HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 26, 2019

WATUMISHI WA UMMA NCHINI MARUFUKU KUTUMIKA KISIASA

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka watumishi wa umma nchini kutotumika kisiasa kwani uwepo wao una lengo mahususi la kuboresha utoaji huduma wenye viwango stahiki ikiwa ni pamoja na kuijenga Serikali ili iweze kuleta maendeleo kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Kisarawe ili  kujiridhisha na utekelezaji wa mpango huo. 
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, serikali inahitaji utaalam wa watumishi wa umma katika kujenga utumishi wa umma imara uliotukuka, utumishi ambao utaziwezesha taasisi za umma zote nchini kutoa huduma stahiki kwa wananchi. 
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa, hategemei kumuona mtumishi wa umma yeyote akijihusisha na siasa zinazosababisha kukwamisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa kuwasimamia kikamilifu Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri ili kujenga ushirikiano wa kiutendaji kati ya Makatibu Tawala wa Wilaya  na Wakuu wa Wilaya kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa umma. 
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amehimiza ushirikiano wa watendaji hao ili kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za serikali kwa ujumla, na kuongeza kuwa, serikali iliyopo madarakani ni moja tu inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, hivyo anashangaa inakuwaje Makatibu Tawala wa Wilaya wasiarifiwe masuala yanayoendelea katika halmashauri.

“Kuanzia sasa barua yoyote ya kiutendaji itakayotoka mkoani kuelekezwa kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, ni lazima nakala ya barua hiyo ielekezwe pia kwa Makatibu Tawala wa Wilaya ili wafahamu kinachoendelea na kumuarifu Mkuu wa Wilaya kufanya ufuatiliaji wa utendaji kazi’, amesisitiza Dkt. Mwanjelwa.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameyasisitiza yote hayo wilayani Kisarawe ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma Mkoani Pwani ambapo mpaka hivi sasa ameshakutana na watumishi katika Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe. 
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kabla ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani Kisarawe. 
 Baadhi ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani), wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao chenye  lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya Naibu Waziri huyo  kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani Kisarawe. 
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Jokate Mwegelo, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Halmashauri hiyo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na wananchi na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo. 
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akishuhudia baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wanufaika wa TASAF katika kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo. Aliyeambatana naye ni  Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Jokate Mwegelo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad