HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 27 February 2019

TGNP MTANDAO KUZUNGUKA NCHI NZIMA KUPINGA VITENDO VYA UKATILI WA KINGONO KWA WANAWAKE NA WATOTO

* Serikali yahaidi ushirikiano, yaasa wanajamii kushiriki katika kuwalinda watoto

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
KUTOKANA na kukithiri kwa vitendo cha unyanyaji wa kingono hasa kwa watoto na wanawake huku Mikoa ya Dar es Salaam na Iringa ikionekana kuongoza kwa vitendo hivyo,mtandao wa ujinsia nchini TGNP umezindua rasmi kampeni ya kupinga vitendo hivyo na kuhimiza kuwa watoto wote wana haki ya  kulindwa dhidi ya vitendo hivyo.

Akizindua kampeni hiyo Kaimu mkuu wa jeshi la Polisi na Mkuu wa dawati la jinsia nchini DCP Mary Nziku amesema kuwa kampeni hiyo ni ya nchi nzima na kila mmoja kwa nafasi yake awajibike katika kuwalinda watoto  dhidi ya vitendo hivyo hasa kwa wanaotendewa kutoa taarifa panapohusika na anayetenda makosa hayo achukuliwe hatua kali za kisheria.

Aidha amesema kuwa kuna madawati 420 ya jinsia nchini yanayotoa huduma pamoja na askari wenye mafunzo na serikali imechukua  hatua kadhaa ikiwemo kuwepo kwa huduma ya mkono kwa mkono katika hospitali ambapo muathirika wa vitendo hivyo hupata huduma zote kisheria na afya katika hospitali na kuwepo kwa ofisi ya ulinzi katika kata kote nchini.

Pia amewaasa wazazi kuzungumza na watoto wao na kuwakagua kwa kuwa vitendo hivyo hufanywa na watu wa karibu wakiwemo baba, wajomba na ndugu wa karibu zaidi. Vilevile amesema kuwa watakaotenda makosa hayo hatua kali za kisheria zitawachukuliwa mara moja na katika hilo hakuna ridhaa, kama mtoto alikubali ila yupo chini ya miaka 18 kosa hilo ni la ubakaji.

Pia amewaomba viongozi wa dini kushirikiana na Serikali na taasisi kama TGNP kwa kuweka ajenda ya mahubiri ya watoto ili kujenga uelewa na kuweza kujenga taifa ambalo halina maumivu. Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa TGNP Lilian Liundi amesema kuwa kampeni hiyo imelenga kuwakomboa watoto na wanawake dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono na kujenga taifa lisilo la makovu.

Lilian amesema kuwa viongozi wa Serikali akiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamekuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo vya unyanyasaji wa kingono na amewataka viongozi wengine kutumia vyema majukwaa katika kukemea vitendo hivyo vya kiudhalilishaji hasa mimba za utotoni na vitendo vya ulawiti.

Na amewataka wanajamii kushirikiana katika kampeni hiyo ambayo itaokoa maisha ya watoto wengi na kujenga taifa bora zaidi. 

Mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa jinsia nchini TGNP Lilian Liundi akizungumza wakati uzinduzi wa kampeni hiyo ya kupinga ukatili dhidi ya vitendo vya kingono kwa wanawake na watoto na amewataka wanajamii kushiriki katika kampeni hiyo ili kujenga taifa bora leo jijini Dar es salaam.
 Kaimu  Mkuu wa jeshi la polisi na Mkuu wa dawati la Jinsia nchini DCP Mary Nziku akizungumza wakati uzinduzi wa kampeni hiyo ya kupinga ukatili dhidi ya vitendo vya kingono kwa wanawake na watoto leo jijini Dar es Salaam.
 Wanafunzi na wazazi wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali zinazopinga vitendo vya ukatili katika uzinduzi wa kampeni ya kupinga vitendo vya ukatili wa kingono leo kwa wanawake na watoto leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa kampeni hiyo wakiwa katika kampeni hiyo ambayo imelenga kufika nchi nzima na kukomesha vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad