HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 25, 2019

IGP SIRRO KUZINDUA KAMPENI YA ULINZI WA MTOTO DHIDI YA UKATILI WA KINGONO

*Mikoa ya Dar es salaam na Iringa yaongoza kwa vitendo vya ukatili wa kingono.

*TGNP yajizatiti kushirikiana na Serikali katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kingono kwa wanawake na watoto ili kufikia malengo katika ujenzi wa taifa

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
MTANDAO wa ujinsia nchini (TGNP) umeandaa kampeni maalumu inayolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na athari za  ukatili wa kingono kwa watoto pamoja na kuwalinda dhidi ya ukatili wa aina hiyo na kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro Februari 27 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam muibuaji na mfuatiliaji wa wadau Janeth Mawinza amesema kuwa kampeni hiyo inaenda sambamba na kauli mbiu ya “Mlinde Mtoto afurahie utoto wake, ujana wake na uzee wake” na hiyo yote ni kutokana na kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto kuongezeka nchini ambapo tafiti zilizotolewa na kituo  cha sheria na  haki za binadamu nchini (LHRC) zinaonesha kuwa hadi kufikia Julai 2018 takribani watoto 394 wamebakwa kila mwezi huku ulawiti kwa watoto ukiongezeka kwa matukio 12 kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2017 hadi kufikia matukio 533 kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2018 katika maeneo mbalimbali nchini huku Mikoa ya Dar es salaam na Iringa ikiongoza kwa matukio ya aina hiyo.

Mawinza amesema kuwa kutokana na takwimu hizo ambazo si nzuri wakiwa kama mtandao wa ujinsia nchini wamesukuwa na kuona ni vyema kuja na kampeni ya ulinzi wa mtoto iitwayo 1-5-5 Namlinda, ikiwa ni ya kushirikiana kwa mtu mmoja kushirikisha watu watano zaidi na kuungana na Serikali katika kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya watoto kupitia mpango wa taifa wa kutokomeza vitendo hivyo dhidi ya wanawake na watoto ( MTAKUWWA) unaolenga kupunguza ukatili dhidi ya watoto na wanawake kwa asilimia 50 ifikapo 2022.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo imelenga kujenga nguvu za pamoja ya ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wa kingono na kuhakikisha kila mtu katika jamii anashiriki na  kuwajibika katika kumlinda mtoto, hivyo kampeni hiyo imelenga kuwafikia wanawake, wasichana, wavulana, wanaume, viongozi wa dini, serikali, vyombo vya habari, wadau wa afya, wanaharakati,  wabunge pamoja na watoa huduma za usafiri kwa umma wakiwemo bodaboda na daladala.

Kwa upande wake Mratibu wa kampeni hiyo Anna Sangai amesema kuwa kupitia kampeni hiyo jamii yote kupitia mtu mmoja mmoja na kikundi inapaswa kulinda na kuhakikisha ustawi wa jamii unaboreka zaidi na wameiomba Serikali kuu, serikali za mitaa na vyombo vya dola visimamie kikamilifu sheria ya kudhibiti uchawi namba. 12 ya mwaka 1998 (The Witchcraft Act) ambayo imeainisha adhabu kwa watu wanaoendesha vitendo vya kishirikina vinavyoweza kuwadhuru watoto na kuongeza vitendo vya ukatili wa kingono hasa ubakaji.

Aidha wameitaka serikali na wadau kuzijengea uwezo kamati za ulinzi kwa watoto ili waweze kutimiza majukumu yao ikiwemo kubaini maeneo ya hatarishi katika vijiji na mitaa pamoja na kupanga mikakati ya kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.


Pia wamevitaka vyombo vya habari kutoa elimu kwa wingi juu ya athari za ukatili wa kingono kwa watoto, faida ya kuwalinda watoto na kuendelea kukemea vitendo hivyo vya ukatili dhidi yao.
Anna Sangai (katikati) kutoka TGNP Mtandao akizungumza na wanahabari leo (hawapo pichani) kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi kuhusiana na uzinduzi wa kampeni ya ulinzi wa mtoto iitwayo 1-5-5 Namlinda itakayozinduliwa Februari 27. Kulia ni Muibuaji na Mfuatiliaji Miradi, Janeth Mawinza akiwa katika mkutano huo.
Muibuaji na Mfuatiliaji Miradi, Janeth Mawinza (katikati) akifafanua jambo kwa wanahabari leo (hawapo pichani) kuhusiana na uzinduzi wa kampeni ya ulinzi wa mtoto iitwayo 1-5-5 Namlinda itakayozinduliwa Februari 27. Kulia ni Rehema Mwateba mwanachama wa TGNP akiwa katika mkutano huo pamoja na Anna Sangai kushoto.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad