HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 9, 2019

AGA KHAN FANYENI MAPITIO YA GHARAMA ZENU-MAJALIWA

SERIKALI imeutaka Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), ufanye mapitio ya gharama za afya katika hospitali ya Aga Khan ili wananchi wa kawaida waweze kumudu na kunufaika na huduma za tiba wanazozitoa.

Imeelezwa kuwa pamoja na jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya, pia inatambua mchango unaotolewa na taasisi zisizo za Kiserikali ikiwemo Hospitali ya Aga Khan katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisasa.
Hayo yamesemwa leo (Jumamosi, Machi 9, 2019) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

Amesema upanuzi wa hospitali hiyo ni miongoni mwa jitihada za kuwafikishia Watanzania huduma za afya katika maeneo yao na kwa ngazi zote na kwa gharama nafuu, hivyo amewataka watoa huduma wote nchini waangalie upya gharama zinazotozwa katika huduma mbalimbali hususan za matibabu.

“Mtakubaliana nami kuwa gharama zikiwa kubwa hazitawanufaisha wananchi hususan wa kipato cha chini na wananchi hawataona unafuu wa kutibiwa nchini na nje ya nchi, hivyo fanyeni mapitio ya gharama hizo.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua gharama kubwa za uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za afya nchini hususan kwa sekta binafsi. “Lengo la Serikali na kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na mwitikio wa ni mkubwa na lengo lake ni kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya matibabu tena kwa uhakika.

“Nitoe wito kwa taasisi zote zisizo za Serikali kuunga mkono jitihada hizi za Serikali na kuhakikisha wananchi wote wananufaika na huduma zenu kupitia mfumo huu bila kubaguliwa.”

Pia ameutaka uongozi wa Hospitali ya Aga Khan na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakamilishe majadiliano yao katika matumizi ya NHIF kwenye hospitali hiyo ya rufaa. “Dr. Konga Mkurugenzi Mkuu wa NHIF upo hapa kamilisheni mjadala.”

Amesema nia ya Serikali ni kuona wananchi wanakwenda hapo kwenye jengo hilo zuri na wanapata huduma kupitia bima ya afya. “Ni matumaini yangu kwamba jambo hili litafanyiwa kazi kwa kuzingatia maslahi mapana ya pande zote mbili.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji, kuimarisha amani na utulivu, ambapo ametoa rai kwa sekta binafsi ziendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo nchini kwa kuzingatia sheria za nchi, utamaduni na mila za Watanzania.Awali, Waziri Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma katika jengo hilo ikiwemo maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya wazazi. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu sh. bilioni 192, kati yake sh. bilioni 134 ni mkopo wa muda mrefu wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameupongeza Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan kwa upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwani unakwenda kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya kutolea huduma za afya ambapo kwa sasa imeanzisha ushirikiano na sekta ya umma na binafsi kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.

NayeBalozi wa Ufaransa nchini, Balozi Frederic Claiver amesema awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali hiyo utasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya Tanzania.

Pia Balozi huyo amesema Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha inatimiza mkakati wake wa kukuza uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Binti Mfalme Zahra Aga Khan wakati alipowasili Kwenye hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali hiyo, Machi 9, 2019. Katikati ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Binti Mfalme Zahra Aga Khan (wapili kushoto) wakifungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi, 9, 2019. Wengine kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamaii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zaynab Chaula, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, (Agence Francaise de Developpment), Christian Yoka. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Binti Mfalme, Zahra Aga Khan (wapili kushoto) wakifurahia baada ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. Kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo yaJamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, (Agence Francaise de Developpment), Christian Yoka. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Baadhi ya waalikwa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza baada ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpokea mtoto Claribel Mwakatumbula (1) kutoka kwa mama ya Delfina Audax wakati alipotembelea wodi ya watoto katika hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam kabla ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali hiyo, Machi 9, 2019. Mtoto Claribel amelazwa hospitalini hapo kwa matibabu. (Picha na Ofisi ya Waziri Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa amembeba mtoto, Claribel Mwakatumbula (1) wakati alipotembelea wodi ya watoto kabla ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. Mtoto Claribel amelazwa hospitalini hapo kwa matibabu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimfariji mtoto Ilham Ally wakati alipotembelea wodi ya watoto kabla ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. Mtoto Ilham amelazwa hospitalini hapo kwa matibabu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wazari Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Jackline Vicent aliyejifungua mtoto Lois Ladislaus katika hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. Mheshimiwa Majaliwa alitembelea wodi ya wazazi kabla ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa haospitali hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Machi 9, 2019 amefungua awamu ya pili ya upanuzi hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam. Pichani ni jengo lililozinduiliwa.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua chumba cha kisasa cha upasuaji wakati alipofungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipita katika maeneo ya hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salam baada ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali hiyo jijini D, Machi 9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki katika sherehe za ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. Kulia kwake ni Binti Mfalme, Zahra Aga Khan na kushoto kwake ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Binti Mfalme Zahra Aga Khan baada ya kufungua awamu ya pili ya hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad