizi mazuri ya Kongamano la kupongeza Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa miaka mitatu ya Dk.Shein pamoja na ziara yake kisiwani Pemba.

Alisema kupitia ziara hiyo amejiridhisha kuwa Chama Cha Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar kina mtaji na azna kubwa ya wanachama hai wenye uwezo,uzalendo na uthubuti wa kusimamia maslahi ya taasisi hiyo bila kuyumba na kwa mafanikio makubwa.

Alieleza kuwa CCM inaisimamia Serikali zote mbili ya Zanzibar na Tanzania bara ziendelee kuwatumikia wananchi wa makundi yote bila ya ubaguzi kwa kuwasogezea huduma muhimu za kijamii, kiuchumi,kisiasa na kimaendeleo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo, alipongeza Mwenyekiti huyo na Ujumbe aliofuatana nao kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kukagua miradi mbali mbali ya CCM na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kisiwani Pemba.

Alieleza kuwa ziara hiyo imeleta mafanikio makubwa ya kisiasa kwani wanachama wengi hasa wanawake, wamehasasika na kutambua kuwa viongozi wa ngazi za Taifa wanawathamini na kuwajali.

Pamoja na hayo Naibu Katibu Mkuu huyo Ndugu Tunu, alisema Wanawake mbali mbali hasa Wajasiriamali wamejenga matumaini makubwa kwa kuungwa mkono juu ya kazi wanazozifanya za kuwaingizia kipato chao cha kila siku.

Awali Naibu huyo Tunu, alifafanua ratiba ya ziara ya Mwenyekiti huyo wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia, kuwa Machi 11, mwaka 2019 kuanzia saa 2:00 asubuhi atawasili katika Ofisi ya UWT Mkoa wa Magharibi na kuzungumza na Viongozi mbali mbali katika Wilaya ya Dimani kichama,ambapo saa 9:00 ataendelea na ziara yake katika Wilaya ya Mfenesini kichama kwa kutembelea miradi mbali mbali na kuzungumza na Wana CCM.

Machi 12,mwaka huu Mwenyekiti wa UWT Taifa ataendelea na ziara yake katika Mkoa wa Kusini Unguja kwa kukagua Utekelezaji wa Ilani katika Wilaya mbili za Mkoa huo.

Aidha ziara ya Mwenyekiti huyo itaendelea Machi 13, mwaka huu katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM sambamba na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo katika Wilaya mbili za Mkoa huo.

Sambamba na hayo ziara hiyo itahitimishwa katika Mkoa wa Mjini Machi 14,mwaka huu ambapo Mwenyekiti huyo atatembelea miradi mbali mbali katika Wilaya mbili za Mkoa huo pamoja na kushiriki shughuli mbali mbali za Ujenzi wa Taifa.

Mwenyekiti huyo ameambatana na Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Thuwaiba Kisasi, Katibu Mkuu wa UWT Mwl.Queen Mlozi pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa UWT Tanzania Bara Ndugu Jesca Mbogo na kupokelewa na Viongozi mbali mbali wa Chama na Jumuiya zote Tatu za UWT,uvccm pamoja na Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad