HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 19, 2019

HAMASA KWENYE UFUNDI STADI YAZIDI KUPANUKA

Wananchi Newala wakabidhi shule ya sekondari kwa VETA ibadilishwe kuwa chuo cha ufundi stadi. Katika kile kinachoonekana kuwa ufahamu wa umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi unazidi kuenea zaidi miongoni mwa Watanzania, Wananchi wilayani Newala wameamua kuibadilisha shule ya sekondari Kitangari iliyokuwa ikimilikiwa kupitia Mfuko wa Maendeleo wilayani Newala (Newala Development Foundation-NDF) kuwa chuo cha elimu na mafunzo ya ufundi stadi.

Baada ya kufikia maamuzi hayo, Bodi ya NDF imeamua kukabidhi umiliki wa shule hiyo kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), tayari kwa kuanza ukarabati na marekebisho mengine kuwa chuo cha ufundi stadi cha wilaya.

Makabidhiano ya shule hiyo yamefayika leo, tarehe 18 Februari 2019 kati ya Mwenyekiti wa Bodi ya NDF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Mhe. Chitwanga Rashidi Ndembo kwa upande mmoja na Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Mashariki, Joseph Mwanda aliyemwakilisha Mkuruenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu kwa upande mwingine.

Makabidhiano hayo yalishuhudiwa  na viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali, chama na dini, wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Capt. George Mkuchika, Balozi Prof. Abdillah Omari na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Newala, Mussa Chimae. 

Akizungumza kabla ya makabidhiano, Mwenyekiti wa Bodi ya NDF Mhe. Chitwanga Rashidi Ndembo alisema matarajio ya NDF na wananchi wa wilaya ya Newala baada ya kukabidhi shule hiyo kwa VETA ni kuona kuwa vijana wa wilaya hiyo na wilaya zingine za jirani, hususani Tandahimba wanapewa kipaumbele zaidi katika udahili baada ya chuo hicho kuanza mafunzo.

Balozi Mstaafu, Prof. Abdillah Omari alileta hamasa zaidi kwa watu waliohudhuria tukio hilo baada ya kuchambua kwa kina umuhimu na thamani ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi, baada ya kuombwa kutoa nasaha kwa niaba ya Mhe. Captain George Mkuchika, Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

Alisema, elimu ya ufundi stadi inapaswa kupewa kipaumbele kikubwa kwani ndiyo inayozalisha watu wa kwenda kutenda kazi na kusaidia katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

“kama kuna kitu kimetukwaza katika miaka hamsini iliyopita ni kutokuwa na wataalam wa kutosha katika ngazi hizi za ufundi wa kati. Na mwekezaji yeyote anayekuja, tena kabla ya kuja, anauliza technical force (nguvukazi ya kiufundi), haulizi mainjinia (wahandisi). Mwekezaji anauliza wale wanaofanya vitu kwa mikono. Wapo? Wanatosha?,” alifafanua.

Kwa kutambua umuhimu wa ufundi stadi, hasa kipindi hiki, Balozi Omari alipongeza uamuzi wa NDF kubadili shule ya sekondari kuwa chuo cha ufundi stadi na kusema kuwa ni uamuzi wa busara.

Akitoa shukrani kwa kukabidhiwa shule hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Mashariki, Joseph Mwanda, alisema kuwa VETA imepanga kuanza ukarabati na uboreshaji wa majengo ikiwemo kubadilisha majengo yaliyokuwa yakitumika kama maabara ili yaweze kuwa karakana kwa ajili ya kozi za awali ambazo ni uhazili na computa, ushonaji na umeme na kuongeza kuwa tayari shilingi milioni 220 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara, Joseph Kibehele alisema kuwa kuanza kwa mikakati ya ujenzi wa chuo cha VETA Newala ni faraja kubwa kwake kwani kutasaidia kupunguza changamoto ya uhitaji wa mafunzo ambayo chuo chake kilikuwa kikipata.

Alisema, wakati uwezo wa chuo chake ulikuwa ni kudahili takribani wanafunzi mia mbili (200), waombaji walikuwa wanazidi elfu moja (1000).
Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara, Joseph Kibehele akitoa neno wakati wa makabidhiano hayo ya shule ya Sekondari Newala kuwa Chuo Ufundi Stadi hafla iliyofanyika Newala mkoani Mtwara.
Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Mashariki, Joseph Mwanda akitoa neno wakati wa makabidhiano hayo ya shule ya Sekondari Newala kuwa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi hafla iliyofanyika Newala Mkoani Mtwara.
Mwenyekiti wa Bodi ya NDF, Chitwanga Rashid Ndembo akitoa neno wakati wa makabidhiano ya Shule ya Sekondari Newala kuwa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA hafla iliyofanyika Newala Mkoani Mtwara.
Balozi Mstaafu, Prof. Abdillah Omari akitoa nasaha wakati wa makabidhiano ya Shule ya Sekondari Kitangari kuwa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA hafla iliyofanyika Newala mkoani Mtwara.
Walioshikana mikono katikati, kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo Newala akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa VETA   Kanda ya Kusini Mashariki, Joseph Mwanda barua ya kukabidhi shule ya Kitangari kwa VETA ili ibadilishwe na kuwa shule ya sekondari. Wa nne kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika katika hafla iliyofanyika Newala mkoani Mtwara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad