HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 21, 2019

ZIARA TUMEJIFUNZA NA MAMBO MENGI SANA -MWAMUNYANGE

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya majisafi na majitaka Dar es Salaam (DAWASA) wamehitimisha ziara ya siku tatu ya kutembelea miradi mbalimbali inayosimamiwa na Mamlaka hiyo. Ziara hiyo iliyokuwa ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani imemalizika kwa Mwenyekiti wa bodi Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange kutoa tathmini ya jumla ya mambo waliyojifunza.

Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Jenerali Mstaafu Mwamunyange amesema wananchi wana matarajio makubwa na DAWASA ya kupata huduma ya majisafi inayoaminika. Mwamunyange amesema kwenye ziara ya siku tatu wamejifunza mengi sana na wameona ni namna gani DAWASA wanafanya jitihada kubwa kuhakikisha wanafikisha maji kwa wananchi wote ili kufikia malengo ya serikali.

Amesema kuwa,  pamoja na yote kuna changamoto zinazoikabili DAWASA ikiwa ni pamoja na kupasuka kwa mabomba kutokana na miundo mbinu chakavu na kupelekea kupotea kwa maji mengi na watu wanaojiunganishia maji kiholela kitu kinachopelekea Mamlaka kupoteza fedha nyingi sana. 

Ameeleza kuwa Changamoto nyingine ni majitaka na hilo linasababishwa na kuwa na maeneo machache yaliyokaribu na wananchi yanayopokea maji hayo na DAWASA wanaendelea kufanya jitihada za kujenga miundo mbinu itakayokuwa rafiki ikiwemo na kuleta magari yao yatakayokuwa yanachukua majitaka kwa bei nafuu.

“Mradi wa kuchakata majitaka ni jambo la msingi sana na utakuwa na faida kwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo jirani ila bado una changamoto kwani maji yanayozalishwa na kupelekwa kwa wananchi ni mengi tofauti na yale yanayoenda kuchukuliwa,”amesema Jenerali Mstaafu Mwamunyange.

Akizungumzia  miradi mbalimbali iliyojengwa na inayoendelea kujengwa na DAWASA, Mwamunyange amesema kuwa wananchi wanatakiwa kulipia bili za maji kwa wakati ili mamlaka iweze kupata kipato kitakachotosheleza na kuwekeza nguvu zaidi kujenga miradi kwa fedha za ndani.

Kwa upande wa Mjumbe wa Bodi wa DAWASA Mhandisi Gaudence Aksante amesema kuwa, lazima kuweka mkakati wa kupunguza upotevu wa maji ili Mamlaka kuongeza kipato na maji hayo yamekuwa yanapotea kutokana na mtandao wa zamani kuwa mdogo na kwa sasa maji ni mengi sana.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amepokea ushauri huo kutoka kwa bodi ya wakurugenzi ikiongozwa na Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange na watajitahidi kuhakikisha wanapanua mtandao wa maji ili kupunguza upotevu wa maji.

Ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ilitembelea miradi ya ndani ya Dar es Salaam na ile ya Mkoa wa Pwani ikiwemo mtambo wa uzalishaji maji wa Ruvu Juu na Ruvu Chini, Ujenzi wa matanki Bagamoyo, Changanyikeni, Kibamba, Kisarawe, maunganisho mapya ya wateja Salasala, mradi wa uchakataji majitaka Toangoma na mradi wa maji Kijichi, Kiwalani, Bonyokwa na maeneo mengine ya Jijini Dar es Saalam.
 Msimamizi wa Miradi ya Majitaka Mhandisi Charles Makoye akimuelezea Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange mradi mzima wa Kuchakata majitaka uliopo Toangoma Leo Jijini Dar es Salaam.
 Msimamizi wa Miradi ya Majitaka Mhandisi Charles Makoye akimuonesha Mkurugenzi wa Bodi ya DAWASA Jenerali Davis Mwamunyange na wajumbe wa bodi wa Mamlaka hiyo moja ya Chemba inayohifadhi majitaka katik mradi wa Kuchakata majitaka Toangoma Leo Jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa DAWASA Jenerali Davis Mwamunyange akisikiliza maelekezo kutoka kwa Msimamizi wa miradi DAWASA Mhandisi Charles Makoye mradi wa Kijichi unaohudumia wananchi wa eneo hilo leo Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange akionyeshwa eneo linaloanzia mradi wa Bonyokwa utakaohudumia wananchi kuanzia Kimara mwisho hadi Bonyokwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad