HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 22 February 2019

ZIARA YA MAKAMU WA RAIS YALETA NEEMA MANONGA

*Gulamali akabidhi gari la kubebea wagonjwa tarafa ya Simbo, ahaidi kusimamia sekta ya afya, elimu na miundombinu

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Tabora na kutembelea Wilaya zote saba (7) za  Igunga, Nzega, Uyui, Sikonge, Kaliua, Urambo na Tabora .

Katika  wilaya Igunga Makamu wa Rais alipokea taarifa ya utekelezaji ya Mkoa iliyowasilishwa na mkuu wa Mkoa wa Tabora  Aggrey Mwanri katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Igunga, na kukagua maendeleo ya ujenzi wa tanki kubwa la maji ikiwa sehemu ya utekelezaji wa mradi wa maji wa shilingi bilioni 600 ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 58.

Pia Makamu wa Rais alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya Simbo ambapo alipanda mti wa kumbukumbu na kuzungumza na wananchi.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Simbo katika jimbo la Manonga  Makamu wa Rais amesema kuwa, Serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha maji ya kutosha yanapatikana ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa uhuru na ufanisi zaidi. Pia amempongeza Mbunge wa jimbo hilo Seif Gulamali kwa juhudi zake za kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu hasa za afya, elimu pamoja na miundombinu.

Kuhusiana na suala la afya Wilayani humo imeelezwa kuwa, Wilaya hiyo ina Vituo 66 vya afya kati ya hivyo 55 vinamilikiwa na Serikali, huku vituo vingi zaidi vikizidi kujenga na kufanyiwa ukarabati.

Makamu wa Rais amehimiza Elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa bima ya afya ambapo Serikali inaandaa na mpango wa bima kwa wote na kuwataka wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya kutoa elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na kuhakikisha vitambulisho vya wajasiriamali vinatolewa kwa waliokidhi sifa na vigezo.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Manonga Seif Gulamali amekabidhi gari ya kubebea wagonjwa katika tarafa ya Simbo ikiwa ni moja ya utekelezaji ahadi yake ya kuhakikisha huduma za afya, elimu na maji ni muhimu na lazima jimboni humo.

Ikumbukwe kuwa mapema mwaka jana Gulamali alitembelea kituo hicho cha Simbo  pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati na kuahidi kuboresha zaidi sekta ya afya hasa kwa kujenga nyumba za wauguzi, maabara, vyumba vya kuhifadhia maiti na vyumba vya upasuaji katika hospitali jimboni humo.

Na amewata wananchi wa Manonga kutumia fursa zinazotolewa na Serikali hasa katika elimu pamoja na fursa iliyotolewa na Rais Dkt. John Magufuli kwa wajasiriamali kwa kutoa vitambulisho vitakavyowasaidia kufanya biashara zao bila bughudhi

Katika ziara yake Mkoani Tabora Makamu wa Rais aliambatana na Waziri wa Madini Doto Biteko, Naibu Waziri Maji  Juma Aweso, Naibu Waziri Ujenzi  Elias Kwandikwa na Naibu Waziri TAMISEMI Mwita Waitara.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akipokea kitabu cha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi cha jimbo la Manonga kutoka kwa mbunge wa jimbo hilo Seif Gulamali wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mikutano Simbo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Gari la kubebea wagonjwa lililokabidhiwa kwa wananchi ya tarafa ya Simbo na Mbunge wa Jimbo la Manonga, Kulia ni Mbunge wa jimbo hilo Seif Gulamali na kushoto ni Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad